RC Mndeme agawa vitambulisho vya wajasiriamali

21May 2020
Gideon Mwakanosya
RUVUMA
Nipashe
RC Mndeme agawa vitambulisho vya wajasiriamali

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amegawa vitambulisho 9,000 vya wajasiriamali wadogo kwa wakuu wa wilaya zote ili kusambaza kwa wafanyabiashara hao.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akimkabidhi Mkuu wa wilaya ya Nyasa Isabela Chilumba vitambulisho vya wajasirimali wadogo 1000 vilivyotolewa na Rais Mwaka huu.

Mndeme amegawa vitambulisho hivyo katika hafla fupi iliyofanyika nje ya  viwanja vya Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma mjini Songea na kushirikisha wakuu wa wilaya zote, Makatibu Tawala, Maafisa Tehama, Maafisa Biashara na Meneja wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Mkoa wa Ruvuma.

Akizungumza kabla ya kugawa vitambulisho hivyo Mdeme amesema, Rais Dk. John Magufuli ametoa vitambulisho hivyo na kwamba Mkoa wa Ruvuma umepangiwa jumla ya vitambulisho 58,000 na katika awamu ya kwanza vimeletwa vitambulisho 9,000 na katika  awamu ya pili mkoa utaletewa vitambulisho 49,000.

Amesema vitambulisho vitatolewa kwa wajasiriamali wadogo wenye sifa waliopo katika kila Halmashauri ambapo utaratibu wa ugawaji kwa mwaka huu ni wa  kutumia mfumo wa kompyuta  ili kuwawezesha  kutunza kumbukumbu ya wafanyabiashara na watoa huduma.

“Nawaelekeza maafisa Biashara kuhakikisha fomu ya maombi ya kitambulisho inajazwa na pesa inayokusanywa iwekwe Benki kila risiti moja ya malipo ya Shilingi 20,000 itatumika kusajiri mfanyabiashara mmoja,’’amesisitiza.

 Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akimkabidhi Mkuu wa Wilaya ya Songea Pololet Mgema vitambulisho wa wajasirimali 3500 vilivyotolewa na Rais mwaka huu.

Ameutaja mchanganuo wa  mgao wa vitambulisho hivyo mwaka huu katika awamu ya kwanza kuwa Wilaya ya Songea imepewa vitambulisho 3,500, Mbinga vitambulisho 2,000, Tunduru vitambulisho 1,500, Namtumbo vitambulisho 1,000 na Nyasa imepata vitambulisho 1,000.

 Awali akizungumza kabla ya kumkaribisha Mkuu wa Mkoa, Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Steven Ndaki amelitaja lengo la kuwagawa vitambulisho hivyo ni kuwarahisishia wafanyabiashara wadogo katika biashara ili waondokane na usumbufu hivyo kufanya kazi kwa ufanisi.

Naye Mkuu wa Wilaya ya Songea, Pololet Mgema  amesema mwaka jana Wilaya ya Songea Ilipewa Vitambulisho 15,000  ambavyo walifanikiwa kuvigawa vyote kwa wajasiriamali wadogo na kwamba mwaka huu wajasiriamali wadogo wanavisubiri vitambulisho hivyo kwa hamu kubwa.

 Mwaka 2019,Rais Dkt John Magufuli aligawa vitambulisho vya wajasiriamali wadogo 60,000 katika Mkoa wa Ruvuma ambapo hadi kufikia Mei 19, mwaka huu Mkoa ulifanikiwa kugawa vitambulisho 55,607 na kukusanya shilingi 1,112,135,000/=

Habari Kubwa