RC Mghwira amtaka Mbunge wa Siha aache uchonganishi

19Nov 2019
Mary Mosha
KILIMANJARO
Nipashe
RC Mghwira amtaka Mbunge wa Siha aache uchonganishi

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Anna Mghwira ametoa onyo kwa Mbunge wa Siha Dk Godwin Mollel, kuacha uchonganishi baina ya watumishi wa halmashauri, madiwani na wananchi kwa ujumla na badala yake awe kiunganishi ili kuleta maendeleo.

MKUU wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Anna Mghwira.

Inaelezwa kuwa tabia hiyo ya Mbunge ni moja ya sababu Halmashauri ya Wilaya ya Siha kuwa nyuma katika suala la ukusanyaji wa mapato na kufikia hatua ya kuwa ya mwisho miongoni mwa halmashauri nyingine mkoani humo.

Kauli hiyo ya Dk Mghwira ameitoa wakati akizungumza kwenye kikao cha kamati ya ushauri ya mkoa huo ambayo ilikuwa inajadili masuala mbalimbali ya maendeleo katika sekta za Elimu, Afya, Kilimo, Miundombinu na Ushirika.

“Sielewi ninyi wenzetu wa Siha mnakwamba wapi, mbunge nimekusikia ukuzungumza hapa kuhusu maendeleo ya wilaya yako lakini ninazo taarifa kuwa wewe ni sehemu ya tatizo, acha kuwachonganisha watendaji wa serikali, baraza la madiwani, kuwa kiunganishi, usiwe ni tatizo” amesema.

Amesema ukusanyaji wa mapato ya serikali za mitaa kwa mwaka 2018/2019 kwa baadhi ya halmashauri za wilaya siyo ya kuridhisha huku Wilaya ya Siha ikiwa nafasi ya mwisho kwa kukusanya kwa asilimia 65.

Amesema makadirio ya mapato kwa mwaka 2018/19 ilikuwa ni Sh Bil 19.1 kutoka kwenye vyanzo mbalimbali hadi mwezi Juni 2019 huku makusanyo halisi yakiwa ni Sh Bil 17.1 na kwamba Halmashauri ya Wilaya ya Mwanga imefanya vizuri kwa kukusanya Sh Bil 3.1 kati ya Sh Bil 3.03.

Kulingana na jedwali la ukusanyaji wa mapato, wilaya ya Siha ilikadiria kukusanya kiasi cha Sh 1.64 lakini ikakusanya kiasi cha Sh Bil 1.06 sawa na asilimia 65 ya lengo.

"Katika taarifa ya mkoa, inabainisha kuwa wilaya inayofuata kwa kufanya vizuri ni Moshi vijiji ambayo ilikadiria kukusanya Sh Bil 2.6 na ikafanikiwa kukusanya Sh Bil 2.6 sawa na asilimia 101, Halmashauri ya wilaya ya Hai iliyokadiria kukusanya Sh Bil 1.2 na kukusanya Bil 2.1 sawa na asilimia 87," amesema na kuongeza kuwa;

"Inayofuata ni Manispaa ya Moshi ilikadiria kukusanya Sh Bil 5.9 na ikafanikiwa kukusanya Bil 4.9 sawa na asilimia 84, Halmashauri iliyofuata ni Rombo iliyokadiria kukusanya Sh Bil 1.9 na ikakusanya Sh Bil 1.4 sawa na asilimia 74 na Same ilikadiria kukusanya Bil 2.5 na ikakusanya Bil 1.7 sawa na asilimia 70,"

Akichangia suala la ukuaji wa taaluma, Katibu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Basil Lema aliomba Serikali kubadili mitaala ya elimu nchini ili kuwafanya wahitimu wa elimu mbalimbali kuwa na uelewa katika kuleta mabadiliko na ugunduzi badala ya kukariri kujibu mitihani.

Amesema mitaala ya elimu iliyopo sasa inamuanda mwanafunzi katika kusubiri ajira serikali badala ya kujiajiri na kujitegemea katika kuendesha maisha na kuimua uchumi wa taifa kwa ujumla.

Wakati huo huo, Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, amekieleza kikao hicho kwamba zaidi ya wanafunzi 260 wa madarasa ya awali katika shule za msingi Kituri na Kilomeni wamelazimika kusomea katika majengo ya Zahanati ya Kituri baada ya shule zao kujaa maji kutokana na mafuriko.

Amesema mafuriko katika shule hizo yaliyosababishwa na kufurika kwa mto Ghona ambao unatenganisha Wilaya ya Moshi vijiji na Mwanga kujaa maji kasha kutawanyika katika mashamba na kuingia katika taasisi za umma na makazi ya watu.

Habari Kubwa