RC aomba kuingilia kati mgogoro ardhi

17Apr 2021
Gideon Mwakanosya
Namtumbo
Nipashe
RC aomba kuingilia kati mgogoro ardhi

WANANCHI kutoka koo 16 katika Kijiji cha Mchomoro, Namtumbo mkoani Ruvuma wamemwomba Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mdeme, kuingilia kati mgogoro wa ardhi wa zaidi ya ekari 700 kati yao na aliyekuwa Mkuu wa Wilaya hiyo, Luckness Amlima.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mdeme:PICHA NA MTANDAO

Kwa mujibu wa wananchi hao, kuendelea kwa mgogoro huo kumesababisha kuzorota kwa shughuli za kimaendeleo.

Wakizungumza na waandishi wa habari waliofika katika kijiji hicho juzi, wawakilishi wa koo hizo zenye takribani familia 70, walisema mgogoro huo umedumu kwa zaidi ya miaka minne sasa na kwamba viongozi wa kijiji na wilaya wamekuwa wakipuuzia kwa sababu zao binafsi, huku wakiwatuhumu kumpendelea kiongozi huyo mstaafu.

Mmoja wa wawakilishi wa koo hizo, Rashid Malamaye, alidai kuwa kiongozi huyo alivamia katika maeneo yao ya asili ambayo walikuwa wanayatumia kwa shughuli za kilimo na ufugaji kwa miaka mingi lakini cha kushangaza kwa sasa wanataka kudhulumiwa.

Malamaye alisema katika mashamba hayo kulikuwa na nyumba za nyasi lakini zimechomwa moto, mazao ya muda mrefu aina ya minazi, michungwa, migomba na mihogo na kwamba mazao hayo yamefyekwa bila wao kujulishwa na kuwekwa walinzi ambao wamekuwa wakiwapiga wananchi wanaokwenda katika mashamba hayo.

“Tumeshtushwa sana na kitendo hicho cha uharibifu wa mazao yetu na uvamizi wa mashamba ambayo yapo katika maeneo ya mahane katika kitongoji cha Nyerere na mwekezaji ambaye aliwahi kuwa mkuu wa wilaya bila sisi wenye maeneo kujulishwa. Hata tulipolalamika kwenye uongozi wa kijiji na wilaya, hakuna hatua zinazochukuliwa dhidi yake,” alisema Malamaye

Naye Issa Languka alisema kuwa baada ya kutokea kwa uvamizi huo, walitoa taarifa katika uongozi wa kijiji na kwenye uongozi wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) lakini majibu waliyoyatoa ni kwamba mwekezaji huyo yupo kihalali bila kufafanua sheria ipi au mkutano gani wa hadhara ambao ulihalalisha zaidi ya ekari 700.

Languka alisema inasikitisha kuona viongozi wa kijiji badala ya kulinda raia na mali zao, wamekuwa chanzo cha kutengeneza migogoro kinyume cha kiapo chao cha uadilifu.

“Kutokana na kitendo hicho, tumemwandikia Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christine Mdeme, kumjulisha madai yetu ili achukue hatua kwani mwenendo wa viongozi wa wilaya kuhusu mgogoro huu hauridhishi na hatuna imani nao,” alisema.

Habari Kubwa