RIPOTI MAALUM: Dhiki katikati ya kito adimu

14Nov 2017
Gaudensia Mngumi
Nipashe
RIPOTI MAALUM: Dhiki katikati ya kito adimu

NI asubuhi ya saa 12:30 nikiwa nimejihimu kufika kwenye kituo kikuu cha mabasi cha Moshi mjini ili kupanda basi la kunifikisha Mirerani, wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara, licha ya kwamba safari ingeanza saa 2:00.

Ndani ya basi nafundishwa matamshi kuwa mji ninakokwenda ni Mirerani, na siyo Mererani kama ambavyo Watanzania wengi wamezoea kuuita.

Inanichukua mwendo wa kama saa mbili na nusu za kuambaa na barabara mpya ya lami isiyochosha wala kumkera msafiri kufika kwenye mji mdogo huo ulio maarufu kwa uchimbaji wa kito cha tanzanite, madini ambayo yanapatikana nchini pekee.

Kinyume na picha niliyokuwa nimepiga akilini, naanza kushangazwa na tatizo la maji nililokutana nalo punde baada ya kushuka kwenye basi. Mji wa Mirerani ni kama jangwa!

Naelezwa kuwa maji safi na salaam ni tatizo kubwa kiasi kwamba hutolewa katika mji mdogo wa Bomang’ombe uliopo wilaya ya Hai mkoani Kilimanjaro.

Nikiwa kwenye nyumba ya kulala wageni, nagundua boza la maji lililoletwa kutoka mji huo linanunuliwa kwa bei ya jumla ya Sh. 30,000, lakini pia ipo biashara ya ndoo au dumu kwa bei ya Sh. 1,000.

Lengo langu likiwa kufika kwenye mashimo inakotoka tanzanite, sipotezi wakati naelekea migodioni kwa usafiri wa bodaboda.

Ndipo ninapokutana na adha nyingine, kwamba njia nzima ni vumbi na vipande vya mawe na kila ambaye nilipishana naye barabarani ni mweusi mithili ya mtu aliyejipaka masizi.

Vito vya tanzanite ambavyo wachimbaji wake huzamia chini ya ardhi, usiku na mchana, vimesababisha wana-apolo hao, kama wanavyojiita, waathirike na vumbi laini kama saruji yenye kumeremeta, wanaloliita ulanga.

Hunasa kila mahali: kwenye ngozi, meno, machoni, mavazi, mimea na magurudumu ya bodaboda au gari.

wana-apolo wanasema hulazimika kutumia sabuni za unga na za maji wakati wa kuoga ili kuondoa ulanga mwilini.

“(Ulanga) Umekuwa sugu kwa sabuni za kawaida," anasema mwana-apolo aliyejitambulisha kwa jina moja la Hamduni. "Bila sabuni ya unga huwezi kutakata. Vumbi hili linapausha ngozi hata ukipaka mafuta na vipodozi havikubali.”
Wana-apolo wananitembeza sehemu inayoitwa OPEC.

Kimsingi, OPEC ni kifupisho cha Umoja wa Nchi Zinazozalisha Petroli kwa Wingi duniani lakini hapa Mirerani lina maana tofauti kwa wana-apolo - eneo ambalo mwamba wake unatoa madini ya tanzanite kwa wingi kama ambavyo mafuta huzalishwa kwa wingi na nchi wanachama wa OPEC.

Wana-apolo pia wananifikisha ndani ya kitalu cha uchimbaji walichokipa jina la Mochwari, chumba cha kuhifadhia maiti, ambako wanasema, wana-apolo wengi wamezikwa.

“Madini yalikuwa yanapatikana kwa wingi kabla ya (mwaka) 2000, (lakini) uchimbaji ulikuwa duni. Hakukuwa na utaalamu (kama wa saa) na kusababisha wengi kufa baada ya kufunikwa na miamba,” anasimulia Antony Kisungwe.

Licha ya Kisungwe kudai uchimbaji wa tanzanite wa wanaapolo ulikuwa duni miaka 17 iliyopita, naona hakuna hatua iliyopigwa katika zana wanazotumia 2017 sasa. Zana ni duni na licha ya utajiri wa vito, hali ya wachimbaji kimaisha pia ni duni.

Wengi hununua mboga kwa mama lishe kisha kwenda kujiandalia ugali kwenye makambi yao, na hao ni wale wenye maisha ya anasa kwa kiwango cha wachimbaji wadogo wa Mirerani.

Baadhi huishi kwa chai na vitafunio vichache kama chapati, maandazi, vitumbua na half cake kila siku.

“Kila kitu ni Sh. 100 lakini hatuna hela," anasema Ludo Mshelee. "Ni dhiki na njaa kali mama."

“Hapa tunaishi kwenye camp (kambi), kama huna kambi unalala mtaani. Nje ya hapo hakuna sehemu ya kuishi, kula, wala kujisaidia.”

Makazi ya wana-apolo pia hayana vyoo bora wala maji safi ya kunywa. Maji yanayotumika ni meusi yaliyojaa vumbi.

Naelezwa kuwa wanaapolo wengi hawana mshahara wala mkataba wa ajira, na wengi hulipwa kwa kugawana kile ambacho mmiliki amewabakizia baada ya mgodi kutoa mawe.

UJASIRIAMALI
Licha ya kuwa mji unaopaswa kuwa wa biashara ya mabilioni ya shilingi kutokana na tanzanite kupatikana hapo pekee, Odilo maarufu kama Obama, anasema mzunguko wa fedha ni mdogo hivyo kuchochea umaskini miongoni mwa wakazi wake.

Anasema bidhaa zipo kwa wingi madukani lakini hakuna hela kwa vile kinachowapa nguvu ya manunuzi ni kupata na kuuza mawe.
“Kama hakuna mawe (madini), wote tunakuwa kama kuku wenye kideri. Wakati huu hatujapata madini tuko taabani.

Bidhaa zipo na maisha siyo magumu lakini hakuna pesa.”

Wana-apolo huuza madini ya viwango vya chini ambayo huyaita ‘magonga’ kwa Sh. 500 kwa kipande chenye ukubwa wa mbegu ya ubuyu lakini nayo hayapati wanunuzi.

Ndani ya migodi kuna ujasiriamali wa kuuza mifuko chakavu ya viroba ambayo hutumiwa mashimoni kujaza mchanga unaopandishwa juu kuchekechwa, ili kupata ‘mawe’.

Viroba hivyo vimechakaa lakini vinaendelea kuuzwa na hukusanywa kama wajasiriamali wanavyouza chupa na mabaki ya vyombo vya plastiki jijini Dar es Salaam.

“Mirerani kila kitu kinaweza kuuzwa na kuliwa... hata nyama ya punda inalika,” anasema Ndosa Mjanjaa.

ATHARI ZA ULANGA
Sura za wanaapolo niliokutana nao zilinitisha kwa vile walibadilika ngozi, macho, midomo, kucha, nywele na mavazi. Vilinistua na kutaka kufahamu iwapo ulanga una athari kiafya kwa wachimbaji.

Maelezo ya Dk. Allan Tarimo, Mratibu wa Huduma za Kifua Kikuu Maeneo ya Migodi kutoka Ofisi ya Mpango wa Taifa wa Kifua Kikuu (TB) na Ukoma (NTLP), yanathibitisha kuwa ni hatari.

Anafafanua kuwa vumbi hilo linalopatikana zaidi katika machimbo ya Mirerani, linahatarisha afya ya mapafu.

Anasema linapoingia kwa wingi mapafuni linauwa seli za mapafu na kusababisha viungo vya kusafisha hewa vishindwe kufanya kazi.

“Maradhi yanayotokana na ulanga kwa kitaalamu huitwa ‘silicosis’. Haya huumiza mapafu na hayana tiba. Ukipata ugonjwa huu mwisho ni kufa kwa sababu mapafu yanashindwa kufanya kazi ya kuchuja hewa na mchimbaji hufariki dunia,” anasema tabibu huyo.

Ufafanuzi zaidi wa maradhi ya silicosis, unaopatikana kwenye mtandao wa Idara ya Afya na Usalama Kazini ya Marekani (OSHA), unaeleza kuwa madhara yanayotokana na vumbi la madini ya miamba jamii ya ‘silica’ huleta matatizo sugu ya mapafu na kwenye njia za hewa.

Pia ni chanzo cha saratani ya mapafu, maradhi sugu ya ‘bronchitis’ ambayo husababisha kushindwa kuhema kunakoleta kikohozi kikavu, kubanja na wakati mwingine kukohoa damu. Vumbi hilo hilo la silica huchangia vidonda na udhaifu kwenye mapafu na kurahisisha wadudu wa TB kumshambulia mtu.

OSHA inataja dalili za silicosis kuwa ni kukosa pumzi, kuchoka mara kwa mara, kuishiwa hamu ya kula, kubanwa mbavu, kikohozi kikavu kinachoumiza koo na kifua na kushindwa kupumua.

Mtandao huo unaeleza zaidi kuwa kuchimba madini, kuvunja miamba ili kuchimba madini, kuchimba barabara, kutengeneza zege na kazi za ujenzi wa miundombinu, majengo na kazi za kubomoa majengo na kukusanya vifusi, ni chanzo cha TB.

Kibaya zaidi ni kuwa wana-apolo hawana vitendea kazi wanapozama kwenye mashimo. Hawana viziba midomo na pua, miwani wala mavazi maalumu. Wamejaa vumbi la ulanga kila mahali.
ITAENDELEA KESHO