Ripoti yaibua yaliyojificha Mwanga

20Apr 2019
Godfrey Mushi
MWANGA
Nipashe
Ripoti yaibua yaliyojificha Mwanga

RIPOTI ya matokeo ya utafiti kuhusu tathmini ya thamani ya fedha kwenye shughuli mbalimbali zinazofanywa kwa kutumia rasilimali za umma ili kuongeza utawala bora na uwajibikaji hasa kwenye sekta ya maji katika Wilaya ya Mwanga,-

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, mkoani Kilimanjaro, Thomas Apson (wa pili kulia), akikata utepe kuzindua ripoti ya utafiti wa mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma (PETS), katika sekta ya maji wilayani humo juzi. PICHA: GODFREY MUSHI

imeibua changamoto mbili kubwa ambazo ni ushiriki mdogo wa wananchi katika masuala ya maji na kukosekana kwa taarifa za mapato na matumizi.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la kiraia la Kinshai, linalotekeleza mradi wa ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma (PETS), Veronika Shao, amesema matokeo ya utafiti huo yanatokana na taarifa zilizokusanywa katika kata 10 za wilaya hiyo.

"Ripoti hii ni matokeo ya taarifa zilizokusanywa kutoka kata 10 za Wilaya ya Mwanga kuanzia mwezi Februari hadi Machi, mwaka huu. Kutokana na matokeo, changamoto mbalimbali zinazowakabili wanajamii kuhusu utumiaji, upatikanaji na usimamizi wa rasilimali za maji ziliibuliwa.

"Kuna kukosekana ama ushiriki mdogo wa jamii kuhusu masuala yahusuyo maji, kukosekana kwa taarifa za mapato na matumizi ya rasilimali za maji kwa baadhi ya vijiji na kata kwa sababu zilizo juu ya uwezo wa jamii kuzielewa, mwamko mdogo wa jamii katika uchangiaji gharama za maji na uhaba wa maji unaosabaishwa na mabadiliko ya tabia nchi na mgao wa maji usio mzuri," alisema.

Mradi huo unatekelezwa na Kinshai kwa ufadhili wa Shirika la The Foundation for Civil Society.

Aidha, wakati anasoma ripoti hiyo, Mhadhiri wa Kitivo cha Jamii na Maendeleo Vijijini wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi, Prosper Kimaro, alisema utafiti huo ulifanywa katika kata za Mgagao, Lembeni, Kileo, Jipe, Lang'ata, Shighatini, Kighare, Msangeni, Mwanga na Kirya.

Alisema kuwa idadi ya washiriki wote katika utafiti huo walikuwa 365 ambao ni wanaume na wanawake.

Awali, mtaalamu mwelekezi kuhusu dhana ya ufuatiliaji wa rasilimali za umma na mchakato wa bajeti, Gamaliel Mbalase, aliwaeleza wananchi hao wa Wilaya ya Mwanga kuwa ufuatiliaji huo unaongeza ushiriki wa wanajamii katika ufuatiliaji wa rasilimali fedha na mchakato wa bajeti na utekelezaji wake.

Zaidi alifafanua, kwamba PETS ni chombo kinachotumika katika kufuatilia au kuchunguza jinsi rasilimali za umma zinavyotumika kutoka kwenye ngazi zote za kiserikali na kisekta.

 

Kwa upande wake, Mhandisi wa Maji wa Sektretarieti ya Mkoa wa Kilimanjaro, Victor Nassari, alionya kuhusu vitendo vinavyoendelea vya uharibifu wa vyanzo vya maji na baadhi ya wananchi wa kata kadhaa kugoma kufungiwa dira za maji, wakidai maji hayo hawawezi kulipia kwa sababu ni vyanzo vya asili vilivyopo katika maeneo yao.

"Shida kubwa iliyopo Wilaya ya Mwanga, wananchi baadhi yenu hamtaki kufungiwa dira za maji na kwa hasira mnakwenda kuziharibu zile zilizofungwa tayari. Tutachukua hatua kwa atakayebainika kuanzia sasa," alisisitiza Nassari.

Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Thomas Apson, akizungumza na wadau hao na kamati za maji kutoka kata 10 za wilaya hiyo, alisema serikali itapambana kwa kila namna kuhakikisha katika miradi ya maji inayotekelezwa hakuna matumizi mabaya ya fedha wala ya madaraka.

"Tuna vyanzo vingi vya maji katika Kata ya Kileo na Shigatini, lakini hatujaweza kuvitumia ipasavyo. Tumesema katika miradi tuliyonayo hivi sasa tunahakikisha wananchi wanapata maji wakati wote, lakini mapato yake na miundombinu yake inafanana na thamani ya fedha ama zinazokusanywa na kamati za maji au gharama za ujenzi," alisema.

Habari Kubwa