RC amtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana

23Jun 2022
Neema Hussein
Nipashe
RC amtaka mkandarasi kufanya kazi usiku na mchana

Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko amemtaka mkandarasi anaetekeleza mradi wa maji Kibaoni halmashauri ya Mpimbwe wilayani Mlele M/S JEMASON INVESTMENT CO.LTD kuhakikisha anafanya kazi usiku na mchana ili ifikapo Juni 30 kazi hiyo inakamilika.

Mrindoko ameyasema hayo alipotembelea mradi huo wa maji Kibaoni kwenda vitongoji vya Ndemanilwa,Kakuni,Ushirika na Isamvu unaotekelezwa kwa fedha za UVIKO-19 ambapo amesema mkandarasi huyo ahakikishe hadi kufikia Julai mosi mwaka huu vituo vyote vinatoa maji.

"Hayo ndio maelekezo ya Mh Rais na nilazima yazingatiwe wala hakuna wa kuyabadilisha au kuyarekebisha,ni utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi lakini pia ni moja kati ya hatua za kuhakikisha wanamama na wanababa wanatuliwa ndoo kichwani kwa maana ya kupata maji katika umbali mdogo sana" alisema Mrindoko

Awali akitoa taarifa kwa mkuu wa Mkoa, Meneja RUWASA Wilaya ya Mlele Eng. Gilbert Isaac amesema changamoto kubwa iliyojitokeza ni mkandarasi kuchelewa kufika eneo la ujenzi kwa maana ya kuanza ujenzi,pia kasi yake ya kuendelea na utekelezaji wa majukumu yake kuwa ndogo kulinganisha na muda wa mkataba.

Hata hivyo amesema gharama za mradi huo ni milioni 706 ikiwa ni gharama za ujenzi wa tenki la maji lenye ukubwa wa lita 300,000 juu ya mnara wa mita 12, uchimbaji wa mitalo urefu wa km 11.2, ujenzi wa vituo vya kuchotea maji 11 kwa kijiji cha Kibaoni na kazi za uchimbaji wa mitalo.

"Mradi huu wa upanuzi ni mradi unaotumia kisima kirefu kilicho chimbwa mwaka 2011 chenye uwezo wa kuzalisha lita 22,000 kwa saa,ambapo awali tulikuwa tunatumia matanki mawili madogo yenye ujazo wa lita 90,000 hivyo kupelekea wananchi kutokuwa na maji ya kutosha"alisema Eng Issac.

Habari Kubwa