Rugemalira: Sina kinyongo na mtu

17Sep 2021
WAANDISHI WETU
Dar es Salaam
Nipashe
Rugemalira: Sina kinyongo na mtu

VILIO vya furaha vilitawala jana kwenye viunga vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Dar es Salaam kutoka kwa wanafamilia na ndugu baada ya kuachiwa huru kwa mfanyabiashara James Rugemalira aliyekuwa anakabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi.

Hatua hiyo ilifikiwa jana baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) kuwasilisha hati ya Nole chini ya kifungu cha 91(1) kwamba hana nia ya kuendelea na mshtakiwa Rugemalira.

Kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa jana mbele ya Hakimu Mkazi Huruma Shaidi. Mshtakiwa huyo alikuwa mahabusu gerezani kwa takriban miaka minne na miezi mitatu tangu Juni 19, 2017, alipopandishwa kizimbani kusomewa mashtaka dhidi yake.

Mapema jana, Wakili wa Serikali, Grace Mwanga, alidai mahakamani huko kwamba kesi hiyo ilipangwa kwa ajili ya kutajwa.

Hata hivyo, alidai DPP ametoa hati ya Nole chini ya kifungu cha 91(1) cha Mwenendo wa Makosa ya Jinai kwamba hana nia ya kuendelea na kesi hiyo dhidi ya Rugemalira.

"DPP hana nia ya kuendelea na kesi hii dhidi ya Rugemalira, tunaiomba mahakama imwachie," alidai Wakili Mwanga.

Hakimu Shaidi alisema kwa kuwa Jamhuri hawana nia ya kuendelea na kesi hiyo, mahakama inamwachia huru chini ya Kifungu cha 91(1).

Mbali na Rugemalira, mshtakiwa mwingine katika kesi hiyo ni Joseph Mwakandege ambaye kesi yake itatajwa Septemba 23, mwaka huu.

Awali, Rugemalira aliwasilisha hoja kuomba kuondolewa na DPP katika kesi ya uhujumu uchumi.

Alidai mahakamani kuwa aliandika barua kwa Kamishna wa TRA kupitia mjumbe wa Taasisi ya Kuzuia na Kupamba na Rushwa (TAKUKURU) aliyetembelea gerezani akielezea jinsi Benki ya Standard Chartered Hong Kong inavyokwepa kodi na kudai kuwa wanaostahili kujumuishwa kwenye kesi ni benki hiyo na sio yeye.

Pia alidai aliandika notisi kwa taasisi tisa ikiwamo Usalama wa Taifa (TISS) akitaka DPP awasilishe hati ya kuachiwa kwake na asipofanya hivyo, yeye atawasilisha hoja ya kuiomba mahakama imwondoe katika kesi hiyo.

Katika kesi ya msingi ya uhujumu uchumi namba 27/2017, Makandege  anakabiliwa na mashtaka matano likiwamo la kuisababishia  serikali hasara ya Dola za Marekani 980,000, pia yapo ya utakatishaji wa fedha.

Mshtakiwa huyo alisomewa mashtaka hayo Desemba 20, 2019 baada ya kuunganishwa na washtakiwa Mkurugenzi wa Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL, HerbinderSeth na Rugemalira katika kesi hiyo ya uhujumu uchumi.

Makandege anadaiwa kuwa, kati ya Oktoba 18, 2011 na Machi 19, 2014 katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, Kenya, Afrika Kusini na India, akiwa na wenzake walikula njama ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Katika kesi hiyo, Rugemalira alikuwa anakabiliwa na mashtaka 12, likiwamo la utakatishaji fedha na kusababisha hasara ya Dola za Marekani 22,198,544.6 na Sh. 309,461,300,158.27 (Sh. bilioni 309.5).

'SINA KINYONGO NA MTU'

Baada ya kuachiwa huru, Rugemalira aliongozana na baadhi ya ndugu na jamaa zake hadi Kanisa Katoliki Makongo Juu Parokia ya Bikra Maria Mama wa Rozari Takatifu kulikofanyika ibada ya shukrani ambalo ni muumini wake.

Wakati wa ibada hiyo, Paroko wa Kanisa hilo, Joseph Masenge, alimtaka Rugemalira kusamehe, Rugemalira akijibu kuwa 'sina kinyongo na mtu, nimewasamehe wote'.

Baada ya kumalizika kwa ibada hiyo ya shukrani, Rugemalira alitembezwa kuangalia mandhari ya nje ya kanisa hilo zikiwamo nyumba za watumishi wake, akieleza kufurahishwa na ujenzi uliofanyika.

Nipashe ilizuru nyumbani kwa Rugemalira kwa nia ya kuzungumza na mfanyabiashara huyo, lakini walinzi walizuia kwa maelezo kwamba maagizo waliyopewa ni kuhakikisha hakuna mtu anayeruhusiwa kuingia ndani ya nyumba hiyo kwa jana, vinginevyo awe mwanafamilia.

KAULI YA LHRC

Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, akizungumzia kuachiwa huru kwa mfanyabiashara huyo, alisema kuna mchanganyiko wa furaha na huzuni katika tukio hilo, akifafanua kwamba furaha iko kwenye kuachiwa huru baada ya kukaa gerezani kwa miaka mingi na huzuni iko katika kusota miaka mingi gerezani bila dhamana na sasa DPP anasema hana mpango wa kuendelea na kesi.

"Kwa miaka mingi amesota, halafu DPP anasema hana sababu ya kuendelea na kesi. Kwa nini asingeona hivyo mwezi wa kwanza au miezi sita ya mwanzo?" Alihoji.

Kwa mujibu wa Henga, sheria ya jinai ina dosari kwa kuwa mtuhumiwa anasota kwa muda mrefu kwa kusingizio cha upelelezi haujakamilika, hali inayomfanya kuwa kama mfungwa kwa miaka mingi bila kosa lolote.

Alinyoshea kidole sheria ya kumlinda DPP na wapelelezi kwa kuwa aliyetendewa hayo hawezi kushtaki kudai fidia kwa muda na rasilimali alizopoteza.

*Imeandaliwa na Hellen Mwango, Romana Mallya na Salome Kitomari.