RC ataka wananchi kuendelea na maisha

21May 2020
Joctan Ngelly
Kigoma
Nipashe
RC ataka wananchi kuendelea na maisha

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga, amewataka wananchi wa mkoa huo kuendelea na maisha yao kama kawaida na kuwasikiliza wataalamu wa afya kwa kuvaa barakoa na kunawa maji tiririka.

MKUU wa Mkoa wa Kigoma, Emmanuel Maganga, picha mtandao

Maganga alitoa rai hiyo jana wakati akizungumza na wadau mbalimbali wa mkoa huo, baada ya kupokea misaada ya vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa corona pamoja na michango ya fedha kutoka kwa wadau hao jana eneo la Mnarani, Manispaa ya Kigoma/Ujiji.

Aliwataja wadau waliotoa msaada huo kuwa ni Sido, Adventure Connection, Kiwanda cha maji cha Tanganyika, Mamboleo Pharmacy, Turashashe Pharmacy, Kivuma Investment, Unicef, WHO na UNHCR.

Aliwataka wadau hao waendelee kutoa misaada kwa sababu ugonjwa huo utaendelea kuwapo hadi Mwenyezi Mungu atakapoamua kuuondoa.

Aliwataka waratibu wa misaada na michango kusimamia vizuri ili ilenge kwa watu wasio na uwezo, wazee, vijijini na wakimbizi.

Maganga alisema kwa hali wanayokwenda nayo ni nzuri hadi sasa Mkoa wa Kigoma una mgonjwa mmoja wa corona ambaye hali yake ni nzuri na anatarajiwa kuruhusiwa wiki ijayo.

Alisema jana kama walivyoagizwa na serikali waliwaondoa watu wote 60 kwenye karantini na wote walikuwa wametoka nchi za nje na watarudia kwenye utaratibu wa kawaida kwa wale watakao onyesha dalili watawaweka kwenye maeneo maalumu.

Aliwataka wananchi wa mkoa huo kuendelea na maisha yao ya kawaida isipokuwa wawasikilize wataalamu pamoja na kuvaa barakoa, kunawa maji tiririka kama walivyoanza mwanzo.

Kwa upande wake mtaalamu wa kushughulikia magonjwa ya mlipuko wa Shirika la Afya Duniani (WHO), Dk. Jairos Hiliza, alisema kazi yake kwa niaba ya shirika hilo ni kuangalia milipuko inavyo endelea katika nchi hususan Mkoa wa Kigoma.

Dk. Hiliza alisema shirika hilo limechangia Tanzania Sh. milioni 330 ambazo asilimia 70 ya fedha hizo tayari zipo kwa ajili ya mkoa kuendelea kuzitumia.

Habari Kubwa