RC Mwangela amzuia Mkandarasi kutoka nje ya Mkoa

07Apr 2020
Dotto Lameck
Songwe
Nipashe
RC Mwangela amzuia Mkandarasi kutoka nje ya Mkoa

MKUU wa Mkoa wa Songwe Brig. Jen. Nicodemus Mwangela, ameliagiza Jeshi la Polisi kumzuia Mkandarasi wa Mradi wa maji wa Iyula Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe kutoka nje ya Mkoa huo mpaka atakapo kamilisha vifaa na wataalam watakaomalizia mradi huo.

Mwangela ametoa zuio hilo leo mara baada ya kutembelea Mradi wa maji wa Iyula wenye thamani ya shilingi bilioni tano ambao ulitarajiwa kukamilika tangu mwaka 2017.

Amesema mkandarasi huyo aliweka masharti ya kupewa fedha nyingi ambapo tayari ameshapewa sehemu ya fedha hizo lakini bado utendaji kazi wake umekuwa wa kusuasua huku wananchi wakiendelea kupata adha ya kukosa maji.

Naye Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi na Mazingira Vijijini (RUWASA) Mkoa wa Songwe Mhandisi Charles Pambe amesema mradi wa Maji wa Iyula una gharimu shilingi bilioni tano na tayari Mkandarasi huyo ameshapewa bilioni 2.2.

Pambe amesema kutokana na kusuasua kwa mkandarasi huyo RUWASA wana angalia uwezekano wa kuujenga mradi huo wenyewe kwa kutumia Force Account.

Hata hivyo Mkandarasi wa Mradi wa maji wa Iyula kutoka STC Construction ya Dar es Salaam Alan Makame amesema kusuasua kwa mradi huo ni kutokana na kucheleweshewa malipo pamoja na RUWASA kutotembelea mradi huo.

Hata hivyo, ndani ya siku tatu atakuwa ameanza kazi ya kuweka baadhi ya mabomba katika mradi huo na kuwa baada ya wiki mbili atakuwa amekamilisha mradi huo