RC Mndeme:Ruvuma amebaki mgonjwa mmoja corona, anaendelea vizuri

19May 2020
Gideon Mwakanosya
SONGEA
Nipashe
RC Mndeme:Ruvuma amebaki mgonjwa mmoja corona, anaendelea vizuri

MKUU wa Mkoa wa Ruvuma, Christina Mndeme amesema hadi kufikia Mei 18,2020 Mkoa wa Ruvuma umebakiwa na mgonjwa mmoja wa corona  ambaye anaendelea vizuri.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Christina Mndeme akizindua mpango wa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na corona unaofanywa na REDCROSS

Mndeme  ametoa taarifa hiyo wakati anazindua mpango wa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na ugonjwa homa kali ya mapafu katika Mkoa wa Ruvuma ulioandaliwa  na Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania (RED CROSS).

Amesema hali ya kupungua kwa wagonjwa wa corona katika Mkoa wa Ruvuma inaendelea vizuri ambapo katika vituo nane vilivyotengwa kwa ajili ya kuwalaza wagonjwa wa corona,amebakia mgonjwa mmoja tu ambaye ataruhusiwa baada ya muda mfupi kwa sababu anaendelea vizuri.

“Mgonjwa huyu mmoja anaendelea vizuri kwa taarifa nilizopata leo asubuhi,tayari ameanza kufanya mazoezi mwenyewe bila kupewa msaada na daktari,hizi ni juhudi zinazoendelea kufanywa na Mkoa ili kumuunga mkono Rais wetu katika vita ya corona’,alisisitiza.

Ametoa rai kwa Chama cha Msalaba Mwekundu Tanzania,wanapokwenda kutoa elimu ya umma dhidi ya corona kuhakikisha kuwa ,wananchi wanapata elimu itakayowaondoa hofu ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa sahihi namna ugonjwa unavyoambukizwa na njia sahihi za kujikinga.

Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma akionesha mabango yatakayotumika na RED CROSS kwenye mpango wa elimu kwa umma dhidi ya corona.

 Amesema Mkoa wa Ruvuma una jukumu la  kumuunga mkono Rais Magufuli katika vita hii ya kupambana na Corona  kwa sababu amekuwa mstari wa mbele  kuhimiza wananchi kuchukua tahadhari ya kujikinga huku wakiendelea  kuchapa kazi .

Ameahidi kutoa ushirikiano na kwa RED CROSS  katika kuelimisha wananchi mkoani Ruvuma ambapo amewaagiza wakurugenzi katika Halmashauri zote kuhakikisha wananchi katika kata zote wanafikiwa na elimu hiyo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania  Mkoa wa Ruvuma  Judith Kapinga amesema mradi huo ni kwa ajili ya kuelimisha jamii kujikinga na homa kali ya mapafu ya corona ambayo imekuwa inasumbua Dunia nzima.

 “Kazi yetu kubwa katika mradi huu ni kuelimisha jamii kuhusu corona,tumeteuliwa na Wizara ya Afya kwa sababu tuna watalaam wa kujitolea katika nchi nzima’’,alisisitiza.

Amesema katika Mkoa wa Ruvuma program hiyo itagusa kata zote 173 zilizopo katika Mkoa wa mzima wa Ruvuma na watafanya mafunzo kwa kushirikiana na ofisi ya Mganga Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma ambapo katika kila Halmashauri yatatolewa mafunzo kwa watu wa kujitolea 12 ambao watahusika na zoezi zima la uelimishaji.

Hata hivyo amesema uelimishaji huo utafanyika kwa mtindo wa kubandika  mabango,kugawa vipeperushi vilivyotolewa na Wizara ya Afya na kutumia vipaza sauti ambavyo vitakuwa na ujumbe maalum wa kukabiliana na virusi vya corona.

Amesema vipaza sauti hivyo vyenye uwezo wa kusikika meta 500 vitatumika kuelimisha katika maeneo yenye watu wengi ikiwemo stendi za mabasi,minada,kwenye vituo vya afya  na maeneo mengine yenye watu wengi,lengo likiwa ni kuhakikisha   elimu sahihi ya kukabilina na corona inawafikia wananchi wengi katika maeneo yote.

Hata hivyo amesema Chama Cha Msalaba Mwekundu Tanzania Mkoani Ruvuma kimejipanga kuendelea na mafunzo hayo hata kama ugonjwa wa corona utatoweka nchini kwa sababu vifaa vya kutolea elimu vitaendelea kubaki katika maeneo husika na watalaam wataendelea kuwepo.

Naye Rais wa Chama Cha Msalaba Mwekundu  Tanzania David Kihenzile  ameutaja msingi wa kuanzisha chama hicho kuwa ni kusaidiana na serikali katika kutoa huduma za kibinadamu nyakati za vita ikiwemo njaa,ukame na magonjwa ya milipuko kama ilivyo sasa kwa mlipuko wa corona.

 Katika uzinduzi huo Chama hicho kimemkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma msaada wa vifaa vya kujikinga na maambukizi  ya Corona ambavyo ni  vitakasa mikono,sabuni ya kunawia mikono na machine tatu za kunawia mikono.

Ugonjwa wa homa kali ya mapafu upo duniani kote ,unahitajika mkakati wa pamoja kwa ajili ya kukabiliana ikiwemo utoaji wa elimu sahihi kwa umma namna ya kujikinga na ugonjwa huo.

Habari Kubwa