Ripoti undani madudu Airtel yatua kwa JPM

12Jan 2018
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
Ripoti undani madudu Airtel yatua kwa JPM

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango, amekabidhi kwa Rais John Magufuli taarifa ya kamati aliyoiunda kuchunguza umiliki wa kampuni ya simu ya Airtel.

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango.

Desemba 20, wakati akiweka jiwe la msingi kuzindua ujenzi wa jengo la Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) mjini Dodoma, Rais Magufuli alimwagiza waziri huyo kufanya uchunguzi huo akidokeza kuwa kampuni hiyo ni mali ya umma, lakini kuna mchezo mchafu umefanyika kuchukua hisa za serikali.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, Ikulu, baada ya kuwasilisha taarifa hiyo, Dk. Mpango alisema serikali imejiridhisha kuwa ubinafsishaji wa Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kwenda Celtel, baadaye kuhamishiwa Zain na sasa Airtel ulifanyika kwa ukiukwaji mkubwa wa sheria, kanuni na taratibu.

Taarifa hiyo ilieleza kuwa kufuatia ukiukwaji huo, Dk. Mpango alisema serikali inayomiliki asilimia 40 ya hisa za kampuni ya Airtel, imeamua kufanya mazungumzo na kampuni ya Airtel inayomiliki asilimia 60 ya hisa, ili nchi ipate haki yake.

“Lakini niwaambie Watanzania yale ambayo tumeyaona ni machafu sana, ni mambo ya ovyo kabisa, nchi yetu kwa kifupi tuliingizwa mkenge, ni fedha nyingi zimepotea, kwa hiyo sisi katika majadiliano haya lengo letu litakuwa ni kuhakikisha Watanzania wanapata haki yao," Dk. alisema akinukuliwa katika taarifa hiyo ya Ikulu.

Taarifa hiyo pia ilieleza kuwa Rais Magufuli jana alipokea taarifa ya utekelezaji wa maagizo yake aliyoyatoa Novemba 25 wakati wa ufunguzi wa Hospitali ya Taaluma na Tiba ya Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Mloganzila) kutoka kwa Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

Baadhi ya maagizo hayo ni kupunguza baadhi ya idara na madaktari katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) na kuhamishia Mloganzila na hospitali za mikoa kuhamishwa kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwenda Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Taarifa ya Ikulu ilieleza kuwa Waziri Ummy aliwasilisha taarifa hiyo akiwa ameongozana na viongozi wakuu wa MNH, Taasisi ya Mifupa (MOI), Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKHI), Chuo Kikuu cha Tiba na Sayansi Shirikishi (Muhas).

Vilevile, taarifa hiyo ilieleza kuwa Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, amekamilisha kanuni za Sheria ya Madini Na. 7 ya mwaka 2017 na kuwasilisha vitabu vya kanuni hizo kwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi.

Ilieleza kuwa akiwa na Naibu Mawaziri wa Madini, Stanslaus Nyongo na Doto Biteko, Prof. Kabudi alisema kanuni hizo zimekamilika siku moja kabla ya tarehe ya mwisho iliyotolewa na Rais Magufuli na kubainisha kuwa sasa sheria inaweza kuanza kutumika.

Taarifa hiyo ya Ikulu ilisema Naibu Mawaziri wa Madini waliwataka Watanzania na wadau wote wa sekta ya madini kushirikiana na serikali kutekeleza sheria hiyo na kumpongeza Rais Magufuli kwa kutoa msukumo wa kukamilishwa kwa kanuni hizo.

Jumatatu, Rais Magufuli alimwagiza Prof. Kabudi kushirikiana na naibu mawaziri hao kuhakikisha kanuni hizo zinakamilika kufikia leo huku akiweka wazi kutoridhishwa na utendaji kazi wa Waziri wa Madini, Angellah Kairuki.