Royal Tour na fursa lukuki  uwekezaji mkoani Dodoma

16May 2022
Augusta Njoji
DODOMA
Nipashe
Royal Tour na fursa lukuki  uwekezaji mkoani Dodoma

KUANDALIWA kwa filamu ya Tanzania The Royal Tour kumelenga kutangaza vivutio vya utalii vilivyoko nchini.

 

Mbali na madhumuni hayo, filamu hiyo pia ni miongoni mwa fursa muhimu za Tanzania kujitangaza na kujiimarisha kiuchumi kupitia maeneo mbalimbali.

Pamoja na kwamba filamu hiyo imebeba maudhui ya utalii, ni njia moja wapo ya kuonyesha namna Tanzania ilivyobarikiwa kwa kuwa rasilimali ambazo zikitumika ipasavyo, zitavuta watalii na wawekezaji wengi kuwekeza nchini.

Tayari filamu hiyo imeshazinduliwa katika mikoa ya Arusha, Dar es Salaam, visiwani Zanzibar na jana ilikuwa ni zamu ya Mkoa wa Dodoma ambao umeizindua kwa kunadi fursa lukuki zilizoko maeneo mbalimbali mkoani hapa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka, akizungumzia uzinduzi wa filamu hiyo, anasema wameamua kufanya uzinduzi wa aina yake unaotangaza fursa zilizoko na wafanyabiashara kutoa ushuhuda namna Royal Tour itakavyosaidia kuwafungulia fursa zaidi za kujikwamua kiuchumi.

Mtaka anasema Dodoma ni eneo linalofaa kwa uwekezaji na ujenzi wa viwanda vikubwa kutokana na kuwapo kwa ardhi kubwa.

“Kwa Dodoma uzinduzi huu ni wa tofauti kwa sababu tunataka sekta binafsi izungumze manufaa na fursa za filamu hii zitakavyofungua milango ya uwekezaji na ufanyaji biashara.

“Dodoma ni Makao Makuu ya Nchi, tuna fursa ya utalii wa utamaduni wa makabila ya hapa, utalii wa miradi, utalii wa zabibu, utalii wa maliasili, kuna fursa ya kuwekeza viwanda lakini kujenga nyumba za kupangisha au kuuza.

"Hawa wageni watakaovutiwa na Tanzania, wengine wanaweza kutamani kumiliki nyumba Dodoma, tuna fursa nyingi zinahitaji uwekezaji ili Dodoma ifunguke kiuchumi na wananchi wetu vipato vyao vipae,” anasema.

Anatoa wito kwa Watanzania na wakazi wa Dodoma kuchangamkia fursa hiyo muhimu ambayo Rais Samia Suluhu Hassan ameonyesha njia na itakuwa na matunda kwa Taifa.

FURSA ZA KILIMO DODOMA

Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Fatma Mganga, anasema mkoa huo una fursa nyingi za kilimo na ufugaji nyuki na kutoa wito kwa wawekezaji kuchangamkia fursa hizo kwa kuwa tayari kuna mashamba makubwa ambayo yamepimwa, yana hati na yanafaa kuwekeza kwenye kilimo cha alizeti, mtama na zabibu.

“Kuna mashamba yapo Wilaya za Chamwino na Bahi, kilimo ni kitu kinachoweza kuleta fedha nyingi sana. Kwa mfano, Afrika Kusini unakuta mtu ana shamba kubwa, yaani kulitembelea ni kama unafanya safari ndiyo tuna fursa za mashamba ya aina hii Dodoma ambayo yanahitaji uwekezaji,” anasema.

Katibu Tawala huyo pia anasema zabibu ya Dodoma ni zao la kipekee kutokana na kuvunwa mara mbili kwa mwaka na kwamba hiyo ni fursa inayohitaji uwekezaji kwa wageni watakaochangamkia fursa za Tanzania The Royal Tour.

“Kwenye alizeti sisi ni miongoni mwa mikoa minne ya kimkakati ya kilimo cha alizeti, tunahitaji uwekezaji kuwa na mashamba makubwa ya kilimo hiki ambacho kina soko, kama mnavyojua mahitaji ya mafuta ya kula kwa mwaka ni makubwa na uzalishaji ulipo sasa haukidhi mahitaji, lakini ardhi yetu tuliyo nayo inafaa kwa kilimo hiki,” anasema.

Akizungumzia zao la mtama, Katibu Tawala huyo anasema ni zao ambalo kwa sasa lina soko na linahitaji wananchi na wawekezaji kulima kwa wingi kutokana na kupatikana kwa soko katika Shirika la Chakula Duniani (WFP).

Mchumi wa Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Francis Kaunda, anasema kuna mashamba makubwa 171 eneo la Zuzu ambayo yamewekewa miundombinu yote ikiwamo bwawa lisilokauka kwa ajili ya umwagiliaji.

"Hili eneo tunaita ‘urban farming’, kuna miundombinu yote muhimu na lipo katika barabara ya mzunguko (ring road) inayojengwa, ukubwa wa mashamba unaanzia mita za mraba 4,047 (ekari moja), mashamba haya yanahitaji watu waje kuwekeza na kila mita ya mraba inauzwa Sh. 3,000 na yanafaa kwa kilimo cha mboga, alizeti na zabibu,” anafafanua.

Anasema pia kuna fursa ya uwekezaji wa mashamba ya kufuga wanyamapori ambayo itawawezesha watu kutengeneza mbuga ya wanyama na kuongeza vivutio vya utalii ndani ya jiji hilo.

ENEO LA KUJENGA VIWANDA

Mchumi huyo anasema Jiji la Dodoma pia limetenga eneo Nala jijini hapa lenye ukubwa wa ekari 2,094 ambalo lina uwezo wa kuchukua viwanda vikubwa zaidi ya 100.

Anasema eneo hilo lina miundombinu yote huku akitolea mfano kiwanda cha mbolea asilia cha Itracom ambacho ujenzi wake upo kwa asilimia 80, kwamba kwa sasa kuwa ni miongoni mwa viwanda vikubwa vinavyofaa kujengwa kwenye eneo hilo.

"Tuna eneo la Mpunguzi wawekezaji wataweza kulima zao la zabibu na kuanzisha viwanda vingi vya wakulima wadogo wa zabibu,” mchumi huyo anafafanua.

Kuhusu usalama, mchumi huyo anasema jiji lina mpango wa kuimarisha usalama kwa kufunga kamera kwenye mitaa ili kuimarisha usalama wa wananchi na mali zao na kuvuta wawekezaji.

“Pamoja na kuita wawekezaji, hatujawasahau wafanyabiashara wetu wadogo, tunajua Royal Tour italeta wageni na watakuwa na mahitaji yao mbalimbali. Tumejenga soko la kisasa la Machinga, limegharimu Sh. bilioni 7.5, hili ni soko la kipekee, lina huduma zote pale na limejengwa kwa kuwashirikisha wanufaika, litakuwa na uwezo wa kuchukua wafanyabiashara wadogo zaidi ya 3,000,” anasema.

WAFANYABIASHARA WAFUNGUKARais wa Sauti ya Wanawake Wajasiriamali Tanzania, Maida Waziri, anasema filamu hiyo ambayo imechezwa na Rais Samia Suluhu Hassan, italitangaza Taifa na wafanyabiashara watanufaika kwa kiasi kikubwa na fursa hizo.

“Kuna manufaa makubwa ya Royal Tour yanakuja kwa private sector (sekta binafsi), kuna watu wamekuwa wakibeza juhudi  hizi za Rais Samia lakini sisi taasisi binafsi tumeanza kuona manufaa makubwa sana katika nyanja zote,” anasema.

Mfanyabiashara huyo anasema miongoni mwa manufaa ni miradi katika sekta za ujenzi na kilimo pamoja na kuongezeka ajira na watalii.

Habari Kubwa