RC Sengati asisitiza viongozi wa dini kuhubiri amani

03Oct 2021
Marco Maduhu
Shinyanga
Nipashe Jumapili
RC Sengati asisitiza viongozi wa dini kuhubiri amani

​​​​​​​VIONGOZI wa dini kutoka katika madhehebu mbalimbali hapa nchini, wamesisitizwa kuendelea kuhubiri udumishaji wa amani ya nchi.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, akizungumza kwenye uwekaji Wakfu Jengo jipya ya Kanisa la EAGT Ushirika Manispaa ya Shinyanga.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Philemon Sengati, amebainisha hayo leo  kwa niaba ya Makamu wa Rais Dk. Philipo Mpango, wakati wa Ibada Maalum ya kuweka wakfu jengo jipya la Kanisa la EAGT, lililopo ushirika Manispaa ya Shinyanga.       

Amesema serikali inatambua kazi kubwa ambayo inafanywa na madhehebu ya kidini hapa nchini, kwa kuhakikisha amani na utulivu vinatawala, tunu ambayo iliasisiwa na Hayati Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.

"Nipo Kanisani hapa kumwakilisha Makamu wa Rais Dk. Philipo Mpango, ambaye yupo kwenye majukumu mengine ya kitaifa, anaomba viongozi wa madhehebu ya kidini muendele kuhubiri amani ya nchi," amesema Dk. Sengati.

Muonekano wa Jengo jipya Kanisa la EAGT ushirika Manispaa ya Shinyanga ambalo limewekwa Wakfu leo.

"Serikali tunatambua kazi ya viongozi wa dini, ambapo mnaimarisha misingi ya upendo, utu, uzalendo, na mshikamano kwa wananchi, na kuifanya Tanzania kuendelea kuwa na amani na utulivu," ameongeza.

Aidha, amesema serikali pia inatambua mchango wa madhehebu ya kidini, katika mchango wa kuboresha huduma za afya, elimu, na kuahidi kuendelea kuwa unga mkono, huku akilikaribisha kanisa hilo kufanya uwekezaji wa viwanda ambapo watapewa eneo bure.

Katika hatua nyingine Dk. Sengati, amewataka Watanzania kujitokeza kwa wingi kupata chanjo ya UVIKO-19, na kupuuza maneno ya upotoshaji juu chanjo hiyo, ili siku wakipata maambukizi ya virusi vya Corona wasipate madhara makubwa.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Kanisa la EAGT Dk. Brown Mwakipesile, ameishukuru serikali kuendelea kutoa uhuru wa kuabudu bila ya kuwapo buguza yoyote ile, na kuahidi kuendelea kuhubiri amani ya nchi.

Askofu Mkuu wa Kanisa la Evenjelistics Asseblies Of God Tanzania EAGT Dk. Brown Mwakipesile, akizungumza wakati wa uwekaji Wakfu jengo jipya la Kanisa la EAGT Ushirika Manispaa ya Shinyanga.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya ujenzi wa Kanisa hilo jipya John Ntalimbo, akisoma taarifa ya ujenzi, amesema ulianza mwaka 2003 na kuisha mwaka huu, kwa gharama ya shilingi milioni 825.

Waumini wa Kanisa la EAGT Ushirika Manispaa ya Shinyanga, wakiwa kwenye Ibada Maalum ya kuwekwa Wakfu jengo lao Jipya la Kanisa.

Habari Kubwa