RIPOTI MAALUM: Masoko ya Dar ni ng’ombe akamuliwaye bila malisho

17Apr 2018
Salome Kitomari
DAR ES SALAAM
Nipashe
RIPOTI MAALUM: Masoko ya Dar ni ng’ombe akamuliwaye bila malisho

KATIKA toleo la jana tuliona kwa undani hali ilivyo katika soko la Mabibo Manispaa ya Ubungo, matakwa ya sheria, wataalamu, kauli za viongozi wa Manispaa na jiji wanavyoshindwa kuboresha miundombinu ya masoko.

Kadhalika tuligusia hali ya soko la Tandale ambalo nalo linakabiliwa na changamoto kama za Mabibo. Makala ya leo itaangalia masoko ya Manispaa za Ilala na Temeke. Endelea kusoma... Uchunguzi wa Nipashe uliofanyika katika soko la Kisutu ambalo lipo katikati ya mji na ndilo taswira ya Jiji kwa kuwa linahudumia wateja wa nchi mbalimbali duniani, umeonyesha kuwa muonekano na miundombinu yake haviendani kabisa na eneo la jirani linalolizunguka.

Soko hili lililoko katika Manispaa ya Ilala, limezungukwa na majengo ya ghorofa na liko kando ya barabara ya Bibi Titi Mohamed likitazamana na viwanja maarifu vya Mnazi Mmoja. Hapa ni katikati ya Jiji la Dar es salaam.

Muonekano wa paa lake ni wa mabati makuu kuu na maturubai ya kampuni mbalimbali yanayotangaza biashara zake ndiyo yanatumika kuwakinga wachuuzi na wateja dhidi ya jua pamoja na mvua. Miundombinu mingine sokoni hapo ni duni kiasi ambacho haiendani na mazingira yanayolizunguka soko hilo.

Mkuu wa kitengo kinachojishughulisha na uuzaji wa kuku, Juma Omange, anasema miundombinu ya soko hilo si mizuri kwa kuwa ikinyesha mvua aliye ndani hana tofauti na aliye nje, na muda mwingi wafanyabiashara wanakimbia na kukaa nje kwa kuwa kuna hewa nzuri. (Soko la Kisutu halina uongozi wa jumla bali kila idara ina uongozi wake).

“Kama unavyoona majengo haya ni mafupi na chakavu, kila wakati tukitaka kufanya ukarabati tunazuiwa kwa ahadi kuwa serikali itajenga soko la kisasa, tunavyozungumza hapa tumeambiwa tarehe Aprili 30, mwaka huu, haitafika kabla ya kuondolewa kupisha ukarabati, lakini hatuoni dalili zozote,” anasema.

Kwa mujibu wa Omange, tangu miaka ya 1990 Manispaa ya Ilala imekuwa ikiahidi kujenga soko hilo, na mwaka jana viongozi wa vitengo waliitwa na kuelezwa kuwa serikali imepata mkopo wa Sh. bilioni 31 na wakati wowote ujenzi utaanza.

“Ahadi hizi tumeshazizoea labda safari hii zitakuwa za kweli, lakini imekuwa kawaida na hasa kikikaribia kipindi cha uchaguzi tunaambiwa tutajengewa soko la kisasa ambalo lipo kwenye makaratasi yao,” anasema.

Kwa mujibu wa Omange, soko la Kisutu lina wafanyabiashara 700, ambao hulipa ushuru wa Sh. 500 kwa wachuuzi; kuku na nafaka Sh 1,000 na viosk Sh. 1,500 kwa siku.

Sheria inataka halmashauri kubuni chanzo cha mapato na kukusanya, lakini zinatakiwa pia kuboresha chanzo kama ni masoko kuwa na miundombinu bora, na kurejesha asilimia 10 kwa wawakilishi wa wafanyabiashara.

Kauli ya Omange inaungwa mkono na Shabani Wambangulu ambaye anauza kuku sokoni humo kwa miaka 25 sasa.

Anasema hali sokoni huko siyo ya kuridhisha. Mabanda ni chakavu, mafupi na hakuna mifereji ya kupitisha maji ya mvua.

Kuhusu hatua ya kuboresha soko hilo, Ofisa Masoko wa Manispaa ya Ilala, Solomoni Mushi, anasema Tanzania Investiment Bank (TIB) imetoa mkopo wa Sh. bilioni 31 kwa ajili ya kujenga soko la kisasa la Kisutu, na tayari zabuni imetangazwa.

Afisa Masoko huyo, anakiri kwamba masoko mengi yanahitaji kuendelezwa, lakini Manispaa inashindwa kufanya hivyo kwa kuwa mapato yanayokusanywa ni kidogo ikilinganishwa na mahitaji.

Kwa mujibu wa Mushi, masoko ya Manispaa hiyo ni  machakavu yenye miundombinu duni na kinachofanyika kwa sasa ni ukarabati mdogo ambao haukidhi haja.

Kwa mujibu wa Mushi, wilaya ya Ilala ina jumla ya masoko, magulio na maeneo ya wazi 60, kati yake masoko ni 26, makubwa ni 11 ambayo kwa mwezi yanaingiza mapato ya Sh. milioni 206.

Akitoa mapato ya miezi minne kuanzia 2017 na kiasi kilichokusanywa kwa mwezi anasema ni Octoba (Sh. Mil. 182), Novemba (Sh. Mil. 164), Disemba (Sh. Mil. 184)) na Januari 2018 (Sh. mil. 206), na kwamba kwa mwaka kiasi cha Sh. bilioni 3.8 hukusanywa.

“Soko kubwa linalokusanya mapato mengi ni Ilala Sh. milioni 110 hadi 120 kwa mwezi, lina wafanyabiashara zaidi ya 4,000.Linafuatiwa na Buguruni linalokusanya Sh. milioni 40 likiwa na wafanyabiashara zaidi ya 3,500, Kisutu linakusanya Sh. milioni 8.8 kwa mwezi,” anabainisha.

“Asilimia 50 ya mapato ya masoko yanapotea kutokana na kukosekana kwa miundombinu mizuri, kama yangeboreshwa yangeweza kuingiza kiasi cha Sh. bilioni 5 hadi 6 kwa mwaka kutoka Sh. bilioni 3 za sasa,” anasema na kueleza zaidi:

“Masoko ni chanzo kikubwa cha mapato kwa halmashauri, yanatoa fursa kwa wakulima asilimia 70 wauze mazao yao, hivyo ni lazima mazingira yaandaliwe. Kukiwa na vizimba watauza na tutapata fedha, lakini kwa sasa mapato mengi yanapotea.” Soko la Buguruni

Katika soko la Buguruni, umefanyika ukarabati kwa kujenga majengo mawili ambayo hayajamaliziwa baada ya Manispaa kutokuelewana na Mkandarasi.

Mushi anasema soko hilo kwa mwezi linakusanya Sh million 40, na kwamba lipo kwenye mpango wa ujenzi wa jengo la kisasa, huku akieleza kuwa mchakato wa kulimalizia unakamilika.

Katibu wa soko la Buguruni, Furaisha Kambi, anasema lilianza miaka ya 70 likijengwa na wafanyabiashara na miaka ya 80 Manispaa ilijenga eneo dogo na toka wakati huo wanakusanya ushuru tu bila kuboresha miundombinu.

“Soko ni chakavu hadi wafanyabiashara wamejitolea kununua vifaa na kulijenga, jua na mvua viliwasumbua sana. Manispaa wanakusanya ushuru wanaondoka nazo zote hawaachi asilimia 10 ambayo ingesaidia kukarabati,” anasema na kufafanua:

“Walianza kujenga jengo, lakini hawakumaliza ni kama walitegesha maji yote yaingie sokoni, wameweka mabati bila vikingio na hatujui mwisho wake ni nini.

"Tupo kwenye wakati mgumu kwa kuwa bidhaa zinapangwa chini na maji mengi yanamwagika, wafanyabiashara walituomba wanunue mabati au kuweka majani ili waezeke hilo eneo waendelee na biashara, lakini Manispaa imekaa kimya.”

Kambi anafafanua kuwa soko lina wafanyabiashara wa jumla na rejareja zaidi ya 2,500 ambao hulipa ushuru wa kati ya Sh. 500 hadi 1,500 kwa siku.

Baadhi ya wafanyabiashara wanasema ujenzi wa majengo madogo waliona ni neema, lakini ni tabu kwa kuwa hayajamaliziwa kwa kuwekewa makingio ya maji ya mvua.

“Bado hatujaruhusiwa kujenga vizimba, tunapanga bidhaa chini (kama unavyoona), matunda yanaharibika, ni heri wangeturuhusu kumalizia ujenzi huu,” anasema Said Mohamed.

Aidha, Mushi anafafanua suala hilo kuwa Manispaa inatafuta mkandarasi wa kumalizia ujenzi baada ya mkandarasi wa awali kushindwa kutekeleza.

“Aliyepewa kazi ya kujenga soko hakumaliza kwa kwua fedha alizoomba zilikuwa kidogo, Mkurugenzi kabla ya kutuma wakaguzi kuhakiki fedha iliyotolewa na kazi iliyofanyika. Tutamalizia ujenzi karibuni tunatambua kero kwenye soko lile ni kubwa sana,” alibainisha.

Kwa mujibu wa Mushi, kazi za usafi zimetolewa kwa kampuni mbalimbali kwa kuwa Halmashauri haina magari ya kuzolea taka mengi yamekufa. Manispaa ya Temeke

Kama ilivyo katika masoko ya Manispaa za Ubungo na Ilala, uduni wa miundombinu umekithiri katika masoko yaliyoko Manispaa ya Temeke.

Mfano, soko la Temeke Sterio, lina miundombinu chakavu iliyojengwa tangu miaka ya 2000na haijawahi kukarabatiwa, na kwamba ni mali ya Manispaa na wafanyabiashara wako chini ya umoja.

Katibu wa soko la Sterio, Omari Mangilile, anasema soko hilo ililofunguliwa na Rais wa awamu ya tatu, Benjamini Mkapa, ni mali ya Manispaa ambayo inakusanya ushuru kila mwezi.

Anasema kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2016, soko hilo lina wafanyabiashara 4,000 waliogawanyika kwenye maeneo ya vioski 69, maduka manane, vyumba vya mitumba 36, vizimba vya dagaa na vitunguu 176, mabanda ya kuhifadhia kuku 52, vyumba vya baba na mamalishe 16, vyoo vitatu, na nje kuna vioski 18.

Anasema miundombinu ndani na nje ya soko ni mibovu, mitaro imechakaa, uzio unaozunguka soko ni mbovu na Januari mwaka huu ulianguka ukajeruhi watu watatu.

Anasema pia vioski vinavuja na kuna maeneo watu wanafanya biashara juani huku wakiwa wameweka maturubai. Hali huwa mbaya zaidi wakati wa mvua kwa hunyeshewa na bidhaa zao kulowana. Pia mvua huwafanya wanunuzi washindwe kuingia sokoni huko, hali inayowaathiri zaidi kimapato.

Kwa upande wa usafi, Mangilile ingawa jukumu hilo linapaswa kugharamiwa na Manispaa kwa kutumia pesa za ushuru wanazolipa, kazi hiyo inafanywa na wafanyabiashara wenyewe kwa kutoa Sh. 200 kila siku pamoja na ushuru wa Sh. 700.

Kilio cha wafanyabiashara hao pia ni kuwa na uzio na miundombinu ya umeme imara.

Salia Mzome, ni muuzaji wa vinywaji kwenye vioski sokoni hapo na anasema kwa ujumla miundombinu ni chakavu kiasi kwamba wakati wowote linaweza kutokea janga la moto au kubomoka.

“Vibanda vingi ni vya muda mrefu, madirisha yameharibika, nondo zimeondolewa, na kwa sasa wizi unafanyika sana kutokana na kwamba nondo nyingi zimeondolewa,” anasema Robert Kalawila, ambaye anafanunua kuwa licha ya uduni huo wa miundombinu kwa siku analipa Sh. 600, kati yake Sh. 400 ni za ushuru na Sh. 200 ya usafi.

Hata hivyo, wafanyabiashara wanalalamika kwamba licha ya kukusanya ushuru, Manispaa haifanyi maboresho yoyote katika soko hilo kwa madai kwamba hakuna pesa.

Mfanyabiashara anayepanga kwenye vioski analipa Sh 30,000 na bili ya umeme na ushuru wa kutwa ni Sh. 400, mpangaji wa maduka Sh. 50,000 kwa mwezi, mitumba, dagaa, kuku na mamalishe Sh. 15,000,na wafanyabiashara wote kila siku lazima walipe Sh. 400.

Pia wafanyabiashara wa muda wanalipa Sh. 400, na kulipia kuingiza mzigo kulingana na ukubwa wa mzigo.

Robert Kalawila, ambaye amefanya biashara sokoni humo kwa miaka saba sasa, anasema changamoto kubwa ni Manispaa kutotekeleza wanachoahidi licha ya wafanyabiashara kuwa watiifu kwa kulipa ushuru wote.

“Miundombinu kama barabara, mifereji na uondoshaji wa taka, havifanyiki, tunajiuliza fedha wanazokusanya zinakwenda kuboresha wapi na kusahau chanzo muhimu kama hiki?” Anahoji.

Vicky Mbonela anayeuza bamia, anasema mifumo ya mifereji ni mibovu, ukuta umebomoka, mapaa ni chakavu na barabara chakavu, licha ya kulipa ushuru wa Sh 800, ikiwa ni sh 400 ya ushuru wa kutwa na sh. 400 ya kuingiza kiroba cha bamia.

“Halmashauri inapokusanya mapato kwenye soko letu hawarudishi chochote, masoko mengine wanapata asilimia 10 ya makusanyo, tumeshahangaika sana kupata kiasi hicho cha fedha, ila imeshindikana kwa madai kuwa meneja wa soko yupo sokoni humo,” anasema katibu wa soko hilo Mangilile.

Katibu huyo anaongeza kuwa viongozi wa soko wanatoa ushirikiano mkubwa kufanikisha ukusanyaji wa fedha hizo, lakini Manispaa inakwepa kuwapa fedha hizo kwa kuwa wanaona ni fedha nyingi.

“Tunafuatilia kila wakati na majibu yao ni mazuri sana kuwa wamepokea malalamiko yetu wanayafanyia kazi, na siasa imekuwa nyingi sokoni wameona ndilo eneo la kujipatia kura kirahisi kwa kutudanganya. Lakini ikija kwenye utekelezaji hakuna kinachofanyika,” anasema Mangilile.

“Kilio chetu kikubwa ni kuboreshwa miundombinu, soko letu ni la kutiliwa mfano, iwapo wataweka vivuli kwa wafanyabiashara na kuwa na vizimba vilivyoboreshwa vya kufanyia biashara.”  Soko la Mbagala

Soko la Mbagala, pamoja na uwepo wa changamoto za jumla kama kwenye masoko mengine, lipo tatizo la soko kuzungukwa na wafanyabiashara wasiotambulika kwenye mfumo rasmi wa soko ambao wanapanga bidhaa nje kiasi cha kutishia kuua soko kuu.

“Wafanyabiashara wa nje wamekuwa na nguvu kuliko tulio ndani tunaolipa ushuru, cha kushangaza huko ambako siyo rasmi halmashauri inachukua ushuru pia. Wawatafutie eneo la kuwaweka ili tufanye biashara vizuri kuliko ilivyo sasa,” anasema Makamu Mwenyekiti wa soko, Mohamed Omari.

“Tulio ndani tunalipa ushuru kila siku, lakini walio nje ambao ni wengi hawalipi chochote, soko linakufa kwa kuwa watu wanaona ndani hakuna biashara wanaenda nje kuuza,” anasema Shaka Kawabwa, mjumbe wa uongozi wa soko.

“Kwa muda mrefu tumepewa ahadi ya kujengewa soko la kisasa, na hata wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu ahadi ni hiyo hiyo, na hivi karibuni wafanyabiashara wa nje wameruhusiwa kutumia maeneo ya yanayozunguka soko jambo linaloua soko kuu.” 

“Kama Manispaa inashindwa kuboresha soko hilo, watutafutie fedha kama Sh. milioni 20 tuboreshe angalau kipindi cha mvua ili kupunguza matope kuliko hali ilivyo sasa,” anasema Mwenyekiti.

Alisema kwa sasa kuna utata wa wafanyabiashara wa nje ambao wanazidi kuongezeka kila siku na sasa wateja hawaingii tena ndani ya soko.

Mwenyekiti huyo anasema fedha inayokusanywa sokoni humo hairudi kuhudumia soko, kwa kuwa wanachangishana kwa ajili ya kunyonya maji machafu na kuboresha sehemu ya machinjio.

“Tunajiuliza fedha zinazokusanywa kila siku na Manispaa zinakwenda wapi na ni kwa ajili ya nini kama haziwezi kuboresha soko na kuwa na eneo zuri la kufanyiabiashara.” 

Soko la Tandika

Baadhi ya wafanyabiashara wanasema pamoja na ukongwe wa soko hili lilioanza miaka ya 70, hakuna maboresho yaliyofanyika na hivyo kujikuta wanafanya biashara kwenye mazingira magumu huku wakitakiwa kulipa kodi ya vizimba na ushuru kila siku.

Makamu Mwenyekiti wa soko hilo, Mohamed Jongo, anasema lilianza mwaka 1977, lina ukubwa wa ekari moja likiwa na wafanyabiashara takribani 800 wa kuuza nafaka, matunda, samaki na mama lishe ambao hulipa ushuru na kodi ya mwezi.

“Tuna soko la ‘L’lilijengwa mwaka 1977 halijawahi kukarabatiwa, na kuna jingine la samaki mwaka juzi lilijengwa kwa ushirikiano baina ya wafanyabiashara na wananchi,” anasema.

Aidha, changamoto kubwa iliyopo ni miundombinu duni ambayo hakuna mifereji ya kundoa maji na hivyo kipindi cha mvua maji kukosa pa kwenda.

“Miundombinu duni inaathiri biashara, kuna kipindi wateja wanapungua kwa sababu wanashindwa kuingia kufanya manunuzi,” anasema.

Jongo anasema mara kadhaa wameomba maboresho na hata walipoomba ruhusa ya kamati ya soko kushirikiana na wafanyabiashara kujenga mabanda upya hawakupewa. Meneja masoko Temeke

Meneja wa masoko wa Manispaa ya Temeke, Johnson Makalanga, anasema kuna jumla ya masoko 25; kati yake 20 yanakusanya ushuru, lakini kuna changamoto kubwa ya miundombinu bora.

“Soko la la Temeke Sterio ndiyo kubwa lenye wafanyabiashara zaidi ya 4,000 na linaongoza kimapato ya Sh. milioni 100 hadi 140 kwa mwezi linalouza bidhaa zote za kutoka shamba ikiwa ni jumla na reja reja,” anasema.

Anasema soko jingine ni la Tazara linalokusanya Sh. milioni 14 likifuatiwa, Tandika Sh. milioni 7 kwa mwezina Charambe Sh. milioni 10 na Mbagala Sh. milioni 7.

Kwa mujibu wa Makaranga, kwa sasa masoko ya Manispaa hiyo yanaingiza Sh.1.1, na kwamba ikiwa sheria ndogo mpya za mwaka 2017 zitapitishwa na Waziri kwa ushuru wa sh 300 kwa kila kizimba kwa siku watakusanya Sh. bilioni 2.6 kwa mwaka.

Aidha, alisema kuna baadhi ya masoko madogo wamejenga wenyewe ikiwamo la Kilamba kata ya Charambe ambalo lilijengwa na manispaa lakini halina wafanyabiashara.

Alisema mengine yatajengwa na wafadhili kwa mpango wa ushirikiano na sekta binafsi ili kufikia lengo la kuwa na masoko ya kisasa.

“Tunampango wa muda mfupi wa uboreshaji na Benki ya Dunia wanafanya upembuzi yakinifu kwa soko la Temeke Sterio ili liweze kujengwa la kisasa,” anasema Meneja huyo.

Kuhusu kurejesha asilimia 10 ya mapato kwenye uongozi wa soko, anasema hairejeshwi kwa kuwa usimamizi wa masoko kwa asilimia 100 unafanywa na Manispaa na hawaoni sababu ya kuwapa fedha hizo kwa kuwa zinatumika vibaya na jukumu la kusafisha soko ni la Manispaa.

“Uzalishaji wa taka ni mkubwa sana, kipindi cha matunda soko la Temeke Sterio linatumia Sh. milioni moja kwa siku na Sh. milioni 30 kwa mwezi,” anafafanua.

Aidha, anasema masoko mengine yanakufa kutokana na wafanyabiashara kukim

bilia barabarani na hakuna sheria inayozuia watu kufanyabiashara kokote kiasi cha kutumia uhuru huo kupanga bidhaa kokote.

“Wilaya ya Temeke inachangamoto hii kwa kiasi kikubwa, wafanyabiashara wanayaacha masoko na kupanga bidhaa maeneo mengine, mnunuzi akishuka kwenye daladala anapata bidhaa amabzo angezipata sokoni. Athari yake ni kuwa Manispaa inakosa mapato na masoko yanakufa,” anasema.

Anasema soko la Sterio linapokea magari zaidi ya 100 yanayoshusha bidhaa mbalimbali, na kwamba maboresho yaliyopo ni ya muda mfupi kulingana na kilichoharibika.

Kuhusu mapato, anasema bajeti ya Manispaa hiyo ni Sh bilioni 30 kwa mwaka, na kati yake Sh. bilioni 2 zinatoka kwenye masoko, huku akitolea mfano mwaka 2017/18 bajeti imeongezeka hadi Sh. bilioni 37 na makaridio ya makusanyo ya masoko ni Sh. bilioni 2.2

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita anathibitisha kuwa “Kuna mambo mengi (ambayo) kama jiji halijatimiza" na kufafanua "kama ubora wa vyakula vinavyoingia na kutoka, kujua masoko yote ni muhimu kwa wananchi, hatujakusanya vizuri ushuru wa kungiza bidhaa ndani ya masoko na kuboresha miundombinu". 

"Tuliweka mpango wa kujenga masoko ya kisasa na bado tuna nia hiyo.

“Jiji siyo wanufaika wa moja kwa moja maana vyanzo vyote vipo chini ya Manispaa na kazi yetu ni kuangalia na kuhakikisha yanafanya vizuri. Hiyo ni baada ya kuwa na mvutano nao baadaye tuliamua kuyaacha masoko chini yao.” 

Kuhusu kwa nini masoko hayajengwi na kuwa katika hali bora, alisema wafanyabiashara masokoni hawalipi fedha na zinazolipwa ni kidogo ambazo haziendani na huduma inayohitajika kama uondoshaji wa taka kwa mwezi ni Sh. mil 100 na soko linaingiza Sh mil 200, kabla ya makato ya mishahara ya wafanyakazi.

“Kutokana na kipato kidogo Halmashauri inashindwa kuendesha masoko. Pia mamlaka zinazosimamia zimeshindwa kwa kuwa hakuna ufuatiliaji.”

Kwa mujibu wa Meya huyo, mwaka huu Manispaa zilihimizwa kukopa ili kuboresha masoko, huku akitolea mfano wa wilaya za Ilala na Kinondoni ambazo wamepewa Sh. bilioni 10 kwa ajili ya kuboresha masoko.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Equality for Growth, Jane Magigita anasema asilimia 85 ya Watanzania wako sekta isiyo rasmi na masoko ni chanzo kikubwa cha mapato na ajira, lakini hakuna anayeyajali zaidi ya kukusanya mapato tu.

“Tumefanya utafiti kwenye masoko ya Dar es Salaam na tumebaini mengi yamejaa, hayana mifumo ya maji taka, chemba zinamwaga majitaka ovyo, mabanda ni chakavu na hakuna vizimba vya biashara, sakafu, mpangilio mbovu, lakini cha kusikitisha kinachoangaliwa ni ukusanyaji wa fedha bila kuboresha chanzo husika,” anasema Magigita.

Anasema masoko mengi yanakufa kutokana na uwepo wa siasa ambazo zinaruhusu watu kufanyabiashara nje ya masoko na kuwafanya walio ndani kutoka kwa kuwa hawatengenezi faida.

“Kuna kauli za migongano kwa viongozi wetu kuhusu masoko, ndiyo maana wafanyabiashara wamezagaa,watu wanaangalia maslahi yao ya kisiasa na wanafanya siasa kwenye masoko kwa kuwa kuna watu wengi, lakini hakuna sera wala sheria ya kuwatambua wafanyabiashara hawa hivyo wameachwa kwa kuwa wanatumiwa kwa manufaa ya kisiasa.” 

Magigita anasema toka waanze kazi mwaka 2009, kila Manispaa ilisema itajenga masoko ya kisasa, lakini hadi sasa hayajajengwa na cha kusikitisha, michoro iliyobuniwa siyo rafiki kwa biashara husika na hivyo upo uwezekano mkubwa wa kutofanikiwa.

Anasema mfano mzuri ni jengo la Machinga Complex ambalo lilijengwa kwa muundo wa ghorofa, lakini wafanyabiashara hawakunufaika nalo kwa kuwa wateja wako maeneo ya chini na hivyo kujikuta wanarudi eneo la chini, na kwamba upo uwezekano wa kujenga majengo ya kuvutia wateja kuliko maghorofa, na sasa limebaki kuwa mradi ulioshindwa.

“Watendaji wamebeba kauli za kisiasa wanakusanya fedha, lakini hawarudishi huduma kwenye masoko na kinachosemwa ni kuwa makusanyo ni madogo, hii yote ni kukosa vipaumbele kwa fedha yote kuwekwa kwenye kapu moja na kufanya shughuli nyingine na kuacha kutumika kuboresha chanzo husika,” anafafanua.

“Huwezi kukamua ng’ombe bila kumpa malisho, masoko ya Dar ni mabaya sana, machafu, hayana mpangilio maalum na halmashauri zinashindwa kuyajali na kukamua maziwa (fedha) kila uchao bila kujali afya za watumiaji na walaji."

Habari Kubwa