RC awaonya walimu `mafataki’ kuwapa mimba wanafunzi

14May 2017
Rose Jacob
Nipashe Jumapili
RC awaonya walimu `mafataki’ kuwapa mimba wanafunzi

MKUU  wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, amemwagiza Mkuu wa Polisi wa Wilaya ya Ukerewe, Ignatus Kapila, kuhakikisha kesi zinazohusu wanafunzi kupewa mimba na ubakaji kwa watoto kufanyiwa kazi ndani ya wiki moja, kwa watuhumiwa kufikishwa mahakamani ili kutoa fundisho kwa watu wengine.

Mongella ametoa agizo hilo wakati akizungumza na wadau wa elimu wilayani humo kuhusu changamoto mbalimbali zinazoikabili Sekta ya Elimu katika wilaya hiyo, serikali itawachukulia hatua walimu watakaobainika kujihusisha kimapenzi na kuwapa ujauzito wanafunzi kwa kuwafukuza kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola.

“Wilaya ya Ukerewe inaongoza kwa kuwa na wanafunzi wengi wa shule za msingi na sekondari katika Mkoa wa Mwanza wanaopewa ujauzito na baadhi ya walimu wao, kitendo ambacho kinakatisha ndoto za maisha yao ya baadaye na kusababisha taifa kuwa na watu wasio kuwa na elimu ya kutosha…,” alisema.

Aidha, alimtaka Mkurgenzi wa halmashauri hiyo, Frank Bahati, kuhakikisha anapata taarifa za mahudhurio na maendeleo ya wanafunzi wa shule za msingi na sekondari za kila mwezi, ili kubaini mtoto mtoro na aliyepata ujauzito ili hatua zichukuliwe.

Katika hatua nyingine Mongella alimuagiza Mkuu wa Polisi wilayani humo, kumkamata Diwani wa kata ya Bwisha, Dismas Busanya na aliyekuwa Ofisa Mtendaji  wa kata hiyo, Ladislaus Mabagala, kufuatia tuhuma ya kushindwa kukamilisha nyumba ya mtumishi huku fedha zaidi ya Shilingi milioni sita, wakidaiwa kuzichukua.

“Haiwezekani watu waibe fedha halafu wabaki huru, kwanza kitendo cha kumdaganya Mkaguzi wa Mahesabu kuwa nyumba hizo zimeisha kamilika kinaonyesha wazi kuna wizi umefanyika, OCD hawa ni watu wako nenda nao ninachotaka ni fedha  za wananchi zirudi haraka hakuna kitu kingine watajua watazipata wapi, hayo ni majukumu yao,” alisema.