Rufani Mbunge Chadema kutikisa mahakamani

20Feb 2017
Cynthia Mwilolezi
ARUSHA
Nipashe
Rufani Mbunge Chadema kutikisa mahakamani

MAJAJI watatu wa Mahakama ya Rufani, leo wanatarajiwa kusikiliza rufani ya aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole (Chadema), ya kupinga kutenguliwa ubunge wake, Juni 29, mwaka jana.

aliyekuwa Mbunge wa Longido, Onesmo Ole Nangole.

Kesi hiyo itasikilizwa na Jaji Bernard Luanda, atakayekuwa Mwenyekiti wa Jopo la Majaji Stella Mugasha na Kipenka Mussa.
Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, ilitengua matokeo ya ubunge wa Nangole kutokana na dosari kadhaa.

Moja ya dosari hizo ni pamoja na kujazwa kwa matokeo ya ubunge kwa kutumia fomu namba 21c za kujaza matokeo ya udiwani na kujaza matokeo ya ubunge, badala ya kutumia fomu namba 21b.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Bukoba, Silvangilwa Mwangesi, aliyekuwa akisikiliza kesi hiyo, alisema katika uchaguzi huo, kulikuwa na dosari nyingi ila dosari kubwa ya ujazaji matokeo ya ubunge katika fomu za udiwani na huku baadhi zikiwa zimefutwafutwa, ilikuwa ni kosa kisheria na hivyo akatengua matokeo ya uchaguzi wa ubunge na kuamuru urudiwe.

Alisema baada ya kutokea dosari hizo, ilitakiwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Longido, Felix Kimario, kutoa maelezo mahakamani juu ya uamuzi wa kutumia fomu hizo, lakini alipofika hakutolea maamuzi, hivyo mahakama iliona kasoro hiyo ilifanywa kwa makusudi.

Pia mahakama hiyo ilithibitisha kulikuwa na fujo katika uchaguzi huo ambazo zilianzishwa na Nangole katika chumba cha majumuisho ya kura na hivyo ikawa hoja nyingine ya kutengua ubunge wake.

Katika hukumu hiyo, Jaji Mwangesi aliamuru taarifa za kutenguliwa ubunge huo zipelekwe haraka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na kwa Msimamizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Longido, ili uchaguzi mwingine uandaliwe.

Aliutaka upande wa Chadema kulipa gharama za kesi hizo.

Hata hivyo, mahakama ilitupilia mbali madai ya kuwapo kwa lugha za kashfa kwa Dk. Steven Kiruswa, aliyekuwa mgombea ubunge kupitia CCM na suala la Wakenya kupiga kura na kutumika kwa magari ya Chadema kubeba masanduku ya kura.

Katika kesi hiyo, upande wa mdai Dk. Kiruswa, alitetewa na Dk. Masumbuko Lamwai, akisaidiana na Edmund Ngemela na Daud Haraka, huku mdaiwa wa kwanza Nangole, akitetewa na Wakili Method Kimomogolo aliyekuwa akisaidiana na John Materu.

Upande wa mdaiwa wa pili ambao ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali, uliwakilishwa na Daud Akway, akisaidiana na Neema Nyanda.

Hata hivyo, Nangole hakuridhika na hukumu hiyo na hivyo aliamua kukata rufani Mahakama ya Rufani.

Habari Kubwa