RIPOTI MAALUM: Serikali inavyokosa mabilioni michezoni-2

09Aug 2016
Na Waandishi Wetu
Nipashe
RIPOTI MAALUM: Serikali inavyokosa mabilioni michezoni-2

WAKATI Mamlaka ya Mapato (TRA) imepandisha makusanyo kutoka wastani wa Sh. bilioni 800 kwa mwezi kabla ya Novemba mwaka jana hadi kufikia wastani wa Sh. trilioni moja kwa mwezi.

waziri wa michezo, nape nnauye.

Bado serikali inakosa mabilioni ya shilingi kutokana na ada za usajili na mishahara ya wachezaji na makocha wa soka nchini kutokatwa kodi.

Katika sehemu ya kwanza ya ripoti hii jana, aliyekuwa kocha mkuu wa Simba, Muingereza Dylan Kerr alieleza kuwa mshahara wake haukukatwa kodi katika kipindi chote alichokuwa mwajiriwa wa klabu hiyo ya Msimbazi.

Aidha, wachezaji mbalimbali wa soka nchini walisema mishahara na ada za usajili wao hazikatwi kodi, hivyo kuikosesha serikali mapato.

Pia tuliona jinsi kadhia hiyo ya ukwepaji kodi inavyokinzana na dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais John Magufuli kuimarisha uchumi wa nchi na kupanua wigo wa ukusanyaji kodi. Sasa endelea ...

VIONGOZI WA TIMU WALONGA

Katibu mkuu wa timu ya JKT Ruvu Stars, Ramadhani Madoweka alisema waliambiwa na Mamlaka ya Mapato (TRA) mwishoni mwa mwaka jana kuwa kuanzia Januari waanze kulipa kodi ya mishahara ya wachezaji na makocha wao, lakini hawakutekeleza agizo hilo kutokana na kutoujua mfumo rasmi wa kufikisha kodi kwenye mamlaka hiyo.

"Tulianza kuwakata kodi (wachezaji) Januari kwa kutoa kile kiwango kinachotakiwa kulingana na chati ambayo TRA ilitupa wakati ikitoa semina mwishoni mwa mwaka jana.

Tulitekeleza agizo hilo kwa mishahara ya Januari lakini hata hatukujua TRA itazipata vipi fedha hizo," Madoweka alisema. "Baadaye tukazirudisha kwa wachezaji wetu tuliowakata."

"Pengine TRA itauweka sawa mfumo wake ili tuwe tunalipa kodi. Sisi suala la ulipaji kodi tumeshaliweka rasmi kwenye mikataba mipya ya wachezaji na tunangoja mfumo tu maana kwa sasa tunalipa mishahara yetu dirishani kwa baadhi ya wachezaji.

"Tuna makundi mawili ya wachezaji kwenye timu yetu.

Wapo wachezaji ambao ni watumishi wa jeshi (Jeshi la Kujenga Taifa), hao wanakatwa kodi kwa sababu wanafuata mfumo rasmi wa ulipaji kodi ya PAYE wakiwa ni wafanyakazi wa jeshi.

"Kundi la pili ni la wachezaji ambao si watumishi wa jeshi letu. Hawa tunawapa fedha zao bila kupita benki, hivyo hakuna kodi wanayokatwa," alieleza zaidi Madoweka.

Katibu wa Mwadui FC, Ramadhani Kilao alisema walianza kuwakata kodi wachezaji na makocha wao Januari mwaka huu baada ya TRA kutoa semina kwa timu za soka nchini kuhusu umuhimu wa ulipaji kodi.

"Baada ya TRA kuendesha semina ya kodi, sisi (Mwadui FC) tulitekeleza mara moja kwa kuhakikisha wachezaji wetu wanalipa kodi.

Tangu Januari wachezaji wetu wamekuwa wakilipa kodi. Mwadui FC ni timu ya kampuni ya Petra Diamonds na watumishi wa timu ni watumishi wa kampuni, wachezaji nao ni sehemu ya kampuni, hivyo sasa nao wanalipa kodi," alisema Kilao.

"Hata kwenye usajili sasa tunahakikisha kipengele cha makato ya kodi kinakuwapo na wachezaji wanakatwa kodi kwenye fedha zao za ada ya usajili," alisema zaidi kiongozi huyo wa timu hiyo ya mgodini.

Mtendaji Mkuu wa Azam FC, Saad Kawemba alisema baada ya semina ya TRA, walianza kulipa kodi kwa serikali kutokana na makato ya PAYE ya mishahara ya watumishi wao na kodi ya ada za usajili wa wachezaji.

"Tangu TRA walipotoa agizo la kuanza kukata kodi kwenye mishahara ya wachezaji na watumishi wengine wa timu, sisi tulianza kutekeleza mara moja.

Tunalipa kodi kwa serikali, lakini tumeshtushwa na taarifa kwamba baadhi ya timu hazijaanza kutekeleza agizo hilo. Hii si sawa," alisema Kawemba.

"Kanuni na taratibu zipo wazi - mchezaji lazima awe na mkataba na tumeagizwa na serikali kuwa kuanzia Januari mwaka huu kuwe na kipengele cha kodi."

UKWEPAJI KODI WA BIL 1.6/-

Desemba 4, mwaka jana, TRA ilizuia fedha kwenye akaunti zote za TFF ikilitaka shirikisho hilo lenye mamlaka ya juu ya soka nchini kulipa jumla ya Sh. 1,637,334,000 ikiwa ni kodi ambayo lilikwepa kipindi cha kuanzia mwaka 2010 hadi 2013.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa Idara ya Elimu na Huduma kwa Walipa Kodi wa TRA, Richard Kayombo, sehemu kubwa ya kodi hiyo ilikuwa PAYE ya waliokuwa makocha wa timu za taifa za soka, Mbrazil Marcio Maximo na Wadenmark Jan Poulsen, Kim Poulsen na Jacob Michelsen.

Sehemu nyingine ya deni hilo ilitokana na kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) katika mchezo wa timu ya taifa ya soka (Taifa Stars) dhidi ya Brazil uliofanyika Juni 7, 2010 kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam na kuingiza Sh. bilioni 1.7.

Kwa mujibu wa aliyekuwa katibu mkuu wa TFF, Frederick Mwakalebela wakati akitangaza mapato ya mchezo, mechi ya Taifa Stars dhidi ya Brazil iliyomalizika kwa wageni kushinda 5-1 iliingiza Sh. bilioni 1.674.

Mwaka 2014, aliyekuwa naibu waziri wa iliyokuwa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia, aliiambia Nipashe kuwa makocha wa Taifa Stars katika utawala wa Serikali ya Awamu ya Nne walikuwa wanalipwa na serikali mshahara wa dola za Marekani 12,500 kwa mwezi.

Baada ya TRA kuzizuia akaunti zote za TFF, rais wa shirikisho hilo, Jamal Malinzi, alisema hawakuwajibika kuwakata kodi walimu hao wa timu za taifa kwa kuwa mishahara yao ilikuwa inalipwa na serikali.

Malinzi pia alisema mchezo kati ya Taifa Stars na Brazil ulisimamiwa na kamati maalum ya serikali na fedha zake hazikuingizwa kwenye akaunti za TFF.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Nape Nnauye, wakati wa mjadala wa makadirio ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2016/17, alikiri bungeni mjini Dodoma Mei 13 kuwa TFF haihusiki na kadhia ya ukwepaji kodi iliyokuwa inaikabili, hata hivyo.

Nnauye alisema serikali inapaswa kulaumiwa kwa kutokata fedha za PAYE katika mishahara ya makocha wa timu za taifa ambao walikuwa wanalipwa na Hazina.

"Tatizo ni la serikali. Mshahara ulikuwa unalipwa na Hazina, TFF na Hazina walitegeana kukata kodi ya PAYE. TRA inamjua mteja wake ni TFF ndiyo maana imekuwa ikimfuata mara kwa mara na kuchukua fedha," alisema Nnauye.

"Hata pesa za mechi ya Brazil, TFF haihusiki."

Nnauye alisema kulikuwa na kamati iliyoundwa kuratibu mechi hiyo (ambayo ilikopa Sh. bilioni tatu kutoka benki ya NMB kufanikisha mechi hiyo). "Tumekubaliana aliyepaswa kuilipa, ailipe na serikali inalisimamia vyema jambo hili," alifafanua zaidi waziri huyo.

Wakati sakata hilo linafikishwa bungeni siku hiyo na Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma a Maendeleo ya Jamii, Peter Serukamba, tayari TRA ilikuwa imechukua fedha zote zilizokuwamo kwenye akaunti za TFF kiasi cha Sh. milioni 407.

ITAENDELEA KESHO

Habari Kubwa