RC Mjema ahamasisha wananchi wajitokeze kuhesabiwa sensa

17May 2022
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe
RC Mjema ahamasisha wananchi wajitokeze kuhesabiwa sensa

​​​​​​​MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amewasisitiza wananchi wa Mkoa huo, kujitokeze kwa wingi kuhesabiwa katika zoezi la sensa ya watu na makazi, ili Serikali ipate idadi kamili ya watu wake ili iwe rahisi katika utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo.

Mjema amebainisha hayo leo Mei 17, 2022 wakati akitoa hotuba kwenye maadhimisho ya uhuru wa vyombo vya habari mkoani humo.

Amesema anawaomba wananchi wa Mkoa huo, siku ya zoezi hilo la kuhesabiwa sensa ya watu na makazi, ambalo litafanyika Agosti 23 mwaka huu, wajitokeze kwa wingi ili Serikali ifanikiwe katika mipango yake ya maendeleo.

"Waandishi wa habari nawaomba mtusaidie kutoa elimu ya kuhamasisha wananchi wa mkoa huu, siku ya zoezi la kuhesabiwa sensa ya watu na makazi ambalo litafanyika Agosti 23 mwaka huu wajitokeze kwa wingi," amesema Mjema.

Aidha, amewataka pia waandishi wa habari mkoani humo, wahamasishe wazazi kupeleka watoto wao kupata chanjo ya Polio ambapo zoezi hilo litafanyika mei 18 hadi 21 mwaka huu, ili wapate kinga dhidi ya ugonjwa huo wa kupooza.

Katika hatua nyingine Mjema, amewataka waandishi wa habari mkoani humo, wanapokuwa katika majukumu yao, wazingatie weledi wa taaluma yao pamoja na habari zao ziwe na uwiano kabla ya kuzitoa kwenye vyombo vyao.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari mkoani humo Greyson Kakuru, akizungumza kwenye maadhimisho hayo, amemuahidi Mkuu huyo wa Mkoa kuendelea kusimamia maadili ya waandishi wa habari ili wafanye kazi zao kwa weledi.

Pia, amewaomba viongozi wa Serikali mkoani humo, waendelee kuwa na ushirikiano na waandishi wa habari hasa pale wanapohitaji kufanya uwiano wa habari zao ili kutowapa ugumu wa majukumu yao na kuingia katika mafarakano.

Maadhimisho ya uhuru wa vyomba vya habari hufanyika kila mwaka Mei 3, ambayo kitaifa mwaka huu yalifanyika Jijini Arusha, na Mgeni Rasmi alikuwa Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassani, na Mkoani Shinyanga yamefanyika leo Mei 16 ,2022.

Habari Kubwa