Ripoti Maalum Madhila yanayobeba majonzi ulawiti wa wanafunzi shuleni

17Feb 2020
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Ripoti Maalum Madhila yanayobeba majonzi ulawiti wa wanafunzi shuleni
  • *Wabuni mfumo, maficho 'kuharibiana'
  • *Malalamiko ya bibi, butwaa kwa walimu

NI habari na simulizi iliyojaa ukakasi kuanzia kuisikia au kuifahamu kwa namna yoyote, haina kokote inakoweza kusimama zaidi ya neno mbaya, wanafunzi kulawitiana. Sasa hata jina na hadhi ya Mkuranga nayo inaangukia kwenye ubaya.

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu. picha mtandao

Mamlaka za kiuongozi wilayani humo, kuanzia Ofisi ya Mkuu wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wilayani na nyenzo zake za usalama, Ustawi wa Jamii na walimu wa watoto hao, kila mmoja kwa nafasi yake anakiri kulifahamu na ama hatua zinazochukuliwa au kinachostahili kufanyika kukomesha hilo.

“Wanafunzi wenzangu walikuwa wananivizia wakati natoka shuleni kurudi nyumbani, mmoja ananishika mkono wa kulia na mwingine wa kushoto, halafu wananivua nguo na kuniinamisha chini...

“Wanafanya hivyo kwa zamu, mmoja akimaliza, anaanza mwingine na baada ya hapo, huwa wananitishia nisiseme kwa mtu yeyote, kwamba nikifanya hivyo wataniua."

Ni kauli ya mwanafunzi wa darasa la tano (jina tunalo) katika shule iliyoko kilomita chache kutoka makao makuu ya Wilaya ya Mkuranga mkoani Pwani.

Mwanafunzi huyo alikuwa akitoa ufafanuzi kwa Nipashe iliyomfuata kupata uhalisia wa tetesi hizo, ikiwa ni sehemu ya uchunguzi iliyoendesha wilayani humo kuhusu tuhuma za ulawiti miongoni mwa wanafunzi wenyewe.

Huku akiwataja kwa majina, alifafanua baadhi ya waliomtenda hivyo wanasoma naye shule moja na wengine si wanafunzi wenzake.

Aliendelea: “Siyo peke yangu wanayenifanyia hivi, tuko wengi (anawataja kwa majina), wanaotufanyia hivi, wengi ni wa darasa la saba (anawataja kwa majina). Wakati mwingine huwa wanatudanganya kwamba watatununulia chipsi."

Ni mazingira yapi hayo yanafanyika?

Mwanafunzi huyo ana simulizi ya ziada kwa Nipashe akisema: “Walikuwa wanatufanyia vitendo hivyo kila siku tunapotoka shuleni au tunapokuja (shuleni) asubuhi na kuna siku walinifanyia hivyo nikawa naumia sana! Nilishindwa kujizuia siku hiyo kwa sababu maumivu yalikuwa makali, nililia mpaka nyumbani na bibi aliniponiuliza, nilimwambia wamenifanyia vibaya.

"Bibi alinipeleka chooni kuniangalia, ndiyo akaanza kuniuliza, tena nilipojisaidia kilitoka 'kinyama'... alinishika na kunisafisha halafu akasema anipeleke shuleni akawaulize walimu.

“Nilimwambia bibi kwamba walionifanyia ni wanafunzi wa la saba, akasema 'twende akawatafute shuleni' na tulipofika na walimu nao walianza kuniuliza na nikawataja walionifanyia hivyo.”

Mwanafunzi huyo aliendelea kusimulia kwamba hatua iliyofuata, alipelekwa hospitali alikopatiwa dawa, aliyofafanua matumizi yake kuwa: "Mpaka sasa bibi ananiwekea na sasa hivi sisikii maumivu tena. Tangu bibi alivyokuja kushitaki shuleni na nikawataja wale waliokuwa wananifanyia, sasa hivi wanawafanyia wengine, mimi wameniacha."

KULIKONI SHULENI?

Nyayo za udadisi wa Nipashe zilifika hadi katika shule za msingi zinazohusika na kashfa hiyo kupata ufafanuzi na katika shule ya kwanza ilibahatika kukutana na Victoria Msuya na Rahim Mbululu, ambao ni walimu wakuu wasaidizi wa shule ambayo mtoto huyo anasoma.

Kwa kauli ya pamoja, walianza kwa kukiri uwapo wa kashfa hiyo katika maeneo yao ya kazi na baada ya kuwadadisi, kila mmoja kwa maelezo yake, aliangukia kuwa na taarifa ya vitendo hivyo vya ulawiti kufanyika kati ya wanafunzi wenyewe katika vipindi vya mapumziko na muda wa kwenda nyumbani.

Mwalimu Victoria alisema wanafunzi wengi waliowabainika kufanyiwa ukatili huo, ni wa madarasa ya tatu, nne na tano, kashfa hiyo ikifanyika zaidi eneo ambalo wanafunzi hao wamelibatiza jina la ‘Chimbo’.

“Ukishamaliza eneo hili la shule, kuna sehemu ambayo walikuwa wanachimba mchanga, huko ndiko tuliwabaini wakiwa wanaenda kufanyia hivyo vitendo," alisema, huku akielekeza kwa kidole kwamba:

"Kama unavyoona shule yetu haina uzio… inapofika wakati wa mapumziko, watoto wengine huwa wanapata mwanya wa kwenda hata huko mtaani kutafuta vyakula vidogo vidogo.

“Wengine ndiyo huenda huko kwenye machimbo na huwezi kujua, na ndiyo huo muda huwa wanautumia kushawishiana."

Mwalimu huyo alisimulia njia zingine wanazotumia wanafunzi kutekeleza mabaya hayo, ni kwa wanaosoma kwa kubadilishana, baadhi yao hufanya hivyo kabla ya muda wa kuripoti shuleni.

Victoria alitoa mfano wa namna mojawapo njama hizo zinavyofanyika, kwamba kuna baadhi ya wanafunzi wanaoingia masomoni saa nne asubuhi, lakini wanaaga kutoka nyumbani mapema, kumbe safari yao inaanzia kwenye uasi huo na kisha inakamilishwa shuleni.

“Kwetu walimu, inakuwa si rahisi kujua kwa sababu unamwona mtoto amewahi darasani kama kawaida, kumbe kabla ya hapo kuna mahali alipitia," alieleza.

WALIMU WALIJUAJE?

Mkasa wa bibi kuwasilisha rasmi ukatili dhidi ya mjukuu wake, ndiyo Mwalimu Victoria aliutaja kusaidia kuwafumbua macho na masikio ya kuwapo utovu huo wa nidhamu, akiwa na ufafanuzi kwamba: "Jambo hilo lilitushtua sana na tukaamua kuwaita wanafunzi wote kuwahoji."

Alieleza hatua za haraka walizochukua kwamba ni: “Watoto walianza kutajana, tulibaini kwamba watoto wengi waliokuwa wanafanyiwa, ni wa darasa la tatu, nne na tano na waliwataja waliokuwa wanawafanyia na wengine tayari wazazi wao wameshawaondoa shuleni.”

Naye Mwalimu Mbululu alisema wameanzisha utaratibu wa kufanya operesheni ya kufuatilia katika maeneo yote (likiwamo 'Chimbo') wanakobaini wanafunzi hao kufanyia vitendo hivyo.

“Kwa sababu tumeshafahamu mtandao wao, hata tukiona kuna mwanafunzi haonekani darasani, huwa tunawabana wenzake watuambie alipo na wakati mwingine wanatupeleka huko machimboni na tukienda tunamkuta.

“Kinachotushangaza ni kwamba hata hao wanaowaona huko mtaani wanashindwa kutoa ushirikiano kwa walimu. Kwa hatua hii waliyofikia hawa watoto, tunahitaji kushirikiana na jamii kuwasaidia hata kama siyo mwanao. Tabia hii ikienea, itaharibu watoto wengi," alibainisha.

Safari ya Nipashe ndani ya uwanda wa Wilaya ya Mkuranga, ilitinga kwenye shule nyingine ya msingi yenye wasifu wa kipekee kuwa na jumla ya wanafunzi 2,284 ikiwa na vyumba vya madarasa 10 tu.

Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Adrian Tete, ambako ni umbali mrefu zaidi kutoka makao makuu ya wilaya, alianza kutambulisha ugumu wa mazingira ya utendaji wake katika kuwamudu wanafunzi akitamka:

"Kwa picha hiyo unayoiona hapa, hata kama kuna mtoto ametoroka, huwezi kujua mpaka umalize kufundisha halafu uwaite majina, na wakati huo tayari kama ameenda huko porini kufanya mambo yao hayo, hata ukienda kumtafuta unakuwa umechelewa.

“Tungekuwa na madarasa ya kutosha, wanafunzi wote wakawa wanasoma kwa wakati mmoja bila ‘shift’, halafu kukawa na uzio, ingesaidia, hata namna ya kuwadhibiti ingekuwa rahisi kwa sababu wakati wa mapumziko wasingekuwa wanatoka nje.”

Nipashe ilipomdadisi zaidi kutaka kujua nafasi yake katika kashfa inayowakabili walimu wenzake kuhusiana na nidhamu mbaya ya vitendo vigeni visivyokubalika katika jamii kuvamia shule za Mkuranga, naye alikiri kwamba hajanusurika.

Katika picha ile ile inayowakabili walimu wenzake, Mwalimu Tete alisema tatizo kwa wanafunzi wake wamekuwa 'wakiharibiana' wenyewe kwa wenyewe, wahusika wakuu wa madhila hayo wakiwa ni wa madarasa ya pili, tatu na nne.

“Ni kweli katika shule yetu tulibaini watoto wetu wakifanyiana vitendo vibaya... hasa katika nyakati za mapumziko au wanapotoka majumbani kwao kuja shuleni na wanapotoka shuleni kurudi majumbani," alisema.

*ITAENDELEA KESHO

Habari Kubwa