RC Mahenge atembelea wamachinga Singida

21Sep 2021
Na Mwandishi Wetu
Singida
Nipashe
RC Mahenge atembelea wamachinga Singida

MKUU wa Mkoa wa Singida Dk. Binilith Mahenge, amefanya ziara katika masoko na mitaa ya Manispaa ya Singida ili kubaini hali halisi ya maeneo hayo na changamoto zinazo wakabili wafanyabiashara wadogo maarufu kama wa machinga.

Ziara hiyo iliyoshirikisha Kamati ya Usalama ya Mkoa na viongozi mbalimbali wa Manispaa hiyo ililenga kubaini maeneo yenye changamoto kwa wafanyabiashara wenye maduka na wanaopanga bidhaa barabarani.

Akiwa katika ziara hiyo Mkuu wa Mkoa huyo amewataka Wakurungezi na wakuu wa Wilaya kuhakikisha zoezi la kuwahamisha wafanyabiashara hao linafanyika kwa njia yamajadiliano badala ya kutumia nguvu.

Mahenge amesema mchakato wa kubaini maeneo mapya ya kufanyia biashara na mipango ya kufunga baadhi ya barabara kwa nyakati tofauti inafanyika ili kuhakikisha kila mfanyabiashara anaendelea na shughuli zake bila kubuguziwa.

Aidha, Dk. Mahenge amemshauri Mkurungezi wa Manispaa ya Singida mjini ashirikiane na vyombo vingine ikiwemo TARURA ili walete mapendekezo ya maeneo tarajiwa pamoja na mipango ya namna ya utekelezaji.

“Nashauri wafanyabiashara wa mjini ambao watatakiwa kupisha maeneo waliopo watafutiwe pengine upande wa huko mjini na wafanyabiashara wa mitaani watafutiwe maeneo karibu namitaa yao.” amesema Dk. Mahenge.