RITA yasajili vyeti kuzaliwa 10,495

19Jul 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
RITA yasajili vyeti kuzaliwa 10,495

WAKALA wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) umevunja rekodi ya kusajili na kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wananchi 10,495 ndani ya siku 16 katika Maonyesho ya 45 ya Kimataifa ya Biashara (Sabasaba).

Akitoa taarifa hiyo kutoka katika banda la RITA viwanja vya Sabasaba, Kaimu Kabidhi Wasii Mkuu wa Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), Emmy Hudson, amesema kuwa wananchi wamekuwa na mwitikio mkubwa wa kufuatilia vyeti vya kuzaliwa kutokana na kujua umuhimu wa kuwa na cheti hicho ili kujipatia mahitaji muhimu katika jamii.

Hudson alisema mkoani Dar es Salaam wakati akizungumza na wananchi waliofika katika banda hilo kwa ajili ya kupata vyeti vya kuzaliwa siku ya kufungwa kwa maonyesho hayo.

Alisema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa RITA kuwafikia wananchi katika kila sehemu na kutoa huduma pamoja na kwenye maadhimisho na maonyesho mbalimbali kama hayo ili kuwarahisishia upatikanaji wake karibu na maeneo wanayoishi.

Alisema licha ya maonyesho hayo kumalizika, wataendelea kutoa huduma hiyo katika ofisi za RITA kama kawaida na wananchi wanatakiwa kuendelea kufika ili kupata vyeti kwa kuwa ni haki ya kila Mtanzania.

"Changamoto tuliyoipata Uwanja wa Sabasaba ni watu kuwa wengi, ambapo ikasababisha huduma hiyo kutolewa hadi saa moja usiku, ili kila aliyefika katika banda hili aweze kupata huduma kulingana na mahitaji yake," alisema Hudson.

Mmoja wa wananchi hao, Amina Abdallah, aliipongeza RITA kwa huduma hiyo na yeye kufanikiwa kupata cheti chake cha kuzaliwa kwa gharama nafuu na kwa haraka.

“Kwakweli wananchi tulikuwa wengi sana ambao tunahitaji huduma ya vyeti, lakini tulipokelewa vizuri na maofisa wa RITA waliokuwa wanatoa huduma na kutuhudumia kulingana na mahitaji yetu," alisema.

Joseph Mashaka alisema, hakuwahi kutegemea kupata cheti cha kuzaliwa kulingana na umri wake kutokana na baadhi ya wananchi mtaani kutoa taarifa za upotoshaji kuhusu ugumu wa kupata huduma hiyo, lakini baada ya kufika katika banda hilo alipewa maelekezo na kisha kuanza hatua za kupata cheti tofauti na alivyodhani hapo awali.

Mmoja wa viongozi waliotembelea banda hilo ni Meya wa Jiji la Ilala, Omary Kumbilamoto, ambaye aliupongeza wakala kwa kutoa huduma hiyo hadi muda wa usiku kwa lengo la kuhakikisha kila mwananchi anapata huduma ya cheti cha kuzaliwa.