RC Malima aagiza Bodi ya Kahawa kutafuta wanunuzi

02Jun 2020
Na Mwandishi Wetu
MARA
Nipashe
RC Malima aagiza Bodi ya Kahawa kutafuta wanunuzi

BODI ya Kahawa imetakiwa kutafuta wanunuzi binafsi kadri iwezavyo ili kuongeza ushindani ili wakulima wauze Kahawa kwa bei nzuri isiyokandamizi.

Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima.

Kauli hiyo imetolewa leo na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima, alipokuwa akizungumza kwenye kikao kazi na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Prof.Jamali Adam ofisini kwake.

Amesema wanunuzi hao binafsi wataruhusiwa kununua kahawa kupitia Vyama vya Ushirika badala ya kwenda moja kwa moja kwa wakulima.

Amebainisha hatua hiyo itasaidia kukabiliana na unyonyaji dhidi ya wakulima wa kahawa pamoja na mazao mengine Mkoani Mara.

"Mkulima yoyote akisikia bei nzuri ya kahawa lazima atauza hawezi kwenda Kwenye bei ndogo wakati ameona kuna mahala kuna bei nzuri inayoendana na jasho lake,"amesema.

Amesema kuwa serikali iliamua kuanzisha Ushirika kwa ajili ya wakulima  kuuza mazao yao kwa bei nzuri hivyo wanunuzi binafsi ni ruksa lakini wanapaswa kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa.

"Uuzaji wa Mazao ya wakulima kupitia Vyama vya Ushirika tumeuweka ili kama wakulima wakiibiwa au kupunjwa sisi iwe rahisi kumpata muhusika na tunachukua hatua kali dhidi ya wote watakaofanya ubadhilifu, lakini tukimkuta mnunuzi binafsi ameingia mpaka shambani ni kama ameingia chumbani atapata balaa," amesisitiza Malima.

Amesisitiza kuendelea kutekeleza maagizo yaliyotolewa na Rais John Magufuli kuhusu wanunuzi binafsi wakati akizungumza na wananchi wa Kyaka, Rwamisheye, Kemondo Muleba, Nyakabango na Kyamyorwa mkoani Kagera Julai 11, 2019.

Sambamba na hilo, ameipongeza Bodi hiyo kwa kutoa Miche 40,000 kwa ajili ya mkoa wa Mara huku akiisisitiza umuhimu wa Bodi hiyo kuwaongezea wakulima miche mingi zaidi ili kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini.

Kwa upande wake,  Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Kahawa Tanzania, Prof.Jamal Adam, amesema kuwa Bodi ya Kahawa imejiwekea malengo muhimu ya kuongeza uzalishaji wa kahawa nchini, nakuwa na bei nzuri.

Amesema Bodi itaendelea kusimamia na kutekeleza maagizo ya serikali ikiwemo upatikanaji wa Miche Bora kwa wakulima na malighafi kwenye viwanda vya kahawa.

Amesisitiza  wakurugenzi wa Halmashauri mbalimbali nchini walioombwa vibali na wanunuzi binafsi na wenye viwanda kufanya hivyo kwa wakati ili Bodi iweze kutoa leseni.

Habari Kubwa