RC Kagera ataka fedha za wakulima kurejeshwa

08Nov 2019
Dotto Lameck
Kagera
Nipashe
RC Kagera ataka fedha za wakulima kurejeshwa

MKUU wa Mkoa wa Kagera, Brigedia Generali Marco Gaguti, amewataka watumishi na taasisi zilizokopa fedha katika Benki ya wakulima iliyofungwa kuhakikisha wanarudisha fedha hizo ndani ya siku nne.

Brigedia Generali Marco Gaguti

Akizungumza na viongozi wa Chama Kikuu cha Ushirika Mkoa wa Kagera KCU, Chama Kikuu cha ushirika Wilaya ya Karagwe na Kyerwa KDCU, amesema kuwa kutokana na ufatiliaji amekuta zaidi ya shilingi bilioni 2 zimo mikononi mwa watumishi na taasisi ambazo bado hawajazirejesha baada ya kukopa.

Gaguti amesema chanzo cha benki hiyo kufungwa ni kutokana na ukopeshwaji wa fedha bila kufuata taratibu, hivyo wote waliokopeshwa wanatakiwa kurejesha fedha hizo ambazo ni mali ya wakulima.

“waliosababisha benki hiyo kufungwa ni watu waliokopa na kutokomea na fedha hizo hadi kupelekea benki hiyo kufilisika mpaka kufungwa, sasa nasema fedha hizo lazima zirudi nimefatilia nimeona wapo watendaji wanaoendelea na maisha kama kawaida zimo taasisi zinazoendelea na maisha kama kawaida huku fedha zilizokuwa za wakulima hazieleweki zilipo,” amesema Gaguti.

Ametoa angalizo kwa yeyote atakayeshindwa kurejesha fedha hizo ndani ya siku nne anatakiwa kujisalimisha kwenye kamati ya ulinzi na usalama ya Mkoa vinginevyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Hata hivyo, Gaguti amewataka viongozi wa vyama hivyo kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanampatia taarifa kuhusu namna rasilimali za vyama hivyo zinavyotumika na namna zinavyowanufaisha wakulima.

Habari Kubwa