Saa 96 za Waziri Mkuu na msako wezi nondo tani tano

20Jul 2019
Godfrey Mushi
MOSHI
Nipashe
Saa 96 za Waziri Mkuu na msako wezi nondo tani tano

WIZI wa nondo tani tano zilizonunuliwa kwa fedha za umma kwa ajili ya mradi mkubwa wa ujenzi wa stendi ya mabasi ya Ngangamfuni, Manispaa ya Moshi, umemshtua Waziri Mkuu Kasim Majaliwa, na kuagiza waliotekeleza hujuma hiyo wakamatwe katika muda usiozidi saa 96.

Waziri Mkuu Kasim Majaliwa.

Kituo hicho cha kimataifa cha mabasi cha Ngangamfumuni ni mradi mkakati uliopitishwa na Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) na kutengewa Sh. bilioni tisa.

Majaliwa alishangazwa na hali hiyo juzi, baada ya kutembelea na kukagua mradi huo.

Kutokana na wizi huo, Waziri Mkuu alisema Serikali inaweza kusitisha kutoa fedha za ujenzi wa mradi huo endapo matukio ya wizi wa vifaa vya mradi huo utaendelea.

Akiwa katika eneo hilo, Waziri Mkuu alimpa siku nne Kamanda wa Polisi mkoa wa Kilimanjaro, Hamisi Issah, kuhakikisha anawakamata walinzi waliokuwa wakilinda mradi huo na endapo atashindwa amkamate mmiliki wa kampuni ya ulinzi iliyopewa zabuni ya ulinzi.

Alisema Serikali imekuwa na utaratibu wa kutenga fedha na kuzipeleka katika halmashauri nchini ili kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo ambapo manispaa ya Moshi ilipambana kuona mabasi yanapata stendi baada ya kuona iliyopo haikidhi matakwa na kubuni ujenzi wa stendi ya Sh. bilioni tisa.

Aidha, alisema kituo hicho cha mabasi kitakuwa stendi ya mfano kitakapokamilika kutokana na ramani yake ilivyo.

Majaliwa alisema wakati Serikali ikipambana kuleta fedha ya mradi huo, wananchi wa Moshi wamekuwa wakiiba vifaa vya ujenzi wake na kudai kuwa nondo tani tano zimeshaibiwa.

“Haiwezekani mwananchi akatoka Lindi na kuja kuiba hapa Moshi, ni nyie wenyewe wananchi wa Moshi mmekuwa mkiiba vifaa vya mradi huo na kuanza kuuhumuju mradi huu,” alisema Majaliwa.

Alisema ni jambo la fedheha na linalokatisha tamaa kuona Serikali ikileta fedha kwa ajili ya maendeleo, lakini wananchi wanaondoka na mawe pamoja na nondo.

Aliongeza nondo hizo tani tano zilizoibwa hazikutoka hivi hivi bali wahusika walikuja na winji ya kupakilia na kuitega na kuanza kupakia na sio kwamba walichukua mojamoja, na kueleza kuwa serikali imesononeka na wizi huo na kuwa wanapoelekea siko kabisa.

Aidha Waziri Mkuu alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Kippi Warioba, kuhakikisha anawachukulia hatua wale wote waliobainika kuhusika na wizi huo.

“Hawa waliofanya wizi huu malengo yao sio mazuri, wanataka tukwame tusiwe na kituo cha mabasi halafu mabasi yaendelee kusongamana pale kati kati ya mji …kwanza pale eneo ni dogo na sisi lengo letu mabasi madogo ndio yabaki katikati ya mji,” alisema Majaliwa.

Kwa mujibu wa Majaliwa, hali hiyo ya wizi ikiendelea Serikali haitasita kusitisha ujenzi wa mradi huo na fedha hizo kupelekwa sehemu nyingine ambapo watu wanasubiria fedha ili kupeleka maendeleo.

Aliwataka wananchi kila mmoja kuwa mlinzi wa mwenzake na pindi wanapoona mtu anaiba kifaa chochote katika mradi huo kutoa taarifa kwa jeshi la polisi au watoe taarifa kwa kiongozi wa Serikali.

Kamanda Issah alisema nondo zilizokuwapo zilipatikana katika nyumba moja iliyopo jirani na eneo la ujenzi wa mradi huo.

Habari Kubwa