RIPOTI MAALUM; Makali ya kunguni majumbani, shuleni -2

02Jul 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
RIPOTI MAALUM; Makali ya kunguni majumbani, shuleni -2

Katika toleo letu la jana tuliona jinsi wadudu aina ya kunguni wanavyosababisha usumbufu kwa taasisi hususan shule za bweni na majumbani. Katika sehemu hii ya pili na ya mwisho, waathirika wanaendelea kusimulia, taarifa mbalimbali za utafiti na kauli ya serikali.

kunguni.

Agnes Moses (siyo jina lake halisi) anasimulia kuwa mmoja ya watoto wa ndugu yake walipata matatizo akawekwa moja ya mahabusu (anaitaja) jijini Dar es Salaam baada ya kutoka alifikia nyumbani kwake, Mikocheni.

Alisema baada ya kijana huyo kukaa siku chache na baadaye kuondoka, wakati wakifanya usafi kwenye chumba alichokuwa akilala, walikuta idadi kubwa ya kunguni.

“Tumeshatumia dawa za kila aina, kuna dawa ambayo tuliambiwa ndiyo kiboko kutoka Afrika Kusini, tulinunua tukatumia kuwaangamiza, lakini baada ya muda hali imerejea. Tunachofanya sasa ni kupiga dawa na kutoa magodoro na viti nje kila siku, lakini bado wapo,” alisema.

Aliongeza: “Kunguni akiingia ndani ni kero huwezi kummaliza, gharama tuliyotumia ni zaidi ya milioni, lakini hatujafanikiwa, ukikaa kwenye kochi wapo, vyumbani wapo.”

Alisema kutokana na changamoto hiyo anaogopa kutembelewa na ndugu, jamaa na marafiki au wao kwenda kwao kwa kuhofia kuwasambaza.

JESHI LA POLISI LAFUNGUKA

Akitolea ufafanuzi kuhusu malalamiko ya baadhi ya mahabusu kudaiwa kuwa na kunguni, Msemaji wa Jeshi la Polisi nchini, David Misime, aliliambia gazeti hili kuwa ofisi zote za serikali zina utaratibu wa kupulizia dawa za kuua wadudu mara kwa mara.

 “Utaratibu uliopo kila siku asubuhi mahabusu husafishwa tena siyo kwa maji, wanasafisha kwa kutumia maji yenye dawa ili kuua wadudu pamoja na hao unaowataja. Pia upo utaratibu wa kupulizia dawa ya kuua wadudu ‘fumigation’ baada ya muda fulani ili kuondokana na maambukizi ya magonjwa kwa sababu sehemu hizo huingiwa na watu wa aina tofauti tofauti,” alisema.

SERIKALI YATOA HOFU

Naibu Waziri wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, aliliambia Nipashe kuwa kunguni haambukizi magonjwa kwa binadamu zaidi huleta maudhi.

“Kimsingi, kunguni ni wadudu ambao kitaalamu siyo vijidudu vinavyosababisha magonjwa, lakini kama wataalamu wa afya tunaona ni mdudu anayeleta maudhi, anapokuuma unawashwa unajikuna.

Aliongeza: “Mtu anapowashwa sana anajikuna na akijikuna sana, anaweza kupata maambukizi mengine ya ngozi ambayo sasa inaweza kumletea mtu madhara zaidi. Lakini kunguni kama mdudu siyo vijidudu vinavyosababisha magonjwa.”

Dk. Ndugulile alibainisha mdudu huyo anahusishwa masuala ya usafi wa mazingira ya mtu binafsi na kubainisha kuwa kama yatakuwa machafu uwezekano wa mdudu huyo kuwapo ni ukubwa.

“Unapokuwa na mazingira safi basi kunguni siyo rafiki wa usafi, unapoona sehemu ina kunguni maana yake hali ya usafi hairidhishi. Nitumie fursa hii kutoa rai kwa jamii, shule na maeneo mengine kuhakikisha mazingira yetu wakati wote yanakuwa masafi,” alisema.

Dk. Ndugulile alibainisha kuwa wadudu hao hupenda kujificha kwenye kuta zenye nyufa, chaga za vitanda, magodoro na maeneo mengine yasiyo na mwanga.

“Kama ukiona una tatizo la kunguni jitahidi vitu vyako uvitoe nje uvianike kwenye jua, hakikisha unatumia maji ya moto kufua matandiko, kuanika magodoro juani na kupulizia dawa, lakini kikubwa zaidi ni kuzingatia usafi na nyumba zenye nyufa zizibwe,” alisema.

Kuhusu utafiti ambao umefanyika hadi sasa ambao unabainisha kuua kunguni kirahisi kwa sumu, Dk. Ndugulile alisema siyo kweli na kueleza kuwa zipo kemikali ambazo zinaweza kutumika kuwaangamiza.

“Siyo kila dawa unayoitumia inaua mdudu, kwa sababu viumbe hivi vimeumbwa kwa utofauti na hali ya upokeaji wake wa dawa, ni vizuri mtu anayesumbuliwa na kunguni apate ushauri kwa washauri wataalamu ili upate njia sahihi ya kuwaua,” alisema.

UTAFITI DUNIANI

Utafiti uliofanywa kuhusu mdudu huyu umekuja na matokeo kuwa, wanaweza kustahimili kupuliziwa dawa nyingi ya sumu kwa kuimarisha uwezo wake wa kujikinga dhidi ya sumu moja baada ya nyingine.

Mdudu huyo ameonyesha ana uwezo mkubwa wa kibaiolojia ya kujikinga dhidi ya sumu kali na kadri vizazi vya kunguni vinavyopuliziwa dawa yenye sumu ndivyo  wanavyoimarisha uwezo wao wa kuzuia maafa miongoni mwa watoto wao.

Taarifa iliyochapishwa katika jarida la utabibu la The Journal of Medical of Entomology, watafiti wanasema  vipimo 1000 vya sumu kali aina ya (neo-nicotinoid) vinahitajika kuua kunguni mmoja huko Marekani katika majimbo ya Cincinnati na Michigan ikilinganishwa na maeneo mengine duniani.

“Kuna hatari kubwa ya mdudu huyu kuenea kote duniani kutokana na utandawazi na soko huria ambao umefanya ulimwengu kuwa kitongoji kikubwa tu,” watafiti hao wanabainisha.

Wanasayansi hao wanashauri kutafutwa mbinu mpya tofauti ya kukabiliana na wadudu hao badala ya kutumia sumu, kutafuta wadudu wengine wanaoweza kuwala ili kuzuia kunguni kuenea duniani kote.

RANGI WAZIPENDAZO

Watafiti nchini Marekani baada ya kufanya uchunguzi wa kina, wamebaini kunguni hupenda baadhi ya rangi kushinda nyingine.

Uchunguzi uliofanywa na watafiti hao umebaini wadudu hao hupenda rangi nyeusi na nyekundu na huchukia njano na kijani kibichi.

Matokeo ya utafiti huo ambayo yalichapishwa katika jarida la kimatibabu la Journal of Medical Entomology, watafiti hao wanasema bado ni mapema kubaini iwapo shiti za rangi ya njano zinaweza kutumiwa kuwafukuza wadudu hao kitandani au la.

Daktari Corraine McNeill na wenzake walitaka kubaini iwapo rangi zinaweza kuathiri maeneo wanayovamia na wadudu hao.

Katika uchunguzi wao walitumia vibanda vidogo vya rangi mbalimbali kwenye maabara na kuchunguza kunguni ndipo alipobaini wanapenda rangi hizo mbili.

"Hata hivyo, baada ya uchunguzi, sababu kuu tuliyobaini iliwafanya kupenda rangi nyekundu ni kwa sababu kunguni wenyewe huonekana wakiwa wa rangi nyekundu, hivyo hudhani rangi hiyo ni kunguni wenzao,” walibainisha watafiti.

Utafiti uliofanywa awali umebainisha kwamba rangi hizi pia hazipendwi na wadudu wengine wafyonza damu kama mbu.

MWONEKANO WAKE

Kwa wasiomjua, kunguni ni mdudu mdogo mwenye miguu sita, kulia mitatu na kushoto mitatu na hawezi kuruka kama  mende, hutambaa na huishi kwa kutegemea damu kama chakula chake ndiyo maana amekuwa msumbufu kwa watu.

Wadudu hawa wapo wa aina nyingi, wanaouma popo tu na wapo wanaowauma binadamu.

Kihistoria wadudu hawa walikuwapo enzi na enzi, lakini mwaka 1940 walimalizwa katika nchi zilizoendelea kama  Marekani na za Ulaya, lakini ilipofika mwaka  1995 walirudi upya.

Sababu za kurudi kwao zinatajwa ni dawa za kuwaua ziliwatengenezea usugu, hivyo kukosa nguvu ya kuwaangamiza, kupigwa marufuku dawa hizo baada ya kuthibitika zina madhara kwa binadamu na huweza kusafiri nchi moja hadi nyingine.

Mdudu huyo hutaga yai kila siku kuanzia yai moja hadi matano na baada ya yai anakuwa  mdogo mwenye milimita 1.5, kisha hukua hatua kwa hatua hadi anafikia kuwa kunguni kamili.

TABIA ZA KUNGUNI

Mara nyingi mdudu huyu amekuwa na tabia ya kujificha hasa nyakati za mchana kwenye maeneo ambayo siyo rahisi kugundua kama wapo na hushamiri na kuonyesha makeke yao nyakati za usiku watu wakiwa wamelala.