RUWASA kumaliza kero ya maji Kata ya Rutamba

25Sep 2020
Na Mwandishi Wetu
Nipashe
RUWASA kumaliza kero ya maji Kata ya Rutamba

Serikali kupitia Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) inatekeleza mradi wa maboresho wa Mradi wa Maji wa Rutamba kwenye Halmashauri ya Mtama katika mkoa wa Lindi kwa lengo la kumaliza changamoto ya upatikanaji wa majisafi na salama kwa wakazi wa kijiji hicho.

Wataalam kutoka Wizara ya Maji wakikagua Mradi wa Maji wa Ng’apa katika Mkoa wa Lindi.

Meneja wa RUWASA mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa amesema mradi huo ulianza Aprili, 2020 na utakamilika ifikapo Novemba, 2020 umelenga kuongezea uwezo mradi uliopo kwa kutoa huduma kwa vijiji 4 baadala ya viwili kama ilivyokuwa hapo awali, na unatekelezwa kupitia mpango wa PfR (Payment for Results) kwa thamani ya Sh. milioni 340 kwa kutumia wataalam wa ndani.

Amesema mradi huo utamaliza changamoto ya upatikanaji wa maji iliyotokana na uchakavu wa miundombinu ya zamani na kushindwa kukidhi mahitaji baada ya ongezeko la wananchi hali iliyowalazimu kuchukua hatua ya haraka kutatua kero hiyo.

Timu ya Wataalam ya Wizara ya Maji ikiwa na kikao na Katibu Tawala wa Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge.

Akizungumza mbele ya wataalam kutoka Wizara ya Maji, Mwenyekiti wa Kamati ya Watumia Maji inayosimamia mradi huo, Ahmadi Mtambo amesema mradi huo umetumia fedha kidogo na kuzingatia ubora. Akitoa shukrani kwa Serikali kwa kusikia kilio cha wananchi na kusisitiza kamati kuusimamia vizuri na kuutunza kama shukrani yao kwa Serikali uweze kutoa huduma kwa muda mrefu.

Mhandisi Lubasa amesema mpaka sasa RUWASA inaendelea na utekelezaji wa miradi 37 inayotarajiwa kukamilika Novemba, 2020 itakayonufaisha wananchi 170,000. Akisisitiza kuwa mpango uliopo ni kutekeleza jumla ya miradi 55 kwa mwaka wa fedha 2020/21 ambapo kati ya hiyo 25 itakuwa chini ya mpango wa PbR (Payment by Results).

Meneja wa RUWASA Mkoa wa Lindi, Mhandisi Muhibu Lubasa akitoa maelezo kuhusu Chanzo cha Maji cha Chitachita kinachotumika na Mradi wa Maji wa Rutamba.
Mkurugenzi wa Huduma za Ubora wa Maji, Philipo Chandy na Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Lindi (LUWASA), Mhandisi Soud Othman pamoja na Wataalam wa Wizara ya Maji kwenye eneo la mradi wa mabwawa ya majitaka, mkoani Lindi.

Kukamilika kwa miradi hiyo kutaongeza huduma ya upatikanaji wa majisafi na salama Lindi vijijini kufikia asilimia 74, ambapo kwa sasa ni asilimia 61.

Aidha, Mradi wa Maji wa Nandambi wenye thamani ya Sh. Milioni 825 unatarajia kukamilika ndani ya siku 21 na kutoa huduma kwa wananchi 4,320 wa vijiji vya Nandambi na Mtutu, katika Wilaya Lindi.

Hatua hiyo imekuja mara baada ya changamoto ya kuchelewa kwa mabomba kutatuliwa na tayari mabomba hayo yamefika kwenye eneo la mradi na kazi ya kuyalaza inatarajiwa kuanza mara moja.

Mhandisi Joshua Lawrence akikagua ubora wa tenki la Mradi wa Maji wa Nandambi katika Wilaya ya Lindi.

 

Habari Kubwa