Ripoti ya ndege yaibua udhaifu

25Nov 2022
Na Mwandishi Wetu
BUKOBA
Nipashe
Ripoti ya ndege yaibua udhaifu

RIPOTI ya awali ya ajali ya ndege ya Precision Air, imeibua udhaifu katika utayari wa kukabili majanga nchini huku ikishindwa kumtaja Jackson Majaliwa, aliyeonekana shujaa katika ajali hiyo kutokana na kuokoa watu kadhaa, bali ikielezea wavuvi kuwa ndio waliosaidia katika uokoaji.

uzi, ripoti yenye taarifa hizo  ilisambaa kwenye mitandao ya kijamii na ikakanushwa baadaye na Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa,  kupitia ukurasa wa twiter, jana jioni Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Prof. Makame Mbarawa, alizungumza na waandishi wa habari kutoa ripoti ya awali.

Ripoti hiyo ilitolewa juzi na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi, ikiwa ni baada ya siku 14 tangu kutokea kwa ajali hiyo, Novemba 6, mwaka huu, na ndani yake hakuna sehemu iliyomtaja shujaa huyo.

Katika ajali hiyo, Majaliwa alijizolea umaarufu na kuitwa shujaa, baada ya kitendo chake cha kuokoa baadhi ya manusura wa ajali hiyo ndipo serikali ilipomzawadia kwenda kusoma mafunzo ya uokozi katika Jeshi la Zimamoto na Uokozi hatimaye kupewa ajira serikalini.

Ajali hiyo ilitokea wakati ndege hiyo ikitoka Dar es Salaam kwenda Mwanza kupitia Bukoba na ilianguka Ziwa Victoria na kusababisha vifo vya watu 19 na manusura 24.

Jana, Waziri Mbarawa alisema hali ya hewa katika Uwanja wa Ndege wa Bukoba iliripotiwa kuwa nzuri hadi saa 2:20 asubuhi lakini ilibadilika ghafla na mvua kunyesha ikiambatana na mingurumo ya radi na upepo mkali, mawingu mazito na ukungu.

Alisema ndege iliingia katika anga la Bukoba saa 2:25 asubuhi na kukuta hali ya hewa imebadilika dakika chache  na kuanguka takribani dakika 20.

“Baadaye rubani alianza matayarisho ya kutua katika njia ya ndege kuruka na kutua namba 31 kutoka uelekeo wa ziwa. Kutokana na maelezo ya manusura, njia ya kutua ilikuwa inaonekana pamoja na alama zake kabla ya ndege kutua kwenye maji,” alisema.

Waziri Mbarawa alisema uwanja huo uko katika hali nzuri ni wenye mwinuko wa futi 3,740 kutoka usawa wa bahari na una njia moja ya kuruka ndege yenye urefu wa kilomita 1.5.  Alisema kiwanja kina kituo cha zimamoto ambacho kina gari moja na kikosi cha wafanyakazi 10.

MLANGO WA NDEGE

Kuhusu mlango wa ndege ulivyofunguliwa, alisema ulifunguliwa na mhudumu wa ndege kwa msaada wa abiria.

“Kama ripoti ya uchunguzi ilivyosema wananchi waliokuwa wanafanya shughuli za uvuvi walifika dakika tano baada ya ndege kuanguka. Waliendelea  na juhudi za kufungua mlango kwa nje, hali iliyompa mhudumu wa ndege na abiria ujasiri wa kuendelea kufungua baada ya kuona nje ya ndege kuna msaada,” alisema.

Prof. Mbarawa alipoulizwa kwa nini Majaliwa hajatambuliwa, alisema ripoti haijataja jina la mtu ndiyo maana hata mhudumu na abiria hawajatajwa kwa majina.

VIKOSI VYA UOKOZI

 Kuhusu kuchelewa kwa vikosi vya uokozi, Mbarawa alisema “napenda kutoa ufafanuzi kuwa katika zoezi lote la uokozi pale ambako kuna ajali au janga lolote hususan ajali za majini upo muongozo wa kimataifa juu ya uendeshaji wa uokozi.”

“Tunaongozwa na mkataba wa kimataifa kuhusu masuala ya utafutaji na uokoaji majini, ambao umetoa mwongozo kwamba ajali kwenye maji au ajali inaruhusu mtu au kikundi cha watu walioko karibu na eneo la ajali kuwajibika kwa vyombo vya uokozi na kutoa taarifa kwa vyombo vya uokozi na wataendelea kushiriki hadi vyombo au wataalam wafike.

Alisema mwongozo huo unaendana na utamaduni wetu wa kusaidia kuokoa na ndicho kilichofanywa na wavuvi na kwamba walitimiza wajibu wao kizalendo na inakubalika kimataifa.

KUCHELEWA KWA BOTI

Alisema kuna boti ya uokozi na kwamba wakati wa ajali boti ilikuwa mbali kwenye kutekeleza majukumu yake ya doria na ilipofika shughuli za kuokoa zilikuwa zimekamilika.

Alikiri  kuwa uwezo wa kukabiliana majanga unatakiwa kuimarishwa ili kuokoa maisha ya watu.

Ripoti hiyo ilisema lengo halikuwa kutua kwenye maji kwani abiria hawakuambiwa wavue viatu au wavae makoti ya kujiokoa na matairi ya ndege yalifunguka kuashiria ndege ilikuwa tayari kutua uwanjani.

Ilieleza kuwa kilichotokea kilikuwa ghafla na rubani hakuwa amejiandaa nacho na kwamba iwapo uokoaji ungefanyika kwa wakati, watu wengi zaidi wangeokolewa. Pia ilisema marubani walishindwa kufungua mlango wa chumba chao na ule wa dharura juu ya ndege kutokana na msukumo mkubwa wa maji.

“Boti ya kitengo cha polisi cha majini ilifika saa 7:00 mchana eneo la tukio kwa sababu haikuwa Bandari ya Bukoba ilikuwa inafanya oparesheni zingine. Baada ya kufika walikuwa na changamoto ya ukosefu wa oksijeni na mafuta ya kutosha. Lakini  kabla ya kufika, mvuvi mmoja tayari alianza kutoa maiti zilizokuwa ndani ya ndege,” ilisema.

Kwa mujibu manusura wa ajali hiyo, ndege hiyo ilishuka salama lakini kabla haijakanyaga ardhi, ilibadili uelekeo kuelekea upande wa Ziwa Victoria.

Ripoti pia ilibainisha kuwa Uwanja wa Ndege wa Bukoba hauna mnara wa kuongozea ndege na kwamba mawasiliano yote hufanyika kwa kutumia mnara ulioko Mwanza, jambo ambalo Waziri alisema ni kawaida kuongozwa kwa mnara mwingine.

Pia ilisema rubani alijua anatua kwenye njia ya ndege na si kwenye maji na kwamba kuna uwezekano ndege ilisukumwa na upepo kwenda ziwani wakati akijaribu kutua.