Rufiji wamlilia JPM malipo ya korosho

15Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
Rufiji
Nipashe
Rufiji wamlilia JPM malipo ya korosho

WAKULIMA wa korosho kata za Muhoro na Chumbi, wilayani Rufiji mkoani Pwani, wamelalamika korosho zao tani 180 zimeendelea kubaki katika maghala ya vyama vya ushirika vya msingi, hivyo kusababisha malipo yao kukwama kwa miezi mitatu sasa.

Wakizungumza na waandishi wa habari jana, wakulima hao walilalamika kwamba kati ya tani 260 za korosho zilizotunzwa katika maghala ya msingi, ni tani 80 ndizo zilizopelekwa katika ghala kuu lililopo Kibiti, ambako ukaguzi hufanywa kwa ajili ya maandalizi ya malipo.

Akizungumza kwa niaba ya wakulima wenzake mwenyekiti wa wakulima wa Kata ya Muhoro, Rajabu Mikindo, alisema tangu wakusanye korosho na kuzipeleka katika maghala ya vyama hivyo, ni zaidi ya miezi mitatu sasa.

“Lakini bado hazijaondoka na tutajikuta tunaishi maisha magumu kwa kukosa pesa za kujikimu. Tunaamini Rais wetu (John Magufuli) ni msikivu sana, anajua taabu tunazopata wakulima, tunaomba atuangalie wakulima wa Muhoro kwa kuzinusuru korosho zetu zifike ghala kuu na kufanyiwa malipo ili tujikimu kimaisha,” alisema Mikindo.

Mkulima mwingine wa kata hiyo, Sophia Kumchaya, aliiomba serikali kuziondosha korosho hizo kwa madai kwamba ziko katika maghala ambayo si salama kwa uhifadhi.

Aliongeza kuwa zikipelekwa katika ghala kuu lililochaguliwa zitafanyiwa malipo ili waweze kujikimu na pia kuandaa mashamba yao kwa msimu ujao.

Kwa upande wake, Bakari Chopo, alisema alipeleka korosho zake katika maghala ya vyama vya msingi zikiwa nzuri, hivyo hatakubali kurudishiwa zitakapoharibika kutokana na kukaa muda mrefu katika maghala yasiyo na viwango.

Katika Kata ya Chumbi, Hassan Mtupa, alisema tangu wakusanye tani 130 za korosho katika ghala la msingi, ni tani 30 tu ndizo zimechukuliwa na kupelekwa ghala kuu huku nyingine wakiwa hawajui hatima yake.

"Tunapata wasiwasi na kauli ya Waziri wa Kilimo kutangaza mwisho wa kupeleka korosho katika maghala makuu yaliyoteuliwa kwamba ni Januari 30 wakati sisi zetu hazijafika, tutapata hasara tunaomba serikali na Rais aingilie kati ili zifikishwe huko zifanyiwe malipo,” alisema Mtupa.

Wakulima hao wamefikia hatua hiyo baada ya kuona uharibifu unaoweza kusababishwa na mvua zinazotarajia kuanza kunyesha kabla ya korosho zao kuondolewa na kupelekwa ghala kuu kwa ajili ya kufanyiwa malipo.

Habari Kubwa