Rufaa ya Mbowe, Matiko kesho

05Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rufaa ya Mbowe, Matiko kesho

Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imetoa wito kwa  Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na Mbunge wa Tarime mjini, Esther Matiko, ikiwataka kufika mahakamani hapo kesho Jumatano Machi 6, 2019 kwa ajili ya usikilizwaji wa rufaa.

Habari zilizothibitishwa na Wakili wa wanasiasa hao, Peter Kibatala leo Jumanne Machi 05,2019, ni kwamba rufaa hiyo itasikilizwa kesho saa 3:00 na Jaji Sam Rumanyika.

Usikilizwaji wa rufaa hii umekuja siku nne tu tangu waliposhinda rufaa ya Mkurugenzi wa Mashtaka aliyekuwa akipinga uamuzi wa Mahakama Kuu kukubali kuendelea na usikilizwaji wa rufaa yao, licha ya kuiwekea pingamizi.

Hukumu hiyo ya Mahakama ya Rufani ilitolewa na Machi Mosi na jopo la majaji watatu waliosikiliza rufaa hiyo likiongozwa na Jaji Stella Mugasha, Dk Gerald Ndika na Mwanaisha Kwariko.

Katika hukumu hiyo iliyosomwa na Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani, Sylvester Kainda, mahakama hiyo ilitupilia mbali hoja za rufaa ya DPP ikisema kuwa hazina mashiko.

Habari Kubwa