Rugemalira apanda kizimbani kesi uhujumu uchumi

17Jun 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Rugemalira apanda kizimbani kesi uhujumu uchumi

MKURUGENZI Mtendaji wa Kampuni ya VIP Engineering, James Rugemarila na Mwanasheria wa Independent Power Tanzania Limited (IPTL), Joseph Makandege, wamepanda kizimbani kuendelea na kesi ya uhujumu uchumi inayowakabili baada ya mshtakiwa mwenzao, Habinder Sethi, kuachiwa huru.

Mfanyabiashara James Rugemalira akiwa chini ya ulinzi wa askari Magereza, baada ya kesi inayomkabili ya uhujumu uchumi, kutajwa kwenda kuisikiliza Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar es Salaam jana. PICHA: JUMANNE JUMA

Washtakiwa hao wamefika leo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wakati kesi inayowakabili ilipotajwa mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi.

Wakili wa Serikali Mwandamizi, Wankyo Simon, amedai mahakamani kwamba kesi ilikuja kwa ajili ya kutajwa na upelelezi haujakamilika, hivyo aliomba tarehe nyingine ya kutajwa.

Mahakama ilikubali kuahirisha kesi hiyo hadi Julai Mosi kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa walirudi rumande.

Baada ya Sethi kuachiwa huru kwa masharti, Rugemalira na Makandage walibaki kwenye kesi hiyo.

Rugemarila, ambaye ni mmiliki mwenza wa zamani wa IPTL anadaiwa kutenda makosa hayo mkoani Dar es Salaam na nchi za Afrika Kusini, Kenya na India.

Anakabiliwa na mashtaka 12 yakiwamo ya utakatishaji fedha, miongoni mwa mashtaka hayo yapo ya kula njama, kujihusisha mtandao wa uhalifu, kughushi na kutoa nyaraka za kughushi na kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, kutakatisha fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.60 na Sh. 309,461,300,158.27.
                                                            
Inadaiwa kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 jinini Dar es Salaam, walikula njama katika nchi za Afrika Kusini, Kenya na India ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Mwanasheria Makandege, anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuisababishia serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000.

Makandege aliondoa maombi yake ya kufanya mazungumzo na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Mei 6, mwaka huu, na Rugemarila hakuwahi kuandika barua kuomba kukiri makosa yake.

Habari Kubwa