Rungwe sasa atoa mpya marudio uchaguzi Z'bar

12Jan 2017
Rahma Suleiman
Nipashe
Rungwe sasa atoa mpya marudio uchaguzi Z'bar

MWEYEKITI wa Chama Cha Ukombozi wa Umma (Chauma), Hashim Rungwe, amesema uchaguzi wa marudio wa mwaka jana visiwani Zanzibar ni jipu lililoleta mdororo wa kiuchumi nchini.

Rungwe ambaye aliwania nafasi ya Urais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, aliyasema hayo jana katika mkutano wa hadhara wa uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo wa Jimbo la Dimani; kwenye Viwanja vya Maungani, nje kidogo ya mji wa Zanzibar.

Alisema uchaguzi huo uliofanyika Machi 20, mwaka jana baada ya uchaguzi mkuu kufutwa na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), umesababisha baadhi ya nchi kusitisha misaada yake na kupelekea wananchi kuwa na hali ngumu kimaisha.

Kutokana na kususwa huko, Rungwe alisema maisha ya Watanzania yamekuwa duni na fedha haionekana kutokana na nchi kupoteza karibu asilimia 60 ya fedha zilizokuwa zinahitajika kwa ajili ya bajeti ya mwaka huu wa fedha.

Aidha, Rungwe alidai serikali zilizopo madarakani - Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) - zimepoteza haiba kwa kuwa wananchi wanashindwa kuwaamini viongozi wa serikali hizo.

“Kama mmeshindwa, ondokeni madarakani kuliko kuwaonea wananchi. Maisha yamekuwa magumu, wananchi wanalalamika fedha haionekani na wanalia njaa," alisema Rungwe.

Aliongeza kuwa nchi ina njaa kali na vijana wengi hawana ajira huku serikali ikiwa imepandisha kodi karibu kila sehemu wakati maisha ya wananchi ni duni.

Aidha, Rungwe alisema uchaguzi mdogo wa jimbo hilo na kata 22 nchini utakaofanyika Januari 22, ni fursa kwa vyama vya siasa kueleza dukuduku lao kwa kuwa tangu kumalizika kwa uchaguzi mkuu uliopita, vyama vimezuiliwa kufanya mikutano ya hadhara.

Aliwaomba wananchi wa Jimbo la Dimani kumchagua mgombea ubunge wa jimbo hilo kutoka chama chake ili kuwasaidia kukabiliana na njaa na kuwaletea maendeleo.

Alisema chama hicho kitahakikisha kinakiondoa Chama Cha Mapinduzi kwa njia za demokrasia katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 kwa kuwa wananchi hawana imani na CCM.

Akizungumza katika mkutano huo, mgombea ubunge kupitia chama hicho, Abdallah Kombo Abdallah, aliahidi kupeleka maendeleo makubwa jimboni humo ikiwa wananchi watampa ridhaa ya kuwa mbunge wao.

“Nitahakikisha huduma bora zinapatikana kwa kila mwananchi wa jimbo hili zikiwamo za afya, elimu, babaraba na maji safi na salama," alisema Kombo.

Uchaguzi wa Jimbo la Dimani unafanyika kufuatia kifo cha Hafidh Ali Tahir (CCM), aliyefariki dunia akiwa katika vikao vya Bunge mjini Dodoma, mwishoni mwa mwaka jana.

Habari Kubwa