Sababu 4 mafao sasa kuahirishwa

03Dec 2018
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Sababu 4 mafao sasa kuahirishwa

KANUNI mpya za Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya mwaka 2018 zimebainisha sababu nne za mafao ya mwanachama wa mfuko kuahirishwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi ya Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dk. Irene Isaka.

Kwa mujibu wa kanuni hizo, mwanachama aliyechangia kwa miaka 15 anakuwa ametimiza masharti ya kupata malipo ya mkupuo.

Hata hivyo, kanuni hizo zimeweka masharti ya kuahirishwa kwa mafao ya mwanachama husika ikiwa kutakuwa na sababu nne, ikiwa ni pamoja na mwanachama husika kuacha kazi na kuchaguliwa kushika nafasi ya kisiasa.

Kanuni ya 12 inaeleza kuwa mwanachama aliyechangia kwa miezi 180, yaani miaka 15 na yupo chini ya umri wa kustaafu, kutakuwa na sababu nne za kuzingatiwa kuahirisha pensheni yake.

Mbali na kuchaguliwa kwenye nafasi ya kisiasa, sababu nyingine ni kupunguzwa kazi, mabadiliko ya muundo wa taasisi na kufutwa kwa ofisi.Kanuni hiyo imebainisha kuwa jambo hilo likijitokeza, mwanachama atalipwa kwa mujibu wa Kanuni ya Nane (8) malipo ya mkupuo na kisha kulipwa pensheni ya mwezi pindi atakapofikisha umri wa kustaafu.

Kanuni hiyo (ya 8) imeweka bayana kikokotoo kuwa ni moja ya 580 mara jumla ya miezi ya uchangiaji mara mishahara minono ya miaka mitatu katika miaka 10 ya mwisho kabla ya kustaafu mara 12.5 mara asilimia 25.

12.5 ni umri wa makadirio ambao mwanachama ataishi baada ya kustaafu na imewekwa kwenye kikokotoo kwa ajili ya kurahisisha ukokotoaji.Moja ya 580 ni faida ya uwekezaji inayofanywa na mfuko kwa kutumia fedha ya mwanachama.

Akizungumza na Nipashe jana, Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi ya Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Dk. Irene Isaka, alisema mwanachama wa kundi hilo analipwa malipo ya mkupuo yake kwa asilimia 25.

Alisema asilimia 75 itaendelea kubaki kwenye mfuko hadi afikishe umri wa kustaafu kwa mujibu wa sheria ambao ni miaka 55 kwa hiyari na miaka 60 kwa lazima, lakini kwa kada maalum kama vile madaktari na maprofesa umri wa kustaafu ni miaka 60 kwa hiyari na 65 kwa lazima.

"Tunawahamasisha waendelee kuchangia badala ya kuzichukua, lakini kama hataki atapewa asilimia 25 yake na hata akitaka kuendeleza michango hatakatazwa," alisema Dk. Isaka.

Alisema kwa mwanachama ambaye atapunguzwa kazi, anaweza kuingia katika fao la upotevu wa ajira au kupewa asilimia 25 ya mkupuo na asilimia 75 ya kila mwezi kuanza kuipokea baada ya kufikisha umri wa kustaafu.

Kwa fao la upotevu wa ajira, Dk. Isaka alisema mwanachama atapewa asilimia 33.3 kwa kulipwa mashahara kwa miezi sita hadi 18, na iwapo muda huo utaisha hajapata kazi, atatakiwa kuingia kwenye uchangiaji wa hiari baada ya kumwandikia mkurugenzi mkuu wa mfuko husika.

Mkurugenzi huyo alieleza kuwa kundi la waliokumbwa na mabadiliko ya muundo wa taasisi na ikaonekana kuwa kutokana na mabadiliko husika hawezi kuendelea kufanya kazi kwa maana ya nafasi zao kufutwa na hawajafikisha umri wa kustaafu, watalipwa asilimia 25 ya mkupuo.

Alisema kuwa iwapo mwanachama husika ofisi yake itafutwa, naye ataingia kwenye mfumo wa kulipwa mkupuo wa asilimia 25 na asilimia 75 inayobaki italipwa kama mshahara wa mwezi baada ya kufikisha umri wa kustaafu.

Kanuni mpya zenye kikokotoo kipya zilianza kutumika Agosti Mosi, mwaka huu baada ya kufanyika marekebisho ya Sheria ya Hifadhi ya Jamii na kuunda Mfuko wa PSSSF ambao unahudumia sekta ya umma na Mfuko wa NSSF unaohudumia sekta binafsi. PSSSF umeunganisha mifuko ya PSPF, GEP, PPF na LAPF. 

 

 

Habari Kubwa