RIPOTI MAALUM: Elimu bure mtihani mzito kwa Serikali

07Feb 2016
Nipashe Jumapili
RIPOTI MAALUM: Elimu bure mtihani mzito kwa Serikali
  • *Shule yenye wanafunzi 650 imejengwa kwa miti na nyasi

WAKATI Rais John Magufuli akitarajiwa Ijumaa kutimiza siku 100 tangu aingie Ikulu, bado kuna kazi kubwa ya kufanikisha utoaji wa elimu bure kwa kila Mtanzania kama alivyodhamiria kutokana na hali duni iliyotawala katika baadhi ya shule nchini.

Uchunguzi uliofanywa na Nipashe kwa kuhusisha ziara kwenye Shule ya Msingi Lupemba iliyopo katika Kijiji cha Bubinza, Kata ya Lubugu, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, umebaini kuwa hali ni mbaya katika baadhi ya shule na hivyo hatua za haraka zinahitajika ili kuupa mafanikio mpango huo wa serikali wa kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne. Nipashe imebaini kuwa shule hiyo ya Lupemba, iliyopo katika Wilaya ya Magu mkoani Mwanza, ilianzishwa mwaka 2006 na sasa ina wanafunzi 651. Hata hivyo, ni wanafunzi wa darasa la kwanza na la saba tu ndiyo husomea kwenye vyumba rasmi viwili vya madarasa vilivyopo huku waliobaki wakilazimika kusomea kwenye mabanda yaliyojengwa kwa miti na nyasi. Kadhalika, shule hiyo ina walimu tisa huku madawati yakiwa msamiati mgumu kwa wanafunzi walio wengi kwani yapo 45 tu, wengine wakiishia kukalia mawe na vipande vya matofali. Aidha, Nipashe imebaini kuwa licha ya wananchi kufurahia agizo la serikali la kuhakikisha kuwa elimu inatolewa bure kama ilivyoahidiwa na Rais Magufuli kwa kupiga marufuku aina zote za michango shuleni, kwa shule ya Lupemba mambo ni magumu. Maelekezo hayo ya elimu pasipo malipo yaliyotolewa na serikali kupitia waraka namba 5 wa 2015 na ufafanuzi wa utekelezaji wake kwenye waraka namba 6 wa 2015, umeiacha Lupemba ikizidi kudidimia kwa kushindwa kutekeleza mipango kadhaa iliyojiwekea. “Mpango huu wa elimu bure umetusaidia sana kutupunguzia mzigo wa gharama uliokuwa ukitokana na utitiri wa michango kwa ajili ya maendeleo ya shule hii. Hata hivyo, hivi sasa mambo mengi yamesimama kwa sababu hakuna tena fedha zitokanazo na michango,” mwananchi mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Martin aliiambia Nipashe wilayani humo mwishoni mwa wiki. "Ni vizuri serikali ikaipa uangalizi maalumu shule hii (Lupemba) kwa kuipa fedha za kutosha ili kuwaokoa watoto wetu ambao hivi sasa wanasoma kwa shida kwenye mabanda ya nyasi na miti." Mwanzoni mwa Januari, Serikali ilianza rasmi kutekeleza ahadi ya Rais Magufuli ya kutoa elimu bure kwa kila mtoto huku ikisambaza fedha katika shule za halmashauri zote nchini. Magufuli alitoa ahadi ya kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana na mwishowe akaibuka mshindi kwa kupata asilimia 58.46 ya kura zote halali zilizopigwa. MWALIMU MKUU ANENA Mwandishi wa Nipashe alipofika kwenye shule hiyo katikati ya wiki, alibahatika kuwaona wanafunzi kadhaa wakiendelea kujisomea kwenye madarasa yao ya miti na nyasi huku shughuli nyingine za kitaaluma zikiendelea kama kawaida. Akizungumza na Nipashe, Mwalimu Mkuu wa shule hiyo, Daniel Matemi, alisema hali ya utoaji wa elimu shuleni kwao ni ngumu lakini wanaendelea kupambana kila uchao ili kutimiza malengo waliyojiwekea. Matemi alisema wanakabiliwa na upungufu wa walimu watano, upungufu wa vyumba 12 vya madarasa ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi walio nao, madawati 175, ofisi moja na pia wana tatizo la kutokuwa na choo kwa ajili ya walimu. Hawana pia nyumba za walimu, alisema. Matemi aliiambia Nipashe kuwa licha ya kukabiliwa na rundo la changamoto, bado shule yao ni miongoni mwa zile zinazofanya vizuri wilayani mwao hata hivyo, hasa kwa kuangalia matokeo ya mitihani iliyopita ya darasa la nne na la saba. Alisema matokeo ya darasa la saba kwa mwaka uliopita walishika nafasi ya kwanza katika kata yenye shule sita, kwa wilaya walikamata nafasi ya 37 kati ya shule 110, mkoa nafasi ya 381 kati ya shule 900 na kitaifa walishika nafasi ya 3,584 kati ya shule 16,096. Matemi alisema kwa matokeo yaliyopita ya darasa la nne, shule hiyo ilishika nafasi ya kwanza ngazi ya kata, wilaya ikiwa ya 10 kati ya shule 111, mkoa ya 109 kati ya 913 na kitaifa ya 2,235 kati ya shule 16,657. WASEMAVYO WAZAZI Kasoli Peji, mmoja wa wazazi wa watoto wanaosoma kwenye Shule ya Lupemba, alisema kila uchao huwa anamuomba Mungu ili wanawe warudi nyumbani salama kwani mazingira ya shule hiyo ni hatarishi, hasa madarasa yao ya miti na nyasi ambayo huwa katika hatari kubwa ya kuzolewa na upepo au mvua kubwa inaponyesha. “Huku kwetu wengi ni masikini wa kipato, hali ni duni sana. Ni vizuri serikali ikatekeleza wajibu wake wa kutujengea walau vyumba vya madarasa ili wanetu wawe na uhakika wa usalama wao,” alisema Peji. Gaudensia Amos alisema watoto wao wanasoma kwa hofu hasa katika kipindi cha mvua ambapo walimu hulazimika kuwaruhusu warudi nyumbani katika siku zote za mvua na wakati mwingine, mvua inaponyesha ghafla, watoto wote hurundikwa katika vyumba hivyo viwili vya uhakika vya madarasa ili kuwahakikishia usalama. “Hivi sasa matumaini yetu ni kwa serikali ya awamu ya tano. Rais Magufuli aliahidi kuboresha elimu na bila shaka serikali yake itaiangalia shule hii kwa jicho la huruma ili watoto wetu wasome kwenye madarasa yenye kutuhakikishia usalama wao,” mzazi mwingine aliyekataa kuandikwa jina lake alisema. KABLA YA TAMKO LA ELIMU BURE Mtendaji wa Kijiji cha Bubinza ambako ndiko ilipo shule ya Lupemba, Masalu Sosela, alisema kabla ya uamuzi wa serikali wa kuzuia michango shuleni, wananchi walikuwa wakichangishwa fedha kwa ajili ya kusaidia uboreshaji wa shule hiyo. Kwa mfano, alisema, mwaka 2012/13 kila kaya ilichangia Sh. 2,000 kati ya kaya 819, kisha wakapewa mifuko 100 ya saruji kutoka mfuko wa jimbo na hivyo kufanikiwa kujenga vyumba vya madarasa mawili vinavyotumiwa sasa na wanafunzi wa darasa la kwanza na la saba. Alisema baadaye kijiji kiligawanywa na kubaki na kaya 312 na kaya zisizo na uwezo ziliondolewa katika uchangiaji na hivyo wakabaki na kaya 295. “Mwaka 2014/15, kaya hizo 295 zilichanga Sh.10,000 kila moja kwa ajili ya ujenzi wa vyumba viwili na ofisi moja ambazo moja ipo kwenye hatua ya linta na nyingine ipo kwenye usawa wa madirisha," alisema Sosela. "Hivi sasa wanaendelea kuchangisha mchango wa Sh. 3,500 ili kukamilisha ujenzi huo.” Mjumbe wa kamati ya shule, Nestory Mwemweta, alisema wanawashukuru wananchi kwa kutambua umuhimu wa kuchangia lakini wamekuwa wakiomba kila mara serikali iwekeze nguvu shuleni hapo, hasa kwa kuwasaidia katika ujenzi wa vyumba vya madarasa. Diwani wa kata hiyo, Lukas Zabroni, alisema shule ya Lupemba ina hali ngumu na inahitaji nguvu za serikali katika kuikwamua, kama ilivyo katika shule nyingine za kata yao ambazo zinakabiliwa na changamoto nyingi pia zikiwamo za upungufu wa walimu, majengo, matundu ya vyoo na nyumba za walimu. MGAWO WA RUZUKU Kaimu Afisa Elimu ya Msingi wa Wilaya ya Magu, Veronica Justine, alisema serikali inatoa ruzuku ya uendeshaji wa shule kwa kila mwezi, na kwamba fedha za ruzuku hiyo huelekezwa kwa matumizi ya ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia ambazo ni asilimia 30, ukarabati wa miundombinu asilimia 30, uendeshaji wa mitihani (20), michezo (10) na utawala asilimia 10. Alisema mwezi uliopita, Shule ya Lupemba ilipokea mgawo wa Sh. 363,000, fedha hiyo ikiwa ni kwa ajili ya uendeshaji wa shule na siyo kutumiwa katika suala la maendeleo. Alisema wazazi bado wanatakiwa kujitolea nguvu kazi na mali ili kuleta ustawi na maendeleo ya shule zilizopo ndani ya jamii yao. MKUU WA WILAYA Mkuu wa wilaya ya Magu, Karen Yunus, alisema elimu zaidi inatakiwa itolewe kwa wazazi kujua umuhimu wa elimu, hivyo akaitaka serikali ya kijiji kukaa na wanajamii ili kuwaelimisha. Pia katika ziara ya ukaguzi kwenye shule hiyo, akiwa na wakaguzi wa shule Januari 23, Yunus aliagiza vyumba vya madarasa vikamilike ndani ya siku 30. Alisema kuna haja ya kuwapo uhusiano mzuri kati ya taasisi za elimu na sekta mbalimbali za uzalishaji na wadau wengine ili kuisaidia shule ya Lupemba na nyinginezo wilayani humo zijikwamue kutoka katika changamoto nyingi zilizopo. WAKAGUZI WA SHULE Mkurugenzi Msaidizi wa Udhibiti Ubora wa Shule Wilaya ya Magu, Joseph Kaswa, alisema kulingana na hali ilivyo, shule hiyo haina vigezo vya ubora na hivyo wanasubiri kuona utekelezaji wa agizo la mkuu wa wilaya kuhusiana na uboreshaji wa miundombinu yake na kwamba, lisipotekelezwa, watachukua hatua ya kuifunga shule hiyo. “Tunaamini mpango wa elimu bure ulioletwa na serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli hautaongeza changamoto zaidi bali kuzitatua na kuboresha kiwango cha elimu yetu,” alisema Kaswa.

Habari Kubwa