RC aonya watakaobainika kuuza chanjo ya corona

05Aug 2021
Joctan Ngelly
Geita
Nipashe
RC aonya watakaobainika kuuza chanjo ya corona

MKUU wa Mkoa wa Geita, Rosemary Senyamule, amepiga marufuku hospitali za umma na binafsi kuwatoza wananchi fedha kwa ajili ya chanjo ya corona.

Akizungumza na wananchi kwenye uzinduzi wa chanjo hiyo uliofanyika jana kwenye ukumbi wa GEDECO mjini hapa, Senyamule alisema hospitali yoyote itakayogundulika ikiuza chanjo hiyo, itachukuliwa hatua kali za kisheria.

Senyamule alisema lengo la serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata chanjo ya corona ili kazi hiyo ifanyike kwa uadilifu na kwa haki na kwa walengwa wote kwa sasa.

Alisema kwa awamu ya kwanza mkoa wa Geita unatarajia kuchanja watu 50,000 katika vituo 18 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi ili kupata chanjo hiyo.

Pia alisema Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto inaendelea kuwashauri wananchi kuendelea kujikinga na corona kwa kunawa mikono, kwa kuvaa barakoa, kwa kukaa umbali wa mita moja au zaidi na kuepuka msongamano pamoja na kufanya mazoezi.

Alisema viongozi wa dini na wananchi kuendelea kuombea ugonjwa huu wa Uviko-19 uweze kuondoka hapa nchini ili watu waendelee kukuza uchumi wa Taifa.