Saa 6 za jasho mawaziri wa Magufuli

27Feb 2016
Mary Geofrey
Dar
Nipashe
Saa 6 za jasho mawaziri wa Magufuli

Mawaziri wanne na Naibu Waziri mmoja walioshindwa kujaza na kuwasilisha fomu za tamko la rasilimali, maslahi na madeni pamoja na ahadi ya uadilifu tangu wateuliwe kushika nyadhifa zao mwishoni mwa mwaka jana, jana walikuwa na saa saba za jasho.

Rais Dk. John Magufuli.

Viongozi hao walioibuliwa juzi katika sekta maalumu Ikulu walikuwa na wakati mgumu huo, baada ya Rais John Magufuli kuwataka wawe wametimiza matakwa hayo ya kisheria kwa kwa Secretarieti ya Maadili ya watumishi wa Umma ifikapo jioni.

Aidha, Rais Magufuli aliagiza kuwa Mawaziri na Manaibu Waziri, watakaoshindwa kurudisha fomu hizo hadi jana saa 12:00 jioni tangu taarifa hiyo ilipotolewa saa 5:12 asubuhi, watakuwa wamejifukuzisha kazi.

Agizo hilo la Rais lilitolewa jana na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, wakati akizungumza na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

Majaliwa alisema, Rais Magufuli pia aliagiza majina yao yasomwe hadharani.

Mawaziri hao walitajwa na Majaliwa kuwa ni Waziri wa Mambo ya Ndani, Charles Kitwanga, ambaye hajarudisha fomu zote na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Mazingira na Muungano, Januari Makamba, ambaye hajarudisha fomu hata moja.

Majaliwa aliwataja Mawaziri wengine ambao hawakuwa wamejaza fomu moja kuwa ni Waziri wa Mambo ya Nje, Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Kikanda na Kimataifa, Balozi Augustine Mahiga, ambaye hajarudisha fomu ya ahadi ya uadilifu.

Mwingine ni mwanake pekee Waziri wa Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Profesa Joyce Ndalichako, ambaye hajarudisha fomu ya tamko la mali zake.

Majaliwa alimtaja pia Naibu Waziri wa Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Luhaga Mpina, kuwa hajarudisha fomu ya tamko na ahadi ya uadilifu.

“Rais Magufuli, ameelekeza Mawaziri hawa na Naibu Waziri wawe wameshajaza na kurudisha fomu hizo hadi ifikapo saa 12:00 jioni katika Sekretarieti ya Maadili jijini hapa na yeyote atakayekiuka agizo hili atakuwa amejiondoa mwenyewe kwenye nafasi yake ya uwaziri au unaibu waziri,” alisema Majaliwa.

“Rais pia ameagiza majina yao yasomwe ili popote walipo warudi na kujaza fomu hizo na kuzirudisha mara moja na ofisi yangu itasimamia kwa ukaribu ili kuhakikisha fomu hizo zinarudishwa leo kabla ya saa 12 jioni.”

Akizungumzia wale ambao wako mikoani au nje ya nchi, Majaliwa alisema Mawaziri au Manaibu waliosafiri kwenda nje ya nchi ruhusa yao itakuwa imetolewa na Rais hivyo itakuwa inafahamika.

Alisema hivyo hivyo kwa Mawaziri na Manaibu watakaokuwa nje ya mkoa wa Dar es Salaam, ruhusa zao zitakuwa zimetolewa na Waziri Mkuu, hivyo itaeleweka kwamba wako nje ya Mkoa kiofisi.

“Kwa takwimu za Mawaziri wangapi au Manaibu walioko nje ya mkoa kwa ruhusa yangu kwa sasa sina takwimu sahihi, ila kwa wale ambao hawawezi kufika jijini hapa kwa sababu wako mikoa ya mbali na ruhusa yao inafahamika, sababu hiyo ni ya msingi.

"Ila kwa walioko hapa au mikoa ya karibu wafanye hivyo.”

Kuhusu utaratibu wa kujaza fomu hizo kupitia sekretarieti ya maadili wa viongozi wa umma, alisema ofisi hiyo ina jukumu la kupokea taarifa za mali na kiapo cha uadilifu, kuchunguza malalamiko ya watumishi, kufanya utafiti na kutoa elimu na kusimamia utekelezji wa ahadi za maadili ya viongozi hao.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 9 cha sheria ya maadili kwa viongozi wa umma ya mwaka 1995 sura ya 398 viongozi wote waliotajwa katika kifungu cha nne wanatakiwa kujaza fomu hizo kila mwaka,” alisema.

Alisema fomu hiyo hutolewa kila mwaka na kwamba utaratibu huo ulianza mwaka jana hivyo watumishi wanaoshindwa kurudisha fomu hizo wanatakiwa kutoa maelezo na kama maelezo hayo hayatakuwa na tija watawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

“Mawaziri na Manaibu wamekuwa wanaendelea na zoezi hilo lakini wengine wamesharudisha na wengine ambao jana (juzi), walitajwa na Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji Salome Kaganda, kuwa hawajarudisha fomu hizo, Rais kaagiza leo wahakikishe wamerudisha.”

Jaji Kaganda aliwataja mawaziri na manaibu mawaziri ambao hawajarudisha fomu hizo juzi akiwa kwenye semina ya siku moja kuhusu sheria ya maadili, mgongano wa maslahi, mwongozo wa maadili ya viongozi wa umma na utekelezaji wa ahadi ya uadilifu.

Jaji Kaganda alisema Mawaziri ambao walikuwa hawajarejesha ni wanne na Manaibu Waziri ambao hawakurejesha hadi juzi ni watatu.

Nipashe ilifanya jitihada za kuwapata mawaziri hao ili kujua sababu za kushindwa kuwasilisha matamko hayo, lakini simu zao ziliita bila kupokelewa.

Habari Kubwa