RIPOTI MAALUM; Mabadiliko tabianchi yalivyoathiri Ziwa Tanganyika

24Jan 2022
Salome Kitomari
KIGOMA
Nipashe
RIPOTI MAALUM; Mabadiliko tabianchi yalivyoathiri Ziwa Tanganyika
  • *Kina chaongezeka, wanawake wajasiriamali wakwama biashara ya samaki, washindwa kupeleka watoto shule…

“MAISHA yetu yamebadilika sana kiuchumi, kwa sasa kupata Sh. 2,000 kwa siku ni ngumu sana, hatuna shughuli za kufanya kama zamani, kuongezeka kwa kina cha maji ya Ziwa Tanganyika kumeacha maumivu kwenye maisha yetu,-

Mwonekano wa Chuo cha Uvuvi Kigoma (FETA), Kibilizi, Kigoma Ujiji kilichozingirwa na maji, wanaonekana kwenye ngalawa ni wavuvi wakijiandaa kwenda kuvua. PICHA: MPIGAPICHA WETU

-hadi sasa baadhi yetu watoto wameshindwa kwenda shuleni kwa sababu tumeshindwa kuwanunulia sare na mahitaji mengine,” ndivyo wanavyoeleza baadhi ya wanawake wajasiriamali eneo la Mwalo wa Kibirizi, mkaoni Kigoma.

Wanawake hao ambao wamelazimika kubadili biashara na kuuza maandazi na kufuma mashuka, wanasema ni kawaida kula mlo mmoja kwa siku wa saa 10 jioni, kutokana na hali ngumu huku mtaji ukiisha kwa kuwa ndiyo unaotumika kutunza familia siku wanayokosa fedha.

Miongoni mwao wapo waliofanya biashara hiyo kwa zaidi ya miaka 29, lakini mabadilikio ya tabianchi yamewalazimu kujifunza shughuli mbadala za kuwaingizia kipato huku wengine wakiwa tegemezi wa ndugu zao.

Mialo ya Kibirizi na Nyobonzi ni maeneo rasmi yaliyo na miundombinu muhimu ya kuwawezesha wakulima kuchakata, kubanika samaki, majiko maalum ya kukausha dagaa na kupika samaki, kuna sehemu ya kupokelea, kukaushia na nyavu za juu za kuanika ambao unaruhusu kukauka bila kuingia mchanga pia inaruhusu upepo kupita chini na juu.

Mkoa wa Kigoma uchumi wake unategemea uvuvi na kilimo, na kwamba mabadiliko ya tabianchi yamesababishia kiwango cha dagaa na samaki wa kutosheleza wananchi na biashara kuwa ndogo, kiasi cha kushindwa kupata mapato.

Mlasi Juma kwa jina maarufu Mrisho anayefanyabiashara ya samaki wabichi kwa muda mrefu eneo la Forodha ya Ujiji, anasema wameathirika kisaikolojia kwa muda mfupi kutokana na maji kufunika maeneo yao yote muhimu kwa biashara.

“Tumevamiwa na maji kutoka mahala pake kwenda kwingine, tulikuwa tunafanyabiashara kwenye jumba maalum, tulikuwa tunauza sana, lakini baada ya maji kutuvamia tuliachana na jengo lile na kuhamia upande wa pili, ambako sio eneo la biashara,” anasema.

Aidha, anasema kutokana na hali hiyo mwalo wa Kibirizi umeathirika kwa kiasi kikubwa kwa kuwa nyumba ziliingiliwa na maji na kulazimu baadhi ya watu kutawanyika.

“Sehemu ya kuuzia mboga ilibadilishwa na kwenda kwingine watu wako mitaa ya Mitimingi, Kabondo, Pilimahonda na wengine tumebaki Forodhani, ingawa ni kugumu kupata biashara, lakini tuna afadhali kubwa ukilinganisha na wengine,” anasema Mlasi.

“Maji yamekuwa mengi hadi yametengeneza bwawa, zamani unanunua samaki za 40,000 una uhakika wa kuuza na kupata faida ya Sh. 5,000 au zaidi kwa siku, lakini kwa sasa sipati fedha yoyote kwa kuwa eneo letu limemezwa na maji na wavuvi hawapati samaki, zamani ukiwa Kando ya Ziwa ukiona mtumbwi unampungia mkono anasimama anakuuzia samaki kwa sababu tulikuwa kando ya ziwa, lakini sasa tuko mbali huku sokoni hauwezi kupata,” anasema.

“Hali yangu kiuchumi imekuwa ngumu sana, sasa sina uhakika wa kipato, tupo mbali ambako mtumbwi hauwezi kufika, pia wavuvi wanapata samaki wachache sana, nasi tunakosa wa kuuza wanaenda kuuza kwingine,” anasema.

Anasema kabla ya maji kujaa mwaloni alinunua samaki wa Sh. 60,000 ambao akiuza wote anapata faida ya Sh. 10,000 ya kwenda kula na familia yake.

 

WAHANGAIKA KUPATA SH. 2,000

“Kwa sasa unaweza kuwa na samaki wa Sh. 10,000, lakini kupata Sh. 2,000 ni kazi, familia zinahangaika kiasi cha kula mlo mmoja ambao huliwa saa 10 jioni kwa siku na unamshukuru Mungu kwa kuwa fedha inayopatikana ni ndogo kutosheleza mahitaji ya familia,” anabainisha.

“Wewe ndiyo mama, familia inakuangalia wewe kwa kila kitu. Tunapigana sana kimaisha usiku na mchana tunamwomba Mungu atusaidie mwalo wetu wa Kibirizi urudi kama zamani kama tunavyoahidiwa kuwa bandari ipo na itarudi, tunamuomba Mungu irudi,” anasema mjasiriamali huyo.

Kwa mujibu wa Mlasi, wazee wa zamani walisema maji yalikuwa eneo hilo na jingine kiasi cha wengi kushangaa maji yamerudi, eneo kubwa lilikuwa na makazi ya watu wanapanda boti kwenda, lakini yote yamemezwa na maji kidogo kidogo na sasa watu hawaishi tena.

Aidha, anasema alianza biashara hiyo mwaka 2000 na akilinganisha biashara ya wakati huo na sasa hali ya maisha ni ngumu. “Nilikuwa nikinunua mzigo wa Sh. 100,000 nikiingia nao sokoni nina uhakika wa kuumaliza na kupata riziki ya kula na watoto unapata Sh. 15,000 hadi 20,000.”

“Kwa sasa ukienda sokoni na migebuka ya Sh. 40,000 ni ngumu kuimaliza yote na hali ya maisha inazidi kuwa ngumu kwa kuwa wanategemea ziwa hilo kuendesha maisha yao, kuna kipindi cha nyuma muda huu (asubuhi) walienda kuvua wamesharudi na mzigo mwingi nasi tuna uhakika wa kuuza siku hiyo,” alifafanua.

Mfanyabiashara wa siku nyingi wa samaki, Dinna Jackson, biashara hiyo imemsaidia kuendesha familia kwa kuwa amesomesha watoto wake kupitia kazi hiyo.

“Kwa sasa mzunguko wa biashara ni mgumu sana kwa kipato cha wavuvi anaweza kuvua na kupata samaki mmoja au wawili, yaani imekuwa ngumu mno, maji ni mengi sana,” anasema.

Anasema mazingira ya samaki yalikuwa mazuri kwa kuwa aliweza kuvuka kwa miguu kwenda kuwatafuta, lakini kwa sasa ni ngumu kupata hata wachache, huku eneo la mwalo walilokuwa wanatumia likijaa maji na hawana eneo rasmi la biashara.

“Unapopata Sh. 2,000 unanunua chakula cha familia, unavumilia hivyo hivyo huwezi kujiua, ukipata sawa ukikosa mnalala njaa sawa, kwa kuwa kipato kimekuwa kigumu, kazi nyingine hatuna wenzetu wamezoea kufuma mashuka, lakini sisi kazi yetu ni samaki maisha yangu yote yanategemea Ziwa Tanganyika na sasa kina cha maji kimeongezeka siwezi kupata samaki kama zamani,” anasema.

“Baadhi yetu watoto wetu hawajaenda shule kwa sababu fedha hakuna, kule shule hawataki maneno kinachotakiwa ni fedha, mtoto anatakiwa awe na madaftari, viatu, begi ulipie baadhi ya vitu. Usipokuwa na fedha mtoto atakaa nyumbani hadi vifaa vienee unakwenda shuleni kuwaeleza kuwa sijafanikisha kutokana na hali ngumu ya fedha na nikipata atakuja shule,” anasema.

Naye Zabibu Hamis anasema baada ya maji kujaa mabwawa ya samaki aina ya ngege yaliharibika na wakarudi ziwani huku wafanyabiashara wakihamishwa eneo hilo kwenda jingine.

Anasema wakiwa kwenye mwalo huo walicheza michezo ya kupeana fedha ili kukuza mtaji, walisaidiana kwa umoja wao, walianzisha vikundi ambavyo vyote vilitawanyika kidogo kidogo kutokana na eneo kujaa maji.

Anasema walikaa zaidi ya miezi sita bila shughuli ya kufanya na kwamba walisambaa sehemu mbalimbali kila mmoja akienda kutafuta maisha kwingine.

“Mitaji ilishuka, huingizi fedha unatoa tu mwishowe unakula hadi mtaji, wengine walienda kulima mihogo na nyinginezo, kuna watoto wameshindwa kwenda shule maana huwezi kumpeleka bila viatu na sare za shule,” anasema.

Anasema waliingia kwenye biashara ambayo hawakuitegemea ambayo haiwaiingizii kipato kama ya samaki, lakini hawana cha kufanya kwa kuwa wanahitaji kupata kipato ili kutosheleza mahitaji ya familia.

Ripoti Maalum hii imefadhiliwa na Chama cha Wachapishaji wa Habari Duniani (WAN-IFRA) kupitia Social Reporting Initiative (SIRI).

Habari Kubwa