Roma asimulia siku 3 za hofu, kihoro

11Apr 2017
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Roma asimulia siku 3 za hofu, kihoro

MSANII wa muziki wa kizazi kipya, Ibrahim Musa, maarufu kama Roma mkatoliki, amesimulia namna walivyotekwa, huku akionyesha majeraha kwenye mwili wake aliyoyapata kutokana na kuteswa kwa siku tatu mfululizo na watekaji wao.

Roma mkatoliki, akionyesha majereha aliyoyapata, mbele ya waandishi wa habari.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Roma alisimulia tukio zima tangu walivyotekwa mpaka kutupwa katika dimbwi la maji katika eneo la Ununio, kata ya Kunduchi jijiji Dar es Salaam.

Akisimulia tukio zima, Roma alisema Jumatano alifika katika studio yake iliyopo Masaki majira ya saa 11 jioni na kukuta wafanyakazi wake watatu wakiendelea na kazi.

"Lakini baada ya nusu saa waliingia watu wasiojulikana wakiwa na silaha za moto na kutuamuru tuingie kwenye gari lao," alisema. Alisema baada ya kuamriwa kuingia kwenye gari hiyo walifungwa miguu, mikono na midomo na kuambiwa wainame chini.

Alisema kutokana na kuwaogopa watu waliowateka walilazimika kuinama chini na hivyo kupelekwa mahali kusikojulikana. Roma alisema baada ya kupelekwa huko walianza kuteswa kwa kupigwa huku wakihojiwa masuala mbalimbali ambayo hakuwa tayari kuyataja hata hivyo.

Alisema baada ya mateso hayo ambayo yaliendelea kwa siku tatu mfulilizo, Ijumaa usiku walichukuliwa na kupelekwa tena kusikojulikana na kutupwa huko.

“Tukio lilitokea siku ya Jumatano ilikuwa jioni kuanzia saa kumi na moja kwenda saa kumi na mbili," alisema. "Nilikuwa nimeenda kwa ajili ya kufanya shughuli zangu, lakini nilipofika niliwakuta kina Moris, Bin Raden pamoja na Emma, (na) wakati naendelea na shughuli zangu muda wa nusu saa walifika watu ambao hatukuweza kuwafahamu. "Na mbaya zaidi walikuwa na silaha za moto na amri yao ya kwanza ilikuwa ingieni ndani ya gari.

“Baada ya kuingia ndani ya gari, nakumbuka wale watu walitufunga usoni na vitambaa na pingu na kutuamru tuainame chini na gari ikawasha kutoka maeneo ya studio na kuelekea maeneo ambayo sisi hatukupajua.

"Tulipelekwa mahali ambapo hatupajui na ndiko tulikokaa siku hizo zote mpaka Ijumaa usiku wa kuamkia Jumamosi.

“Katika siku zote hizo kuna mahojiano ambayo yalikuwa yanaendelea kati yetu sisi na hao watu, ambayo tumeyapeleka polisi kwa ajili ya upelelezi, lakini mahojiano yao yaliambatana na vipigo na kutupa majeraha.

"Kila mtu alipata majeraha na kila mtu alipigwa, tulipotolewa na kuwekwa kwenye gari ambayo siku hiyo tulifungwa mdomo na nyuma na miguu tukapelekwa huko tulikotupwa ambako hatukupajua na ilikuwa ni usiku sana na hatukujua ni wapi lakini ilikuwa ni kwenye dimbwi.

“Nilianza kujifungua mimi halafu nikawafungua na wenzangu na tulivyoangalia tukajikuta tuko salama, tukaanza kutembea na ulikuwa ni umbali mrefu sana na tukakutana na kibao kilichoandikwa Mahaba Beach; na ndipo tuligundua kuwa pale ilikuwa ni Ununio.

"Kwa sababu tulikuwa na hofu kila gari iliyokuwa ikipita tulikuwa tunaogopa... tunajificha inapotumulika.”

Roma alisema walifika nyumbani kwake Mbezi Beach usiku huo lakini bahati mbaya hawakukuta familia yake na kushtuka, jambo lililosababisha watafute njia nyingiene ya kuondoka hapo kwenda kutafuta msaada.

Alisema walitafuta usafiri na kuondoka hadi kwa 'bosi' wao ambako waliambiwa waende katika kituo cha polisi cha Osterbay ambacho tayari familia yake ilikuwa imeripoti tukio hilo. Alisema walifika na kueleza kilichotokea, ikiwa ni siku ya Jumamosi.

Akizungumzia usalama katika eneo lake la studio, Roma alisema ofisi yake hiyo imekuwapo katika eneo hilo kwa muda wa miaka 10 sasa na kumekuwapo na usalama wa kutosha kwa kuwa iko katika nyumba ya kiongozi mkubwa wa serikali, na pia imezungukwa na makazi ya viongozi wakubwa wa serikali.

Akizungumzia yasemwayo kwenye mitandao ya kijamaii kwamba wametumika kisiasa ili kujipatia fedha, Roma alisema maneno hayo si kweli.

Kwa upande wake Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Harison Mwakyembe, alisema atahakikisha uchunguzi wa tukio hilo unafanyika haraka ili kubaini kilichowakuta wasanii hao ikiwezekana kabla ya bajeti yake kusomwa bungeni.

Habari Kubwa