RIPOTI MAALUMU; Kina Ziwa Tanganyika kilivyoliza wajasiriamali-2

25Jan 2022
Salome Kitomari
KIGOMA
Nipashe
RIPOTI MAALUMU; Kina Ziwa Tanganyika kilivyoliza wajasiriamali-2

KATIKA sehemu ya kwanza ya ripoti maalum hii, wanawake wajasiriamali wa samaki na dagaa waliokuwa kwenye Mwalo wa Kibirizi, mkoani Kigoma, wakieleza hali ngumu ya uchumi baada ya kuongezeka kwa kina cha maji cha Ziwa Tanganyika, katika sehemu hii ya mwisho watafiti,...

Baadhi ya wavuvi na wanawake wajasiriamali wa dagaa na samaki wakiwa kwenye mwalo wa Kibiziri, ambao umefunikwa na maji kutokana na kuongezeka kwa kina cha maji. PICHA: MPIGAPICHA WETU

... serikali inafafanua hatua zilizochukuliwa. Endelea…

Anasema biashara wanazofanya kwa sasa zinawawezesha kupata faida ya Sh. 3,000 au 4,000 ambayo hawawezi kuigawa kwa ajili ya mahitaji ya familia na kusomesha watoto na ndiyo maana hadi sasa mwanawe hajaenda shule anasubiri kupata sare za shule.

Naye Hadija Sabuni, mkazi wa Karago, anasema alihamia eneo la biashara na familia yake lakini baada ya kina cha maji kuongezeka ilibidi ahame na sasa anafanyabiashara ndogondogo.

 

“Maji yameingia kwenye Mwalo huwezi tena kuuza, wateja wameondoka hatuna mahali pazuri pa kununua mzigo, tumeanguka kiuchumi sana kwa sasa tumeishia kupata fedha ndogo ndogo, kazi kuuza samaki na dagaa niliitegemea kusomesha watoto,” anasema.

Anasema kuna nyumba zimeanguka na kuzolewa na maji, lakini wanaamini mipango ya Mungu kwa kuwa ndiye mpangaji, na sasa wamebaki kuomba msaada wa ndugu walioko mjini ili maisha yaweze kuendelea.

Aisha Zuberi, Mkazi wa Livingi Stone anayefanyabishara ya masende, anasema amegeukia biashara ya maandazi ambayo nayo ni shida sana kupata wateja.

“Boti zinakuja bure wanauza kwa shida, anasema mtaji wake ulikuwa 200,000 na aliweza kuuza na kupata kati ya Sh. 15,000 hadi 20,000 na kupata watoto, na sasa nimeingia kwenye kufuma mashuka na kuuza maandazi ili niendeshe familia,” anasema.

Aidha, anaiomba serikali kuwasaidia kwa kuwajengea eneo jingine la biashara ili maisha yaweze kuendelea.

Zawadi Mfaume, anasema alianza kuuchuza samaki wabichi tangu mwaka 1992, amesomesha mwanawe hadi kidato cha nne na kujenga nyumba kwa kazi hiyo, lakini changamoto kubwa ni kuongezeka kina cha maji ambako kumewafanya waondoke kwenye eneo hilo.

“Baada ya kujaa maji eneo lile tulihamishiwa eneo hilo, tumechangamana wa mboga, samaki wa wabichi na wakavu na inawapunguzia watoto. Naendelea na hii kazi ili watoto wangu waende kusoma, nimesomesha watoto na kujenga nyumba.

Mwenyekiti wa Wafanyabiashara wa Samaki na Dagaa Kibirizi, Machumu Yenda, anasema changamoto kubwa ni upatikanaji wa uhakika wa samaki, kwa kuwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi hawapatikani kwa wakati.

“Hali ya sasa na zamani ni tofauti, mazao tunayoona sasa ni madogo mno ukianzia mwambao wa Kagunga hadi Kibirizi, lakini sasa wanavua kwenye kina kirefu na wanapatikana kwa tabu sana,” anasema.

Anasema asilimia kubwa ya wakazi wa Kigoma wanategemea Ziwa Tanganyika na kwamba hali imezidi kuwa ngumu, mzunguko wa zamani sio wa sasa, wanaiomba serikali kusaidia wapate zana bora ili wavuvi wakavue kirahisi.

Anasema kipindi cha nyuma soko hilo lilikuwa na uwezo wa kupokea tani tatu, lakini kwa sasa inapatikana nusu tani, hali ambayo imeshusha pato la mtu mmoja mmoja, mkoa na taifa kwa ujumla.

Suzanna Ezekiel, mmiliki wa zana za uvuvi na mchakataji katika Mwalo wa Kibirizi, anasema mabadiliko hayo yamewaathiri kwenye mnyororo wa thamani wa mazao yao, huku akisema kipindi cha masika na vuli hawana mahali pa kuanikia samaki kwa kuwa eneo limejaa maji.

Naye mvuvi George Kalea anasema, kutokana na kuongezeka kwa kina hicho wanalazimika kutumia vifaa vya kisasa ili kupata mazao lakini imeshindikana na matokeo yake kufanyakazi kwa mazingira magumu.

UTAFITI

Naye Mtafiti wa Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Prisca Mziray, anasema kasi ya upepo ambao husaidia maji kuchanganyika imepungua huku joto likiongezeka na kwamba kwenye maji kuna tabaka la juu ambao ni joto, la kati ni joto kiasi na la chini baridi na ili yachanganyike inabidi joto la kati ya tabaka moja na jingine isiwe kubwa sana.

“Sasa kutokana na joto kuongezeka sana linafanya tabaka la juu kuwa na joto sana kwa hiyo haya maji kuchanganyikana inakuwa vigumu, uwezo wa maji ya chini kuja juu inakuwa ngumu na ziwa linazidi kuwa na virutubisho vichache kwa ajili ya mazao ya uvuvi,” anasema.

Kwa mujibu wa mtafiti huyo, kuongezeka kwa shughuli za kibinadamu kama kilimo kandokando mwa Ziwa Tanganyika kumesababisha udongo kuingia ziwani ambao huharibu mazalia ya samaki kwenye miamba pamoja na maji ya viwandani ambayo huingia bila kutibiwa.

OFISA UVUVI

Ofisa Uvuvi Mkoa wa Kigoma, Ritha Mlingi, anasema hali ya uvuvi sio ya kuridhisha kwa kuwa mazao yake yamepungua na kinacholetwa kwenye mwalo kimepungua kwa kiasi kikubwa kutokana na mabadiliko ya tabianchi.

“Zamani mvuvi alikuwa akienda anarudi na hadi boxi tano hadi 20 kwa sasa wanakwenda zaidi ya mmoja anarudi na dagaa nusu ndoo, ni dalili kuwa hali ya uvuvi kwenye ziwa letu sio nzuri, pamoja na kiwango, lakini kuna ukubwa wa samaki mfano mgebuka ulikuwa unapatikana mkubwa ila sasa kwenye mialo rasmi na isiyo rasmi ni midogo sana,” anasema.

 

Aidha, anasema kuna aina ya samaki wamepungua na wengine wametoweka kabisa hali inayoonyesha kuwa hali sio nzuri na kuna hatua zinapaswa kuchukuliwa.

Kwa mujibu wa Mlingi, anasema utafiti utafanyika kujua kiwango cha samaki, na kwamba mabadiliko ya tabia nchi yamechangia kupungua kwa samaki, kwa kuwa ni viumbe ambao huathiriwa kwa haraka kukiwa na mabadiliko.

Anasema jingine ni kuongezeka kwa nguvu inayotumika kwenye uvuvi na kwamba zamani walikuwa wengi kwa kuwa walikuwa wachache, ila sasa wengi wameingia kama sehemu ya ajira na kusababisha kuongezeka kwa eneo la kuvua na uharibifu.

Anasema kwa mujibu wa sheria mtu anaruhusiwa kuvua umbali wa kilomita moja kuendelea kutoka kwenye fukwe, na atakayekutwa anavua chini ya hapo ni uvuvi haramu.

HATUA ZILIZOCHUKULIWA

Waliwahamisha wanawake wanaofanya ujasiriamali wa kuuza dagaa wakawapeleka kwenye masoko ya karibu na mialo na waliokuwa na maeneo ya kukaushia yaliyofunikwa na maji waliruhusiwa kujenga maeneo mapya.

“Tulijaribu kujaza maji kwenye mwalo wa Kizuiri ili yasiendelee kuingia na walihamishiwa eneo la jirani na kuna jitihada zinaendelea kuangalia nini kifanyike ili waendelee kufanya biashara zao vizuri zaidi,” anasema.

ZIWA TANGANYIKA

Kwa mujibu wa mtandao wa Wikipedia, Ziwa Tanganyika ni moja ya maziwa makubwa Afrika ya Kati ni la pili kwa ukubwa duniani kwa wingi wa maji limeenea mpakani mwa Tanzania ikiwa ni asilimia 46, likipakana na nchi za Kongo asilimia 40, Burundi na Zambia. Lina kina cha mita 1,470 na kilomita 600.

Ndani ya ziwa hilo sehemu ya Tanzania kuna Kisiwa cha Kupita, Kongo kuna visiwa vya Kavala, Mamba –Kayenda, Milima na Kibishie, huku Zambia kukiwa na Mutonowe na Kumbula.

WAZIRI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Selemani Jafo, anasema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha kuongezeka kwa kina cha maji Ziwa Tanganyika kwa mita mbili jambo ambalo ni hatari, na kwamba kwa sasa wanaendelea na utafiti huku wakihamasisha wananchi kupanda miti.

Ripoti hii imefadhiliwa na Chama cha Wachapishaji wa Habari Duniani (WAN-IFRA) kupitia Social Reporting Initiative (SIRI).

Habari Kubwa