RC Mtaka alipa angalizo Jeshi la Polisi

26Jan 2021
Happy Severine
Bariadi
Nipashe
RC Mtaka alipa angalizo Jeshi la Polisi

MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka, amevitaka vyombo vinavyohusika na ukamataji wa watuhumiwa na kupeleleza kutenda haki pamoja na kutanguliza utu.

Alisema wakati mwingine haki inakosekana kwa watuhumiwa kutokana na vyombo ambavyo vinahusika katika ukamataji na upelelezi kutotekeleza majukumu yao kwa haki pamoja na kutokuwa na utu.

Alisema hayo jana wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Sheria na maadhimisho ya miaka 100   ya mahakama mjini Bariadi.
Mtaka alilitaka Jeshi la Polisi kubadilika katika utendaji kazi wake, kwani haki ya mtuhumiwa huanza kupotea kwenye eneo lao kabla ya kufikishwa mahakamani, hali ambayo watu wengi wamefungwa bila ya hatia.

Alisema malalamiko ya watu kusingiziwa na kubambikizwa kesi mbalimbali yamekuwa mengi na Jeshi la Polisi limekuwa likilalamikiwa kwa tabia hiyo na kuwataka kubadilika ili haki iweze kutendeka.

“Ikiwa mkamataji na mpelelezi wakisema uongo, hapo hakuna haki hata kidogo, wala hakimu au mahakama inaweza kushindwa kupata ukweli ikaonekana uongo wa polisi ndiyo ukweli na mtu akapewa adhabu kumbe siyo kweli.

“Misingi ya haki na utu ianzie kwenye Jeshi la Polisi, hawa ndiyo wahusika wa awali kabisa kwenye kesi yeyote, kama hivyo vitu havitakuwapo ni ngumu mtu mnyonge kupata haki, ni vyema polisi mkabadilika kwenye hilo,” alisema Mtaka.

Awali akizungumza kwenye uzinduzi huo, Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Shinyanga,  Gerson Mdemu, alisema katika wiki hiyo watu watapata fursa ya kupewa elimu ya jinsi mahakama inavyofanya kazi kwa haki.

Jaji Mdemu aliongeza kuwa wamepanga kutumia wiki hiyo kuwafikia watu wote kwenye maeneo ya minada na magulio lengo likiwa kila Mtanzania kupewa elimu ya sheria pamoja na kutambua utendaji kazi wa muhimili huo wa nchi.

“Wananchi mnatakiwa kujitokeza kwa wingi kupitia maadhimisho haya, kwa wiki nzima tutakuwa hapa Bariadi, tutakwenda kwenye minada na magulio, hivyo tunaomba mjitokeze kwa wingi mkapate elimu hii,” alisema Jaji Mdemu.

Habari Kubwa