RC amkabidhi mwanamke zawadi bodaboda

15Jan 2022
Marco Maduhu
Kahama
Nipashe
RC amkabidhi mwanamke zawadi bodaboda

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema, amemkabidhi msaada wa pikipiki Darlen Athanasi (27), mkazi wa Segese wilayani Kahama, kwa ajili ya kufanya shughuli za bodaboda ili kumwingizia kipato.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema (kushoto), akikabidhi msaada wa pikipiki aina ya SanLG yenye namba za usajili MC 110 DCP yenye thamani ya Sh. milioni 2.4 kwa Darlen Athanasi mkazi wa Segese Msalala, wilayani Kahama, jana, kwa ajili ya kufanya shughuli za bodaboda ili kumuingizia kipato. Kushoto ni Kamanda wa Polisi wa mkoa huo, George Kyando. PICHA: MARCO MADUHU

Mjema alimkabidhi jana mwanamke huyo pikipiki hiyo yenye thamani ya Sh. milioni 2.4 ikiwa ni ahadi yake ambayo aliombwa kwenye mkutano wa hadhara, uliofanyika Segese mwaka jana.

Alisema alifarijika kwa ujasiri aliouonyesha mwanamke huyo wa kuamua kufanya shughuli za bodaboda, kwa ajili ya kujipatia kipato na kuendesha maisha yake kwa kutumia pikipiki ya kukodi, ndipo akaona ni vyema ampatie pikipiki yake mwenyewe.

"Namkabidhi pikipiki mwanamke huyu ambayo ataitumia katika shughuli zake za bodaboda na kuendesha maisha yake. Ni mwanamke jasiri sana ambaye habagui kazi na nimetimiza ahadi yangu ambayo aliniomba kwenye mkutano wa hadhara," alisema Mjema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, George Kyando, alimtaka mwanamke huyo akapitie mafunzo ya udereva na kumwahidi kumkatia leseni bure ili ajue sheria za usalama barabarani na kujiepusha na ajali.

Pia alimtaka akawe balozi mzuri wa kupinga matukio ya uhalifu pamoja na kutoa taarifa za wahalifu, akibainisha kuwa bodaboda huwa wanakutana na watu wengi, jambo ambalo litasaidia kukomesha uhalifu mkoani hapa.

Darlen alimshukuru mkuu huyo wa mkoa kwa kumpatia pikipiki hiyo akisema itamsaidia kuendesha familia yake kwa kuwa anaishi na watoto wake wawili na mama yake mzazi.

Habari Kubwa