RC Mrindoko awafunda wanafunzi chuo cha afya

14Jan 2022
Neema Hussein
Katavi
Nipashe
RC Mrindoko awafunda wanafunzi chuo cha afya

MKUU wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko, amewataka wanafunzi wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Mpanda kusoma kwa bidii ili waepuke udanganyifu kwenye mitihani.

Amesema hayo alipokuwa akizungumza na wanafunzi pamoja na watumishi wa chuo hicho, mara baada ya kukabidhiwa madarasa yaliyojengwa kwa ufadhili wa Shirika la Christian Social Services Commission (CSSC).

Mrindoko amesistiza kitengo wanachosomea cha afya ni nyeti kwa maisha ya binadamu na hivyo hakihitaji udanganyifu katika mitihani hiyo.

Ameipongeza pia wizara ya afya ambayo inaongozwa na Waziri Ummy Mwalimu, katika kuhakikisha chuo hicho kinafanya kazi kwa mara nyingine ikiwa ni baada ya kufungwa kwa miaka mingi.

"Nichukue nafasi hii kuwaomba wizara ya afya kuendelea kukisimamia chuo hiki tukishirikiana na sisi watumishi wa mkoa kuhakikisha watumishi wanapatikana kwa idadi inayotakiwa ili masomo yaweze kutolewa vizuri," amesema Mrindoko.

Kwa upande wake Mkuu wa Chuo hicho, Lightness Maiko, amesema chuo kinakabiliwa na tatizo la upungufu wa walimu, vitabu vya kufundishia, madarasa na ofisi za walimu.

Amesema chuo kina walimu 10 na wanafunzi 119 ndani ya walimu hao saba ni wa kudumu na watatu ni wa muda.

"Chuo hiki kilianza mwaka 1974 kikasimama mwaka 1996 baada ya hapo kwa juhudi ya wizara ya afya na ofisi yako kikaanza tena mwaka juzi mwaka 2020 kwa kuanza na wanafunzi 50," amesema.

Kwa mujibu wa Askofu Eusebius Nzigirwa, kutoka Dayosisi ya Katoriki Mpanda ambaye amewawakilisha maaskofu kutoka (CSSC) amesema wanatoa huduma za kijamii ambazo ni wito uliotoka kwa Mungu wa kumuhudumia mwanadamu kiroho, kimwili na kiakili.

"Sisi tumekuja kuwakilisha wenzetu kukabidhi darasa jipya na maabara iliyokarabatiwa kwa marafiki na wadau wa CSSC sisi tunafanya huduma zetu na tunahitaji msaada wa kiserikali na muda wote tumekuwa tukifanya nao kazi na ni wadau wakubwa wa serikali," amesema Askofu Nzigirwa.

Meneja wa benki ya NMB Kanda ya Magharibi Sospeter Magesse, amesema wamekabidhi meza 100 na viti 100 vyenye thamani ya Milion 10/- ambavyo vitatumiwa na wanafunzi kwenye darasa lililojengwa.

"Benk yetu imeendelea kuyafanya haya na siyo mara ya kwanza, benk yetu imekua ikitenga asilimia moja kila mwaka kuipeleka kwenye sekta ya afya na elimu sababu tunajua tukiwa na taifa lenye afya tutafanya maendeleo na tukiwa na watu wenye elimu ndio tutafanya maendeleo kwa hiyo afya na elimu ni sekta za kipaumbele," amesemaMagesse.

Wanafunzi wa chuo hicho wametoa shukurani kwa serikali na wadau wote waliochangia kufanikisha zoezi hilo, hivyo wameomba serikali kuwaongezea walimu hasa katika sekta ya wauguzi.

Habari Kubwa