RC Mwanza azindua kituo cha kufundishia lugha

25Nov 2021
Neema Emmanuel
Mwanza
Nipashe
RC Mwanza azindua kituo cha kufundishia lugha

MKUU wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel, amezindu Kituo cha Kimataifa cha Mahusiano Lugha na Maendeleo (ICILD), huku wananchi wakitakiwa kutumia muda kujifunza ili kupata fursa mbalimbali.

Anasema kuna ulazima wa vijana kujifunza lugha za kigeni kwa sababu mkoa umeweka msisitizo mkubwa kwenye utalii wa ndani na nje ambapo ni lazima wajiandae kupokea wageni kwani unapotaka kufungua milango ya watalii wa nje lazima uwe na maandalizi, ulazima kujifunza lugha, kujua tamaduni zao wanaokuja ikiwemo kujua vyakula wanavyopenda, mazingira wanayoyapenda pamoja na michezo.

Amesema katika kipindi hiki cha mwisho wa mwaka mapinduzi makubwa ya kufungua Mkoa kiuchumi zaidi katika masuala ya kiutalii yatafanyika na utapokea watalii wengi hivyo kuna umuhimu wa kujifunza lugha na tamaduni mbalimbali Ili kuweza kuwasiliana vizuri na wageni hao wakati mwingine kupata fursa kutoka kwao.

"Lugha inatoa nafasi kubwa ya kuvuka mipaka ambayo bila lugha haiwezi kuvuka kituo cha ICILD kimefanya kazi kubwa ya kutoa mafunzo ya lugha za kigeni zaidi ya 15 pamoja na lugha yetu nimeona wanafunzi waliokuja hapa hawajui kuongea lugha sasa wameweza kuongea vizuri sana, " amesema.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kituo hicho Charles Mwombeki, ameeleza kituo hicho ni chemichemi ya maarifa na ufunguo wa dunia iliyofungwa hivyo kilianzishwa kwa lengo la kuondoa kizuizi cha mawasiliano baina ya watanzania na wageni hivyo walianza kufundisha lugha ya kiswahili kwa wageni na kiingeleza kwa wenyeji .

Ameeleza kutokana na mahitaji kuongezeka kituo kililazimika kuongeza lugha nyingine zaidi ya 15 kama kifaransa, Kichina , Kitalianao, Kijerumani, Kiarabu, Kireno, Kijapani, Kikorea, Kirusi, Kidachi na lugha za asili kama Kisukuma na Kihaya .

Ameongeza sera za serikali ambazo ziliweka msukumo wa kuvutia uwekezaji kutoka jumuiya ya kimataifa na kuja kwa sera ya uchumi wa viwanda zimeongeza uhitaji wa lugha kama dhana muhimu kwa mawasiliano Kati ya wageni na watanzania kwa kuondoa kizuizi cha mawasiliano na mahusiano.

Naye Mkufunzi wa Lugha za Kigeni Dk. Christine Salalah, ameeleza kuwa mtalii ni mtu yeyote bila kujali mahali alipo, wengi wanapenda kupumzisha akili, kupata burudani na kuonyeshwa upendo hivyo ni vyema kufahamu mahitaji yao hivyo, kujifunza lugha ni jambo la muhimu na kivutio kikubwa cha wageni.

Habari Kubwa