RIPOTI MAALUM Uhaba wa walimu janga elimu nchini

31Dec 2019
Sanula Athanas
Igunga
Nipashe
RIPOTI MAALUM Uhaba wa walimu janga elimu nchini
  • *Miongo miwili usomaji sayansi wa kubahatisha

UNAPOZUNGUMZIA utekelezaji wa wito kwa wanafunzi, hasa wa sekondari, kuzama zaidi katika masomo ya sayansi na Hisabati, kwa Shule ya Sekondari Ziba kuna kiashiria cha njia panda, ikiangukia sababu ya 'nani atawafundisha?'

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, alipozuru katika Shule ya Sekondari Ziba wilayani Igunga kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo Agosti mwaka huu.

Dhana hiyo ikielekezwa mahsusi kwa somo la Fizikia, mwonekano unakuwa dhahiri zaidi katika sura mbili tofauti, kati ya kipindi shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2000 na 2015, huku zama inayofuata ni miaka minne kuanzia 2015 hadi sasa.

Nipashe ilimpomdadisi Makamu Mkuu wa Shule hiyo, Frank Milazi, alianza kutoa picha ya jumla kuhusu kile kinachojiri katika sekondari hiyo ya kata iliyoko kilometa 57 magharibi mwa Mji wa Igunga mkoani Tabora, akifafanua:

"Hapa hatuna mwalimu wa Fikizia aliyeajiriwa na serikali kwa miaka minne sasa. Shule ilianzishwa mwaka 2000. Awali, alikuwapo Mwalimu Kabahoze aliyekuwa ameajiriwa na serikali kwa ajili ya somo hilo, lakini mwaka 2015 alipandishwa kuwa MEK (Mratibu Elimu Kata) na hakuajiriwa mwalimu mwingine kuziba pengo hilo."

Ili kuhakikisha somo hilo halikwami kutokana na uamuzi wa kiserikali miaka minne iliyopita, Mwalimu Milazi anaeleza mbinu mbadala ambayo uongozi wa shule ulichukua, ni kutafuta walimu wawili wa kujitolea kwa malipo kidogo, kuziba pengo lililojitokeza.

Hata hivyo, katika kipindi cha miaka 15 tangu kuanzishwa kwa shule hiyo, mwalimu wa Fizikia aliyekuwapo, alibeba mzigo uliopitiliza kulingana na wastani wa idadi ya wanafunzi anaopaswa kufundisha.

Kisera, inaainishwa kwamba tija ya mwalimu na mzigo unaobebeka kwake ni anapokuwa na wastani wa wanafunzi 45 kwa darasa. Kwa maana hiyo, wastani unaojidhihirisha hapo ni kuwapo uhitaji wa walimu 20 sekondari ya Ziba yenye wanafunzi 914 (wavulana 317 na wasichana 597).

Kilio cha Mwalimu Milazi kinaenda mbali zaidi, akilalamika kwamba uhaba huo pia unaangukia masomo ya Kemia na Baiolojia, ambayo ndiyo wabia wakuu wa Fizikia katika sayansi, kila somo lina mwalimu mmoja.

Shule ya Sekondari Ziba kwa sasa ina jumla ya walimu waajiriwa 16 na wawili wa kujitolea, ambao ndiyo wamejikita katika somo la Fizikia.

"Kwa kifupi ni kwamba, tuna tatizo la uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi hapa. Tunaiomba serikali itupatie walau walimu wanne, wawili wa Fizikia na wawili wa Kemia na Baiolojia," anapendekeza na kuongeza kilio kingine kwamba:

"Hatuna nyumba za walimu za kutosha, tuna nyumba tatu tu! Hivyo, walimu 15 hawaishi karibu na maeneo ya shule, wanaishi huko mitaani wamepanga."

WALICHOFANYA 'DEI WAKA'

Licha ya mtihani wa uhaba wa walimu iliyonao Ziba, pia imedumu na uhaba wa miundombinu kama mabweni, bomba rasmi la maji na bwalo la chakula yanayoonekana kwa mara ya kwanza mwaka huu katika miongo miwili ya uwapo wake.

Katika matokeo ya Mtihani wa Taifa wa Kidato cha Nne mwaka jana, wanafunzi wa shule hiyo walioandaliwa kwa hatua zote kwenye somo la Fizikia na walimu wa kujitolea, kuna kiwango cha ufaulu ambao 'wameambulia'.

Kati ya watahiniwa 117 katika shule ya Ziba, 48 ndiyo waliofanya mtihani wa somo la Fizikia na kati yao, 27 walipata ufaulu kuanzia alama 'D' na 21 walifeli kwa maana ya kupata alama 'F'.

Matokeo hayo yanaonesha, waliopata alama 'D' jumla yao ni 22; alama 'C' wako wanne; na mmoja ndiye alipata alama 'B', akiwa na kiwango cha ufaulu cha daraja la kwanza alama nane, akiongoza wilaya kwa shule za serikali na yumo katika orodha ya waliofanya vizuri kimkoa.

DED ANASEMAJE?

Udadisi wa Nipashe, ulihamia kutafuta majibu yanayotoa mwanga kwa kiza kinachoikabili shule hiyo, mezani kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya (DED) ya Igunga, Revocatus Kuuli, anayekiri upungufu huo akisema:

"Ni kweli pale Shule ya Sekondari Ziba hakuna hata mwalimu mmoja wa kuajiriwa na serikalini kwa ajili ya somo la Fizikia. Sisi tunapokea walimu kutoka serikalini, tatizo letu hili la uhaba wa walimu tumeshalipeleka Wizara ya Elimu (Sayansi na Teknolojia) na Ofisi ya Rais-Tamisemi, linashughulikiwa huko.

"Tatizo la uhaba wa watumishi Igunga ni kubwa, si kwa walimu tu, bali tuna uhaba mkubwa wa watumishi katika sekta nyingi. Tuna uhaba wa watendaji wa kata na vijiji.

"Kwenye sekta ya afya ndio balaa zaidi, tuna uhaba mkubwa na tumewaandikia barua Wizara ya Afya walishughulikie hili. Kuna vituo vya afya vinne hatutoi huduma za upasuaji kwa sababu hatuna wataalamu. Nafikikiri uhaba wa watumishi si tatizo la Igunga tu, bali la nchi nzima."

HATUA ZA KIBUNGE

Wajibu mkuu wa mbunge ni kutetea maslahi ya wananchi katika eneo lake. Je, kwa shule ya Ziba amefanya nini? Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali, anasema kwa nafasi yake, akiwa daraja kati ya mhimili wa shule na ngazi ya juu, ameshawasilisha maudhui ya kilio hicho kwa mamlaka za juu zichukue hatua.

Vilevile, anasema kwa yaliyo chini ya uwezo wake, amekuwa mbia wa uongozi wa shule na mamlaka nyinginezo katika halmashauri na uongozi wa wilaya, akitaja kushuriki ujenzi wa miundombinu kama mabweni, madarasa na vyanzo vya maji.

"Nimekuwa nikitumia fedha za Mfuko wa Jimbo na wakati mwingine za mfukoni mwangu kuhakikisha shule hii (Ziba) na nyinginezo jimboni zinajengwa," anasema na kuongeza ni matarajio yake kilio cha dai la walimu kitapatiwa majibu kutoka mamlaka husika.

Katika taarifa yake bungeni kwenye kikao cha Bunge la Bajeti Mei 22, 2017, Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma na Maendeleo ya Jamii, ilieleza kuwa Tanzania inakabiliwa na uhaba wa walimu 252,693 wa shule za msingi na sekondari.

Aliyekuwa mjumbe wa kamati hiyo, Mbunge wa Nzega Mjini, Hussein Bashe (sasa Naibu Waziri wa Kilimo), aliliambia Bunge kati ya walimu wanaohitajika, 182,899 ni wa shule za msingi na 69,794 wa sekondari.

Katika kinachoonesha uhaba huo wa walimu una mustakabali wa kitaifa, Mbunge wa Mwanga mkoani Kilimanjaro, Profesa Jumanne Maghembe, aliibua kilio cha aina hiyo katika kikao cha Bunge cha Mei 8 mwaka huu, akidai jimbo lake lina uhaba wa walimu 384 wanaohitajika haraka.

MAJIBU YA SERIKALI

Naibu Waziri Ofisi ya Rais (Tamisemi), Mwita Waitara, anaungana na sauti ya vilio vinavyopazwa kuhusu uhaba wa walimu, lakini takwimu zikiwa tofauti na idadi iliyowasilishwa na Kamati ya Bunge miezi 31 iliyopita.

Waitara ambaye ni Mbunge wa Ukonga, anatoa takwimu za uhaba walimu kitaifa kwamba ni 80,000. Kati yao, 66,000 wanahitajika kwa ajili ya shule za msingi zaidi ya 16,000; na waliobaki 14,000 ni wa kufundisha sekondari zisizopungua 4,000.

Kuhusiana na utekelezaji wake, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Laurean Ndumbaro, alisema wiki iliyopita matarajio ya serikali ni kuajiri watumishi wapya zaidi ya 40,000 katika kada mbalimbali, wakiwamo walimu katika kipindi cha miezi miwili ijayo.

"Katika mwaka wa fedha 2019/20, serikali imetenga idadi hiyo ya ajira ambazo zitaanza kutolewa Februari 2020, zikiwamo za kada afya na elimu ambazo zitasaidia kukabiliana na uhaba wa watumishi," anasema.

AHADI YA OLE NASHA

Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, William Ole Nasha, aliyezuru Shule ya Sekondari Ziba mwaka huu, anaungana katika orodha ndefu ya wanaokiri pengo kubwa lililopo kitaaluma na anaeleza mikakati ambayo serikali inachukua.

Bila ya kutaja kipindi maalum, Ole Nasha, akizungumza na Nipashe jana, alisema serikali ilishachukua hatua ya kuajiri walimu 18,000 kwa mwaka wa fedha uliopo na inatarajia kuajiri wengine 16,000 mwanzoni mwa bajeti ijayo, akiahidi kusikilizwa kwa kilio cha Ziba.

Pia alifafanua undani wa chanzo cha uhaba uliopo wa walimu kitaifa kwa kiasi kikubwa umechangiwa na hatua ya serikali kuwafuta kazi watumishi waliokosa sifa baada ya kufanyika uhakiki, walimu wakiwa miongoni mwao.

Hata hivyo, alitoa angalizo kwamba kwa mujibu wa taratibu, mamlaka ya wizara yake ni kuibua madai na wenye mamlaka ya kuajiri ni Tamisemi, ingawaje alisisitiza matarajio ya utekelezaji.

Naibu Waziri huyo alidokeza mkakati mmojawapo wa kuongeza walimu wa sayansi, ni kuajiri kundi kubwa la wahitimu wa sayansi zaidi ya 5,000 kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), watakaopewa mafunzo maalum ya ualimu.

Habari Kubwa