RC apokea taarifa mzee  aliyetoweka miaka 10

23Jun 2022
Thobias Mwanakatwe
SINGIDA
Nipashe
RC apokea taarifa mzee  aliyetoweka miaka 10

MFANYABIASHARA maarufu wa mjini Singida anadaiwa kumteka na kumficha kusikojulikana kwa zaidi ya miaka 10 sasa, mtu aliyekuwa mfanyakazi wake, ambaye haijulikani kama yupo hai au amefariki dunia.

Mkoa wa Singida, Dk. Bilinith Mahenge.

Madai hayo yalitolewa jana na mkazi wa mkoani hapo, Omari Rashid mbele ya Mkuu wa Mkoa wa Singida, Dk. Bilinith Mahenge, kwenye mkutano wa kusikiliza kero za wananchi uliofanyika katika viwanja vya stendi ya zamani Manispaa ya Singida.

Rashid ambaye alidai ni mtoto wa mtu huyo aliyetekwa, alidai kuwa baba yao hajaonekana tangu mwaka 2010 baada ya mfanyabiashara huyo kumlaghai na kuchukua hati ya nyumba yao na kisha kuwafukuza katika nyumba hiyo na sasa wanaishi kwa kutangatanga.

Aliongeza kuwa mfanyabiashara huyo aliyemtaja kwa jina, alimrubuni baba yao kwamba atamlea na familia yake kwa kipindi chote cha maisha yao, lakini katika hali ya kushangaza, wamejikuta wakitimuliwa na mfanyabiashara huyo ambaye amejimilikisha nyumba yao iliyoko eneo la Majengo, Manispaa ya Singida.

Rashid alisema kinachowashanga na kujiuliza maswali yasiyo na majibu ni kwamba baba yao hajaonekana tangu mwaka huo hali inayowafanya waingiwe na hofu kama yupo hai au ameshafariki dunia.

"Mheshimiwa RC (Mkuu wa Mkoa), utatusaidiaje jambo hili ili tupate nyumba yetu na tujue hatima ya baba yetu alipo?" Alihoji.

Kufuatia ombi hilo, Mkuu wa Mkoa Singida, Dk. Mahenge alimwagiza Katibu Tawala wa Wilaya ya Singida na Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Singida, Lucas Mwakatundu, wachukue maelezo ya kina ya mlalamikaji huyo ili serikali iyafanyie kazi.

Dk. Mahenge aliwaagiza viongozi kuanzia ngazi za wilaya hadi chini kujenga tabia ya kuitisha mikutano ya wananchi na kusikiliza kero zao.

Alitumia nafasi hiyo kuwaeleza wananchi mafanikio mbalimbali yaliyofanywa na serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja wa uongozi wa Rais Samia, Mkoa wa Singida umepatiwa Sh. bilioni 230 kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, barabara, elimu na umeme.

Habari Kubwa