Rushwa ya ngono yamchefua Samia

08Jan 2017
Mary Geofrey
Nipashe Jumapili
Rushwa ya ngono yamchefua Samia

MAKAMU wa Rais, Samia Suluhu Hassan, amekemea kuendelea kushamiri kwa unyanyasaji wa kijinsia na kusisitiza mapambano zaidi dhidi ya vitendo hivyo vikiwamo rushwa ya ngono na wanawake kunyimwa umiliki wa mali.

Kadhalika amesema serikali itahakikisha wanawake na watoto wanapatiwa haki zao kwa uhuru bila ubaguzi wala vitendo vya ukatili wa kijinsia.

Samia aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akifungua mkutano wa nane wa Chama cha Majaji Wanawake Tanzania (TAWJA), uliojumuisha zaidi ya majaji na mahakimu 200 kutoka mikoa mbalimbali nchini.

Alisema ni jambo la kuvunja moyo kuona katika karne ya 21 rushwa ya ngono inaendelea na kusababisha wanawake wengi kujiengua katika nafasi zao.

“Matarajio na ndoto za wanawake zimekuwa zikikatishwa na watu wachache ambao ni hatarishi, hivyo tunahitaji kufanya kazi kuhakikisha tunawasaidia kwa hali na mali kwa sababu waathirika hao wanaweza kuwa mama yako, dada, mke na binti yako,’’ alisema.

Alisema kuondoa vikwazo vya kisheria kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia ni miongoni mwa maeneo makubwa sita katika kupunguza pengo kubwa la kiuchumi nchini.

Aidha, aliwataka majaji na mahakimu kutoa hukumu kwa wakati katika kesi watakazopewa ikiwa ni pamoja na kufuata maadili na kanuni zilizowekwa na kuwataka kutoa elimu ya haki za binadamu na ujuzi bure kwa maofisa wa mahakama, watunga sera na waathirika wa ukatili wa kijinsia.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Mohamed Chande Othman, alisema asilimia 44 ya majaji walioko katika mahakama ni wanawake huku mahakama kuu pekee ikiwa na asilimia 47.9 ya majaji wanawake.

Pia alisema Bunge lina asilimia 46.6 ya wanawake wakati katika nchi za jirani, ikiwamo Kenya, wakiwa na idadi ndogo ya majaji wanawake ambayo ni asilimia 3.3.

Alisema wasajili wa mahakama waliopo, asilimia 34 ni wanawake na kwamba nafasi ya uongozi hususan kwa mahakimu wafawidhi wa mahakama za mwanzo na kati imeongezeka.

Mwenyekiti wa TAWJA, Jaji Imani Aboud, alisema miongoni mwa changamoto zinazowakabili ni pamoja na rushwa ya ngono ambayo licha ya mwanamke kuwa na haki ya kupata kazi, huombwa rushwa hiyo ili kumrahisishia upatikanaji wake.

Alisema tatizo hilo limekuwa kansa ya kimya kimya ambayo inalitafuna taifa kuanzia kazi ya makazini hadi kuiteketeza familia.

Habari Kubwa