RC atangaza kuwachapa viboko mabachela

19Oct 2019
Romana Mallya
Mbeya
Nipashe
RC atangaza kuwachapa viboko mabachela

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, ameibuka na jambo lingine kutishia kuwacharaza viboko waliofikisha umri wa kuoa na kuolewa lakini bado wako nyumbani.

MKUU wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila, picha mtandao

Kiongozi huyo anatoa kauli hiyo, wiki chache baada ya kuwacharaza viboko wanafunzi waliodaiwa kuchoma bweni la Shule ya Sekondari Kiwanja, wilayani Chunya.

Calamila aliyasema hayo juzi katika kijiji cha Godima wilayani Chunya na kueleza kuwa, wameanza kutumia bakora kwa kila jambo hata wakikuta mtu amekaa nyumbani haolewi wala kuoa.

"Hata tukikuta umekaa pale nyumba huolewi ni bakora tu. Nenda katafute mume muda wako wa kukaa hapo umetosha.

"Tumekuona umekaa hapo nyumbani hujaoa, ni bakora tu. Nenda katafute mke, kuna umri ambao unatosha lazima uchangamshwe, kwa hiyo viboko vinasaidia," alisikika katika video iliyorekodiwa katika mtandao wa kijamii wa ‘Youtube’.

Alisema hata baba na mama wakikosana bila watoto kuwaona wakijifungia ndani, wachapane wamalizane huko.
"Mkitoka nje mnasema kwa kweli kila mmoja anapukuta machozi mtoto haoni," alisema.

Oktoba 3, mwaka huu, mkuu huyo wa mkoa alitembelea Shule ya Sekondari Kiwanja na kuwachapa viboko wanafunzi 14 wanaodaiwa kuchoma moto mabweni mawili ya shule hiyo.

Akiwa shuleni hapo na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, Chalamila alichukua fimbo na kuwachapa wanafunzi hao, kitendo ambacho kilizua mjadala katika mitandao ya kijamii.

Oktoba Mosi, mwaka huu, mabweni hayo yaliyokuwa yakikaliwa na wanafunzi 150, yaliteketea kwa moto huku wanafunzi wakidaiwa kuhusika.

Siku nne baadaye, Rais John Magufuli akiwa kwenye ziara ya kikazi mkoani Songwe, alimpongeza Chalamila kwa kuwachapa wanafunzi hao na kuagiza wote wafukuzwe shule.

Akizungumza na wananchi, Rais Magufuli alisema alimpigia simu mkuu huyo wa mkoa na kumpongeza.

"Leo (Oktoba 3) nilikuwa naongea na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, nikamwambia ninakupongeza kweli kweli kwa kuwatandika wale viboko, nikamwambia uliwatandika viboko vichache.

"Haiwezekani serikali tunatoa mabilioni (ya shilingi) kujenga madarasa na shule halafu mtoto anakwenda kuichoma, nikamwambia hao watoto fukuza wote, kwa hiyo kidato cha tano na sita wa shule ile wote wamefukuzwa na bodi imevunjwa kwa sababu huo ni uzembe wa bodi ya shule,” alisema.

Habari Kubwa