RPC amshangaa dereva wa Lissu

14Sep 2017
Renatha Msungu
Nipashe
RPC amshangaa dereva wa Lissu

JESHI la Polisi mkoa wa  Dodoma limesema linashangazwa na kitendo cha dereva wa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (Chadema), Adam Bakari, kutoripoti polisi kutoa maelezo kuhusiana na tukio la kushambuliwa Lissu kwa risasi.

Kamanda wa mkoa huo, Gilles Muroto.

Kamanda wa mkoa huo, Gilles Muroto, alisema hayo jana katika mkutano na waandishi wa habari kuhusiana na vitu mbalimbali walivyokamata katika msako unaoendelea.

Alisema dereva huyo anahitajika kituoni kwa nia njema, ili kulisaidia Jeshi la Polisi kumbaini aliyefanya kitendo cha kinyama cha kumshambulia Mbunge huyo, lakini cha kushangaza
hadi leo anakwepa kwenda kituoni.

“Mimi nashangaa kwa nini hadi leo (jana) hajaripoti kituoni wakati Jeshi lina lengo zuri la kupata ushirikiano wakati zoezi la upelelezi likiendelea,” alisema Muroto.

Alisema wameweka ulinzi katika barabara zote za mkoani hapa kuhakikisha wanafanikisha upelelezi wa tukio hilo lililotokea Alhamisi.

Hata hivyo, wakati Kamanda Muroto anashangaa dereva wa Lissu kutoripoti Polisi, dereva huyo aliondoka na Lissu anayetibiwa katika Hospitali ya Aga Khan tangu Alhamisi usiku, baada ya Lissu kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma.

Katika hatua nyingine, Jeshi hilo linawashikilia raia watano wa China baada ya kupatikana na nyara za serikali kinyume cha sheria.

Kamanda Muroto alisema raia hao walikamatwa katika kiwanda cha kusaga kokoto cha kampuni ya Sands Industry Limited katika Kijiji cha Mpamantwa wilayani Bahi.

Raia hao walikamatwa kwa ushirikiano wa askari wa kikosi cha ujangili Kanda ya Manyoni ambapo walikutwa na magamba 652 ya kakakuona, kucha tano za kakakuona, kucha nne za simba na jino moja la simba.

Alisema uchunguzi unaendelea, ili kubaini mtandao wa majangili na wageni wanaoingia nchini kwa ajili ya kujihusisha na ujangili.

Kadhalika, alisema  msako unaoendelea maeneo mbalimbali na watuhumiwa 12 wamekamatwa kwa  makosa mbalimbali ya uvunjaji na wizi huku akiwataka wananchi wajitokeze kutambua vitu vyao vilivyoibwa.

Alisema jeshi hilo limekamata Flat screen 13, Sabufa 2, spika 5, deki moja, printa moja, king’amuzi kimoja, busta ya gari moja na bangi kete 12. Watuhumiwa watafikishwa mahakamani upelelezi ukikamilika.

Alisema kati ya watuhumiwa hao Dotto Kapenga (43), mkazi wa Chang'ombe alikamatwa na sare za Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) aina ya kombati suruali moja, sweta mbili, mikanda mitatu, kofia tano na buti pea moja. Pia alikutwa na koti la mvua na cheo cha luteni ussu.

Habari Kubwa