RC aigomea Halmashauri bajeti

14Feb 2016
Na Mwandishi Wetu
KATAVI
Nipashe Jumapili
RC aigomea Halmashauri bajeti

MKUU wa mkoa wa Rukwa, Said Magalula ameyagomea makisio ya bajeti ya Sh. 33 bilioni ya Halmashauri ya wilaya ya Sumbawanga mkoani Rukwa, kwa madai yapo chini na hayaendani na uhalisia wa vyanzo vya mapato vya halmashauri hiyo.

MKUU WA MKOA WA KATAVI, SAID MAGALULA

Mkuu huyo wa mkoa alikataa makisio ya bajeti hiyo wakati wa kikao cha baraza la madiwani kilichofanyika jana kwenye ukumbi wa Halmashauri hiyo uliopo mjini hapa.

Alisema kuwa katika bajeti hiyo ilionyesha vyanzo vya mapato vya ndani ni Sh. bilioni 1.8/-, kiasi ambacho hakiendani na vyanzo vya mapato vilivyopo kwa kuwa Halmashauri ina vyanzo vingi lakini makusanyo yake yamekuwa yakisuasua.

Alisema Halmashauri hiyo yenye vyanzo vingi vya mapato kama vile mazao ya kilimo na uvuvi kupitia ziwa Rukwa imekuwa ikipoteza mapato mengi kutokana na uzembe wa watendaji wake ambao wamejisahau katika kutimiza majukumu yao.

"Wapo baadhi yenu kwa makusudi wanaikosesha mapato Halmashauri hii, kwa kuingia mikataba mibovu ya ukusanyaji ushuru na mawakala wasio waaminifu ambao wanashindwa kuilipa fedha Halmashauri kwa wakati kadri mikataba inavyoelekeza" alisema.

Aliongeza kwamba katika makusanyo ya mwaka fedha 2014/15 watendaji hao wameshindwa kuwabana mawakala ili waweze kuwasilisha fedha zitokanazo na ushuru wa makusanyo mbalimbali zaidi ya Sh bilioni moja huku wakilalamika halmashauri kukosa fedha za kujiendesha.

Magalula alipendekeza kwamba ni vema watendaji wa Halmashauri hiyo wakafanya makisio sahihi ya bajeti kwa kila chanzo cha mapato ili kupata bajeti ambayo italeta tija kwa halmashauri hiyo na kupata maendeleo endelevu.

Pia aliwakata madiwani wa Halmashauri hiyo kutobweteka na kuaamini wataalamu pekee kwa kupitia taarifa hizo kiujumla jumla badala yake wajenge utamaduni wa kupitia kasma kwa kasma.

Naye, Mwenyekiti wa Halmashuri hiyo Kalolo Ntila alisema katika kipindi kifupi tangu wachaguliwe kuwa madiwani, wamebaini kuna mikataba mingi mibovu ambayo halmashauri imeingia na mawakala kiasi cha kuikosesha mapato halmashauri hiyo.

Alisema mikataba mingi ya ukusanyaji mapato imekuwa ikiwanufaisha mawakala kwani pamoja na kutakiwa kutoa amana fedha kabla ya ukusanyaji kuanza lakini wengi wao wamekuwa wakifanya makusanyo na Halmashauri haichukui hatua zozote dhidi ya mawakala hali ambayo inaonyesha kuna mchezo mchafu unaendelea baina ya mawakala na watendaji hao.

Naye, Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Adam Missana alisema kwamba wamepokea maagizo ya mkuu huyo wa mkoa na sasa wanajipanga kwa ajili ya utekelezaji.

Habari Kubwa