Rugemalira asimulia siri kutonyoa nywele miaka 4

21Sep 2021
Donald Lukele
DAR ES SALAAM
Nipashe
Rugemalira asimulia siri kutonyoa nywele miaka 4

MFANYABIASHARA James Rugemalira juzi alieleza Kanisa Katoliki, Parokia ya Makongo Juu, Dar es Salaam kuwa hajanyoa ndevu wala nywele za kichwani kwa miaka minne na miezi mitatu alipokuwa chini ya mamlaka za dola.

Akizungumza katika ibada ya shukrani katika kanisa hilo alililojenga kwa kushirikiana na waumini wenzake, alisema “Hizi nywele sijawahi kuzinyoa tangu nilivyoingia gerezani, baby (mke wangu) alitaka kuninyoa ila nilivyokuja kushukuru nilimwomba Paroko amwambie asininyoe, nimeziacha hivi kwasababu, hivi nilivyo kunaongea, sina la kuongea zaidi.”

Rugemalira ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa kampuni ya IPTL, alisema lengo la kwenda kanisani humo ni kumshukuru Mungu kwa kumtetea kauli iliyoungwa mkono na Mkewe Benedicta ambaye alisema ni maombi kama ya Paulo na Sila yamemwezesha mpendwa wao kutoka gezerani.

Aidha, aliwashukuru waumini kwa sala na kumtembelea gerezani kwa kipindi chote alichokuwa gerezani.

“Kiukweli niwapongeze kwa hatua kubwa iliyofanyika, kuwa na Hekalu la Bwana la aina hii yaani naona maajabu kila nikiangalia huku na kule, hongereni sana,” alisema Rugemalira.

Akizungumza baada ya mfanyabiashara huyo kushukuru, Paroko wa Jimbo hilo Joseph Massenge, alimpongeza kwa msimamo na kwamba hakika ushujaa wake ni mfano wa kuigwa kwa waumini hao.

“Huu ndiyo ukristo wa kweli mnatakiwa kuiga mfano wa maisha haya mjitoe sadaka kwa kusimamia ukweli kama unahisi unasimamia ukweli,” alisema paroko.

Aidha, aliisifu imani ya Rugemarila baada ya kitendo cha kuchagua kufika kanisani hapo baada ya kutoka mahabusu kwa takribani miaka minne ambayo ni imani kubwa na ya mfano, huku akimsihi kusamehe yote na kuanza maisha mapya yasiyo na kinyongo wala kulipiza kisasi kwani huo ndio ukristo wa kweli.

Rugemarila aliachiwa Septemba 16, mwaka huu, baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya Nole chini ya kifungu cha 91(1) kuwa hana nia ya kuendelea na mashtaka yanayomkabili mtuhumiwa huyo.

Rugemalira alikuwa akikabiliwa na mashtaka 12 ikiwamo ya utakatishaji wa fedha na kusababisaha hasara ya dola za Marekani 22,198,544.6 na Sh. 309,461,300,158.27.