RC awaweka mtegoni wakurugenzi halmashauri

23Jan 2021
Gurian Adolf
Sumbawanga
Nipashe
RC awaweka mtegoni wakurugenzi halmashauri

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, amewapa siku tatu wakurugenzi wa halmashauri mkoani hapa kujieleza kwa maandishi ni kwa nini wameshindwa kutekeleza agizo la Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan.

MKUU wa Mkoa wa Rukwa, Joachim Wangabo, PICHA MTANDAO

Agizo hilo alilitoa Januari 19, mwaka huu, katika Kijiji cha Mollo, wakati akipanda miti ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Upandaji Miti mkoani hapa.

Wangabo alisema mwaka 2015 Makamu wa Rais aliagiza kila halmashauri nchini ipande miti walau milioni 1.5 katika kipindi cha mwaka mzima, lakini agizo hilo limeshindwa kutekelezwa katika halmashauri zote za mkoa wa Rukwa.

Alisema mwaka 2018/2019 halmashauri zote nne za mkoa wa Rukwa zilipanda miti milioni 2.5 sawa na asilimia 43 ya lengo na mwaka uliofuata zilipanda miti milioni 1.5 sawa na asilimia 26, na hali hiyo imekuwa ikishuka kila mwaka.

Wangabo alisema maelezo watakayotoa wakurugenzi hayo yawe ya maandishi pia waambatanishe na mpango kazi wa utekelezaji wa agizo hilo ili mkoa upande miti milioni sita katika kipindi cha mwaka mmoja.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Mazingira mkoani Rukwa, Kapteni (mstaafu) Zeno Nkoswe, alizishauri shule za msingi na sekondari kuanzisha mpango kazi wa upandaji miti ya matunda, hasa miparachichi.

Alisema iwapo kila shule itapanda miche 100 na kuitunza kwa kipindi cha miaka mitatu, inaweza kutoa matunda 500 kila mmoja na kila tunda likiuzwa kwa Sh. 500, watapata Sh. milioni 25 ambazo zitasaidia kuboresha miundombinu ya shule zao.

Habari Kubwa